UONGOZI wa timu ya soka ya Gor Mahia ya Kenya, umeitaka Simba kutuliza mzuka katika harakati zake za kumwania kiungo wao mshambuliaji, Francis Kahata.
Simba inadaiwa kuwa katika harakati za kumwania mchezaji Kahata, baada ya kuvutiwa na uwezo wa juu aliouonyesha katika michuano ya SportPesa iliyofanyika nchini Kenya hivi karibuni na Gor Mahia kuibuka mabingwa wa michuano hiyo.
Habari za kuaminika kutoka ndani ya Simba ambazo Championi Jumatatu limezipata zimedai kuwa uongozi wa Gor Mahia umewaambia Simba kuwa utawapatia mchezaji huyo mwezi Desemba kama kweli wanamtaka lakini siyo hivi sasa.
Sababu kubwa ya kufanya hivyo ni kwamba bado wanaihitaji huduma yake kwa ajili ya michuano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho Afrika ambayo timu hiyo inashiriki na ipo kundi moja na Yanga.
“Juhudi zetu na kumsajili Kahata bado tunaendelea nazo lakini Gor Mahia wamekuwa wagumu sana kumwachia na wametuambia kuwa bado wanahitaji huduma yake katika michuano ya kimataifa.
“Wametuambia kuwa kama tunamtaka kweli basi wao watamwachia mwezi Desemba mwaka huu, lakini kwa sasa itakuwa ni ngumu,” kilisema chanzo hicho cha habari na kuongeza kuwa bado wanaendelea kupambana ili kuona kama watafanikiwa kumpata kabla ya ligi kuanza.
Hata hivyo, baadhi wa viongozi wa Simba walipoulizwa kuhusiana na suala hilo, hawakuwa tayari kusema chochote zaidi ya kudai kuwa anayeweza kulizungumzia hilo ni kaimu rais wa klabu hiyo, Salim Abdallah ‘Try Again’ ambaye ndiye amekuwa akisimamia shughuli zote za usajili klabuni hapo lakini alipotafutwa simu yake ya mkononi iliita muda mrefu bila ya kupokelewa.
Sweetbert Lukonge, Dar es Salaam
Comments are closed.