The House of Favourite Newspapers

Fursa Kubwa Yanukia Kwa Waandaaji wa Filamu Afrika Mashariki

0
WAANDAAJI wa filamu wa Afrika Mashariki hususani waandishi wa miswada (script writters) watanufaika na mpango maalum ulioandaliwa na Taasisi ya Realness kwa ajili ya kuwapa mafunzo waandaaji wa filamu kutoka barani Afrika ambapo watapata fursa ya kusafiri na kwenda kujifunza zaidi katika nchi za Nigeria, Afrika Kusini na Uswisi.
Waandaaji hao wa filamu kutoka Afrika Mashariki, watashindanishwa ambapo watakaoingia nafasi ya Sita Bora, ndiyo watakaopata nafasi ya kushiriki kwenye mafunzo yatakayofanyika katika nchi hizo tatu katika awamu ya saba ya mafunzo hayo yanayotarajiwa kufanyika kuanzia Agosti 3 hadi Novemba 13, 2022.
Habari njema katika mafunzo ya mwaka huu, ni kwamba Taasisi ya Realness inashirikiana na na Chuo cha Locarno Filmmakers’ Academy cha nchini Uswisi na kuwapa fursa wote watakaokidhi vigezo, kwenda kushiriki katika maonesho ya filamu ya Locarno Film  Festival pamoja na kuhudhuria mafunzo maalum yanayoendeshwa na chuo hicho maarufu kama BaseCamp.
Watu sita wenye bahati watakaokidhi vigezo, watakaa kwa muda wa wiki sita katika vituo vya kukuza vipaji vya Nirox na Farmhouse 58 vilivyopo nchini Afrika Kusini na kupata nafasi ya kunolewa na wakufunzi waliobobea; Selina Ukwuoma, Mmabatho Kau na Cait Pansegrouw.
Baada ya kumaliza mafunzo, Mkurugenzi wa Taasisi ya Realness, Elias Ribeiro atasafiri na washiriki hao mpaka nchini Uswisi katika Tamasha la Locarno Film Festival huku Mehret Mandefro ambaye ni Mkurugenzi wa Maendeleo wa Realness, ataongozana na washiriki hao mpaka nchini Nigeria watakapoenda kushiriki katika maonesho ya kimataifa ya filamu ya Africa International Film Festival (AFRIFF).
Wakiwa nchini Nigeria, washiriki hao watakaa kuanzia Novemba 7 hadi Novemba 13 ambapo mbali na kuhudhuria maonesho ya AFRIFF jijini Lagos, pia watakutanishwa na wadau mbalimbali wa filamu nchini humo kwa ajili ya kujifunza masuala yahusuyo uandaaji wa filamu.
Kwa watakaopenda kushiriki, tayari maombi kwa njia ya mtandao yamefunguliwa kupitia Taasisi ya Realness Institute ya nchini Afrika Kusini ambapo waandaaji kutoka sehemu mbalimbali barani Afrika, hususani Afrika Mashariki wanaruhusiwa kufanya maombi.
Tovuti ya kutuma maombi ya kushiriki ni https://www.realness.institute/realness-residency na kwamba mwisho wa kutuma maombi ni Machi 7, mwaka huu.
Leave A Reply