The House of Favourite Newspapers

FUNDI NGUO ALIYEVUTA MKOKO KWA KUMSHONEA WEMA

Wema Sepetu.

MAISHA ni kama karata, ukijua kuzichanga na kucheza vizuri na Mungu akashusha baraka zake, hakika utafurahia matunda ya mikono yako.  Kijana Kenneth Ndunguru, mkazi wa Salasala jijini Dar ni kati ya watu walioweza kufaidika kwa muda mchache kupitia mgongo wa mrembo wa Bongo Movies, Wema Sepetu.

Alizichanga karata zake vizuri, akakutana na mrembo huyo na akaweza kumshonea nguo mbalimbali ambazo zimemwezesha kununua mkono aina ya Toyota Alteza wenye thamani ya shilingi milioni 12. Hadi sasa, fundi huyo ameshamshonea Wema zaidi ya nguo 50 ambazo kila anapovaa au anapoonekana kwenye kumbi mbalimbali za sherehe anamwagiwa sifa nyingi na mwisho wa siku kila mtu anataka amuelekeze ni wapi aliposhonea nguo hiyo.

ALIKUTANA VIPI NA WEMA?

Fundi huyo ambaye awali alikuwa akishona nguo zake kwa watu wa kawaida kabisa kiasi cha kufikia wakati mwingine kukosa hata uhakika wa kula, alijuana na staa huyo kupitia mbunifu wa mavazi anayeitwa Elisha ambaye alikuwa akimbunia Wema mavazi.

Kila alipokuwa akipata mshono mbunifu huyo alikuwa akimpelekea fundi huyo, anashona na kila nguo aliyokuwa akivaa Wema, inapendwa. “Unajua mimi nilikuwa namshonea lakini mwanzo nilikuwa sionani naye kabisa, niliyekuwa na mawasiliano naye ni mbunifu wake lakini kuna siku mwenyewe alinitafuta na ndipo tulipoanza kujuana kwa ukaribu zaidi.”

ALIMTAFUTA MIAKA 2 ILIYOPITA

Fundi huyo anaeleza kuwa wakati alipokuwa anashona alitamani sana kumshonea nguo moja staa huyo na alijua wazi ipo siku ataipenda lakini aliitafuta namba yake na kujaribu kumtumia mishono mbalimbali hakuweza kupata jibu lolote kutoka kwake hivyo alikata tamaa kabisa lakini Mungu mkubwa akaweza kumpata kwa njia tofauti ambapo sasa hivi humuelezi kitu Wema kwa jinsi anavyomkubali fundi huyo.

“Sikujua kama ipo siku nitaweza kuonana naye uso kwa uso kwa sababu ni mtu ambaye nilipenda sana kufanya naye kazi nikiamini angeweza kuniinua na kipaji changu kingeonekana.”

APATA NDINGA

Fransic anasema kuwa baada ya kuanza kumshonea staa huyo nguo kwa kipindi cha miezi 2 tu ameweza kumiliki usafiri wake mwenyewe aina ya Alteza, kitu ambacho hakuwa na ndoto nacho kwa siku za hivi karibuni lakini kimetimia kwa kushona nguo za Wema.

ALIJIFUNZIA WAPI KUSHONA

Fundi huyo anasema kuwa elimu hiyo ya ushonaji alijifunza akiwa Songea tena kwa fundi tu wa kawaida, alipokuja Dar alikuwa akinunua nguo za mitumba na kuanza kuangalia walivyoshona mpaka sasa ndio ameweza kujua kila kitu kuhusiana na ushonaji.

GHARAMA ZAKE ZIKOJE?

Akizungumzia gharama zake kwa mastaa anaowashanea nguo anasema inategemea na mshono maana anaanzia laki tano kwenda juu. “Kama nguo haihitaji vitu vingi gharama yake sio kubwa sana lakini kuna wengi ambao unakuta vitambaa vyao ni vya juu hivyo na gharama inaongezeka kidogo.”

MASTAA ANAOWASHONEA NGUO

Francis anasema kuwa amepata bahati ya kuwashonea mastaa wengine kupitia Wema, kama Aunt Ezekiel, Zamaradi na Sanchoka ambao kila mmoja akivaa nguo alizoshona wanapendeza.

WEMA ANAMZUNGUMZIAJE FUNDI HUYO

Wema baada ya kuulizwa kwamba ni kitu gani kilimvutia kwa fundi huyo alisema kuwa, tangu aanze kushona nguo kwa mafundi mbalimbali hajawahi kushonewa vizuri kama anavyoshonewa na Kenneth hivyo hawezi kumuacha.

“Mimi nimezunguka kwa mafundi wengi sana, hakuna aliyezima kiu yangu lakini kwa Kenneth sijui ni wapi tena nitaenda, nina nguo nyingi sana nimeshona kwake na kila nguo lazima ipendwe. Lakini pia mimi sipendagi usumbufu wa mafundi ila kwa huyu nikitaka leo atanipa leo,” anasema Wema.

Makala: Imelda Mtema

Comments are closed.