The House of Favourite Newspapers

Furaha Ya Mashabiki Simba, Yanga Ipo Kwenye Usajili Wa Kutunishiana Misuli

1

BURUDANI ya soka kwenye nchi yetu imegawanyika katika makundi tofauti kulingana na matakwa ya wanaohitaji, wapo wanaoburudika kwa matokeo ya uwanjani pekee.

Kundi hili la mashabiki hupenda kuona timu wanayoishabikia ikipata ushindi kwa kila mechi inayocheza bila kujali kama ushindi huo unapatikana kwa dhuluma au kihalali. Mara zote kundi hili ndilo linalosababisha kuwepo na vurugu viwanjani kwa kuvamia uwanja, kurusha chupa na kuporomosha matusi kwa mwamuzi au wachezaji wao wanaoonekana kuboronga pengine kwa bahati mbaya.

Utakubaliana nami kwamba tumeshuhudia pia uharibifu mkubwa wa miundombinu ya uwanja ukifanywa kwa makusudi na mashabiki wa kundi hili ambalo linafahamika kama ‘mashabiki hoyahoya’ waliokosa hata chembe ya ustaarabu. Binafsi naamini mashabiki wa kweli wa soka huwa na mioyo ya uvumilivu kila wakati kwa kwenda sambamba na falsafa ya matokeo matatu ya mpira ambayo ni kufungwa, kushinda na kutoka sare.

Hebu turudi sasa kwa wale wanaopata burudani ya usajili kwenye klabu zao, kundi hili kinapofika kipindi cha usajili wao hujikuta wakifarijika kupita kiasi kila wanaposikia taarifa mpya ya usajili unaofanyika.

Kama ujuavyo Klabu za Yanga na Simba ndizo pekee zilizobahatika kujizolea umati mkubwa wa wafuasi na mashabiki kwa nchi nzima na kufanikiwa kutengeneza utani wa jadi miongoni mwao bila kujali itikadi za dini wala kabila. Kwa hali hiyo mashabiki hawa hupenda kuona kila lililo jema likifanyika upande wao, na yale mabaya yakitokea upande wa pili hasa katika usajili wa wachezaji wazuri wanaowaita ‘vifaa’.

Mashabiki wa Yanga na Simba kinapofika kipindi cha usajili, hujawa na matumaini makubwa kwa viongozi wao na kujikuta wanasahau kabisa hata yale matatizo na mivutano iliyopo ndani ya klabu zao. Usahaulifu huo wa mivutano ndani ya klabu huwa unadumu kwa muda mfupi kwani baada ya zoezi la usajili kumalizika, purukushani zinarejea mahala pake na maisha yanaendelea.

Kama ujuavyo usajili unaofanywa na Klabu za Yanga na Simba hasa kwa wachezaji wa kigeni huwagharimu kiasi kikubwa cha fedha, kwa hiyo klabu mojawapo inapoyumba kiuchumi inakuwa ni burudani kwa upande wa pili ambapo unakuwa unaamini kwamba timu yao itakuwa bora kuliko wenzao.

Wakati mwingine hutokea klabu hizi zinagombania mchezaji fulani ambaye anasemekana ni moto wa kuotea mbali, hapo ndipo utaona purukushani za viongozi zikishika hatamu kwa kuzunguka huku na kule kuhakikisha wanainasa saini yake. Purukushani hizo wakati zikiendelea, mashabiki hupata burudani ya aina yake wakishuhudia jinsi viongozi wao wanavyotunishiana misuli kwa nguvu ya fedha.

Yote tisa kumi ni vizuri klabu zikasajili kulingana na upungufu katika vikosi vyao, zisiangalie wapinzani wao wamemsajili nani ili na wao walipize hapana, soka haliendi hivyo kwani ni lazima mtapoteana tu kwenye ligi kwa kuwa hamkuzingatia matakwa ya benchi la ufundi. Usajili fanyeni lakini mkumbuke kuwa mkikosea sasa basi mtakuwa mmekosea msimu mzima ambao utakuwa na mechi 30 kwa kila timu, sajilini salama na epukeni ajali ya kupewa wachezaji wa benchi.

OMARY KATANGA , CHAMPIONI

1 Comment
  1. […] muundo rejeshi. Katika sehemu ya kwanza na ya pili, anatuonesha mahali yanapofanyika mazishi ya Furaha. Sehemu ya tatu na 20 anatuonesha juu ya maisha ya Furaha mpaka kifo […]

Leave A Reply