The House of Favourite Newspapers

Giroud Atafunga Sana Chelsea

Mshambuliaji mpya wa Chelsea, Olivier Giroud.

 

MCHEZAJI ambaye amekuwa gumzo kwenye kipindi hiki cha usajili basi ni mshambuliaji mpya wa Chelsea, Olivier Giroud.

 

Huyu ni mchezaji ambaye hakuwa kipenzi kwa mashabiki wa timu ya Arsenal kwa kile ambacho walikuwa waamini kuwa alikuwa akipoteza nafasi nyingi za kufunga mabao.

 

Giroud raia wa Ufaransa ni kati ya washambuliaji ambao wameonyesha uwezo mkubwa kwenye michezo mingi ambayo amecheza kwenye Ligi Kuu England kuanzia alipojiunga na timu hiyo ya London.

Juzi Jumatatu mshambuliaji huyo alifanikiwa kuichezea Chelsea kwenye mchezo wake wa kwanza kuanzia alipojiunga nayo ambapo alionyesha kiwango cha juu.

Mshambuliaji huyo mara baada ya kukamilisha dili lake la kujiunga na timu hiyo, alisema kuwa alikuwa anaweza kuwania namba kwenye kikosi cha Arsenal lakini baada ya kuona kocha wa timu hiyo Arsene Wenger anasajili mshambuliaji mwingine alifahamu kuwa muda wake wa kuondoka hapo umefika.

 

Anasema mbali na kuwania namba, lakini kocha wa timu ya taifa ya Ufaransa Didier Deschamps, alishamweleza kuwa kama anataka kucheza fainali za Kombe la Dunia mwakani basi aondoke kwenye timu hiyo.

Giroud anaaminika kuwa anaweza kuisaidia timu ya Chelsea kutawala kwenye Ligi Kuu England msimu huu na misimu mingine ijayo kutokana na staili yake ya kupambana.

Chelsea walimsajili mshambuliaji kwa kitita cha pauni milioni 18, siku ya mwisho kabisa ya usajili.

Inaaminika kuwa staa huyo atapata nafasi kwenye timu hiyo kwa kuwa kwa sasa Alvaro Morata anasumbuliwa na majeraha, lakini pia staa aliyekuwa anasubiri kwenye benchi Michy Batshuayi yeye ameshaondoka na kujiunga na Borussia Dortmund.

Chelsea wamekuwa wakihitaji wachezaji warefu kwenye kikosi chao kutokana na aina ya soka wanalocheza la kushambulia kwa mipira ya juu.

Awali Giroud alikuwa akiwania nafasi na mastaa warefu Andy Carroll, Peter Crouch, Edin Dzeko na Ashley Barnes hali ambayo inaonyesha kuwa kocha huyo amemsajili mchezaji ambaye anamtaka.

 

Rekodi zinaonyesha kuwa Arsenal wanaweza kujuta haraka zaidi kwani mshambuliaji huyo anashika rekodi ya kufunga mabao 27 kwa kichwa kwenye michezo ya Ligi Kuu ya England akiwa ndiye kinara wa kufunga mabao kwa vichwa kwenye ligi hiyo.

Mshambuliaji huyo ana urefu wa futi sita na inchi nne akiwa na umri wa miaka 31 tu kwa sasa kwenye ligi hii.

Inaaminika kuwa pasi za mastaa wa timu hiyo Marcos Alonso, Victor Moses na Davide Zappacosta, wachezaji hawa wameifanya Chelsea kuwa timu inayoshika nafasi ya pili kwa kupiga krosi nyingi hadi sasa kwenye ligi hiyo wakiwa wamepiga krosi 393.

Giroud anakwenda kwenye timu yake mpya akiwa hana presha sana hata kama atakosa nafasi kwenye kikosi cha kwanza kwa kuwa tayari anashika nafasi ya kwanza kwa mchezaji aliyefunga mabao mengi akitokea kwenye benchi baada ya kuwa na mabao 17 hadi sasa.

 

Hata hivyo, inaaminika kuwa uzoefu wake unaweza kuisaidia timu hiyo ya London kwa kuwa hadi sasa ameshacheza michezo 180 kwenye Ligi Kuu England akiwa amecheza kwa miaka mitano na nusu kwenye ligi hiyo.

Staa huyo ambaye alijiunga na Arsenal mwaka 2012, alifanikiwa kuichezea timu hiyo michezo 253 na kufunga mabao 105, lakini jumla amecheza michezo 464 na kufunga mabao 196 kwenye timu sita alizozichezea.

Pia amefanikiwa kuitumikia timu ya taifa ya Ufaransa kwenye michezo 69 na kufunga mabao 29.

Comments are closed.