The House of Favourite Newspapers

Fursa kwa Wahitimu Kidato cha Nne Waliofauru Sayansi

WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amewaagiza watendaji wa wizara hiyo kwa kushirikiana na Baraza la Taifa la Vyuo vya Ufundi nchini (NACTE) kuhakikisha wanawachukua wanafunzi wa kidato cha nne waliofaulu katika masomo yao ikiwemo mchepuo wa sayansi ili kuongeza udahili katika vyuo vya uuguzi nchini sanjari na kupunguza tatizo la uhaba wa watumishi wa afya.

 

Akizungumza katika ufunguzi wa majengo ya Chuo cha Uuguzi Tanga yaliyojengwa kwa msaada wa ufadhili wa mfuko wa dunia wa kupambana na UKIMWI,Kifua Kikuu na malaria kwa gharama ya zaidi ya shilingi bil 3.5, Waziri Ummy amesema wanafunzi wengi wanafaulu lakini wanakosa nafasi kwa sababu ya uchakavu wa miundombinu ya majengo hivyo ni jukumu lao kutumia fursa hiyo kwa lengo la kupunguza uhaba wa watumishi wa afya.

 

Katika zoezi hilo, mwakilishi wa mfuko wa Dunia wa kupambana na UKIMWI, kifua kikuu na malaria Itruda Temba amesema tangu kuanzishwa kwa mradi huo nchini, serikali imenufaika baada ya kupunguza magonjwa makuu ya kuambukiza ikiwemo UKIMWI kutoka asilimia 10% hadi kufikia 4.7%.

 

Kufuatia hatua hiyo mkuu wa mkoa wa Tanga Martin Shigella ameiomba wizara hiyo kutumia fursa hiyo kuongeza idadi ya watumishi wa kada ya afya katika wilaya nane za mkoani humu kufuatia changamoto mbali mbali zinazojitokeza kwa sababu ya tatizo hilo.

Comments are closed.