The House of Favourite Newspapers

Global Publishers Yazindua ‘Jipange na Pepa’

 

Aziz Hashim (Katikati), akizungumza na wanafunzi, walimu na waandishi wa habari kwenye uzinduzi huo. Kulia ni Kennedy Mlawa na Humphrey Humphrey, Maafisa wa Promosheni wa Global Publishers

KATIKA kuunga mkono juhudi za serikali kuboresha sekta ya elimu nchini, Kampuni ya Global Publishers inayochapisha magazeti ya Uwazi, Ijumaa, Ijumaa Wikienda, Risasi, Amani, Championi na Spoti Xtra, imezindua mradi mpya uitwayo ‘Jipange na Pepa’ unaolenga kuwaandaa wanafunzi wa sekondari katika mitihani yao ya mwisho.

Akizungumza katika uzinduzi wa mradi huo leo Novemba 5, 2019 katika ofisi za kampuni hiyo jijini Dar es Salaam, Mratibu kiongozi wa mradi huo, Aziz Hashim amesema katika kila toleo la magazeti pendwa ya kampuni hiyo, kutachapishwa mitihani ya masomo mbalimbali iliyoandaliwa na jopo la walimu wazoefu.

Hashim akionesha ukurasa wenye mitihani ndani ya Gazeti la Uwazi.

Alisema jopo hilo la walimu ambao pia wana mbinu bora za ufundishaji na utungaji wa mitihani, watakuwa wakitunga mitihani ya masomo mbalimbali kwa kuzingatia mfumo wa mitihani ya Taifa ya kidato cha pili na cha nne inayoandaliwa na Baraza la Mitihani nchini (NECTA).

Alisema maswali yatakuwa yanachapishwa kwenye Magazeti Pendwa kuanzia Jumatatu mpaka Jumamosi, huku majibu ya kila mtihani yakitolewa kwenye toleo linalofuatia la gazeti husika.

“Hii itawasaidia wanafunzi kuizoea mitihani, kuelewa namna maswali yanavyoweza kutungwa kutokana na ‘topic’ walizozisoma na kuelewa maeneo ambayo maswali huwa yanatoka zaidi.

“Lakini pia itawasaidia walimu, hasa kwenye zile shule zenye walimu wachache ambapo kwa kutumia mitihani itakayokuwa inachapishwa, watakuwa na uwezo wa kuwapima wanafunzi wao kwa urahisi na kuangalia maeneo ambayo yana udhaifu,” alisema.

Kwa upande wake Meneja Usimamizi wa promosheni za bidhaa za kampuni hiyo, Kenedy Mlawa  alisema mradi huo utawasaidia hata wazazi wanaozingatia maendeleo ya watoto wao ambapo kwa kutumia mitihani itakayokuwa inachapishwa, watakuwa na uwezo wa kuwasimamia watoto wao waifanye, kisha baada ya hapo wanasubiri toleo linalofuata kutazama majibu na kupima uelewa wa watoto wao.

Baadhi ya walimu, wanafunzi na wafanyakazi wa Global Group wakiwa katika picha ya pamoja

Naye Mratibu msaidizi wa mradi huo, Humphrey alisema masomo yatakayoangaziwa na majina ya magazeti husika ni pamoja na; BIOLOGY (Ijumaa Wikienda linalotoka siku ya Jumatatu), GEOGRAPHY (Uwazi, Jumanne), MATHEMATICS (Risasi Mchanganyiko, Jumatano), ENGLISH, KISWAHILI (Amani, Alhamisi), HISTORY, CIVICS (Ijumaa) na PHYSICS, CHEMISTRY (Risasi Jumamosi).

Alisema kwa siku ambazo zina masomo mawili, walimu watakuwa wakitunga mitihani ya masomo hayo kwa kubadilishana kwa lengo la kuhakikisha kila somo linapata nafasi ya kutosha.

Baadhi ya walimu wakiwa katika picha ya pamoja na mratibu wa Jipange na Pepa Project, Aziz Hashim

Kwa ufafanuzi zaidi, endelea kusoma magazeti ya Global Publishers, tembelea mtandao wa Global Publishers au unaweza kupiga simu namba 0719401968 kwa maelezo zaidi! Jipange na Pepa!

Aidha, mmoja wa walimu wanaoandaa mitihani hiyo, Nassoro Ramadhani alisema mradi huo umekuja wakati muafaka katika kuwasaidia wanafunzi wenye uhaba wa walimu kuwa na uwezo wa kuelewa namna ya kujibu maswali hata yale ambayo hawajafundishwa.

Pia mmoja wa wanafunzi waliohudhuria hafla hiyo kutoka kituo cha elimu Mapambano, Malima Julius alisema mfumo huo utawasaidia wanafunzi kuondoa hofu ya mitihani kwa sababu utawaongezea uzoefu wa kujibu mitihani kwa urahisi zaidi.

NA GABRIEL MUSHI

Comments are closed.