The House of Favourite Newspapers

The Graves of The Innocents (Makaburi ya Wasio na Hatia)- 19

0

ILIPOISHIA:

MARA mlango wa wodi ulifunguliwa, daktari mmoja akachungulia nje na kuwaonesha ishara ya kuwaita baba na baba yake Rahma, mapigo ya moyo wangu yakalipuka mno, sikujua anaenda kuwaambia nini, akilini nikawa nahisi kabisa kwamba mambo yameshaharibika.

SASA ENDELEA… “Kuna tatizo.” “Nini tena daktari?” “Mgonjwa wenu anaishiwa damu kwa kasi kubwa mno, isitoshe anatapika damu, hatujui tatizo ni nini kwani vipimo havioneshi tatizo lingine lolote zaidi ya kwamba alikunywa sumu kwa lengo la kujiua.”

“Sasa tutafanyaje dokta?” “Inabidi kwanza tushughulikie hili suala la kupungukiwa damu, inabidi wanandugu muitane kwa ajili ya kuchangia damu, mkiwa tayari mniambie ngoja nizungumze na watu wa kitengo cha damu waandae vifaa,” alisema yule daktari na kuingia wodini, nikawaona baba na baba yake Rahma wakitazamana.

“Nahisi kuna nguvu za giza nyuma ya hili suala na kama tusipotumia nguvu za ziada, tunaweza kumpoteza binti yetu,” alisema baba, mwenzake akawa anatingisha kichwa kuonesha kuunga mkono alichokuwa anakisema. “Mimi nina wazo, unaonaje tukiondoka na mgonjwa wetu tukamtibu nyumbani. Kuna kitu tukikifanya mara moja anapona huyu.”

Nilishangazwa sana na uamuzi walioufikia, yaani mgonjwa ana hali mbaya kiasi kile halafu wamuondoe hospitali na kwenda naye nyumbani? Akifa je? Nilijiuliza bila kupata majibu. Muda mfupi baadaye, baba aligonga tena mlango wa wodi, yule daktari akafungua mlango kwa lengo la kusikiliza walichokiamua. “Mmeshakubaliana kuhusu kuchangia damu?”

“Hapana, imani yetu hairuhusu kuchangia damu, tunamuomba mgonjwa wetu tuondoke naye tukajaribu sehemu nyingine,” alisema baba kwa kujiamini, nikamuona yule daktari akiwatazama wote wawili usoni kwa mshtuko. “Ndivyo mlivyokubaliana?”

 

“Ndiyo,” alisema baba, nikamuona akishusha pumzi ndefu na kuonesha ishara kwamba wasubiri, akaingia ndani nadhani kwa lengo la kwenda kujadiliana na wenzake, muda mfupi baadaye alipotoka, aliwaambia madaktari wenzake wamekataa wazo hilo, wakawaambia afadhali kama wangekuwa wanaomba rufaa kwenda hospitali kubwa lakini kama ni kumrudisha nyumbani, hilo suala haliwezekani.

“Hawa washenzi sana, kwa hiyo wanaamini hatuwezi kumchukua mgonjwa wetu bila ridhaa yao?” alisema baba huku akimshika mkono baba yake Rahma na kuondoka naye, walitoka mpaka nje kabisa ya eneo la hospitali. Nilikuwa na shauku kubwa ya kumsaidia Rahma, nilipohakikisha akina baba wametoka nje, na nilipowatazama mama na mama Rahma kwa mbali ambao walikuwa wakibembelezana pale kwenye

benchi, harakaharaka nilitembea kuelekea kule wodini. “Unasemaje kijana?” “Huyu ni dada yangu, nataka kumtolea damu.” “Ooh! Umefanya jambo la maana sana, twende huku,” alisema yule daktari huku akinishika mkono, tukatoka wodini na kuanza kutembea harakaharaka kwenye korido, tukaelekea mpaka kwenye chumba maalum cha kutolea damu ambapo niliwakuta watu wengine watatu wakiwa wamekaa kwenye vitanda maalum, wakiwa wanajitolea damu.

“Kaa hapo,” alisema yule daktari huku akinionesha sehemu ya kukaa, akapitiliza na kwenda kuzungumza na mwenzake ambaye alikuwa bize akishughulika na mmoja kati ya wale watu waliokuwa wakitoa damu. Akazungumza naye kisha nikaona wote wawili wamegeuka na kunitazama. Muda mfupi baadaye, yule daktari alitoka na kuniaga, akaniambia nikishamaliza niende nikamuone. Alipotoka, yule daktari mwingine ambaye yeye alikuwa amevalia sare za rangi tofauti, alikuja pale nilipokuwa nimekaa, tukasalimiana kisha akaniuliza kama nilikuwa nataka kujitolea damu, nikamjibu kwamba ni kweli.

Alinisogelea na kuanza kunitazama kwenye mkono wangu wa kushoto, akachukua pamba iliyokuwa na spirit, akanipaka sehemu ya ndani ya mkono wangu kisha akanifunga kwa mpira maalum upande wa juu wa mkono, mishipa ikatokeza kwa wingi mkononi. “Huwa unafanya mazoezi?” aliniuliza.

Nilielewa kwa nini ameniuliza swali lile, kazi ngumu za kijijini, ikiwemo kulima na kupasua kuni zilinifanya mimi na ndugu zangu tuwe na nguvu sana mithili ya watu wanaonyanyua vyuma. “Hapana, ni kazi za kawaida tu,” nilimjibu, akatabasamu na kusema wanaume wengi huwa na miili legelege kwa hiyo linapokuja suala la kuchangia damu, inakuwa vigumu kuuona mshipa mkuu wa damu lakini kwangu mimi ulikuwa ukionekana vizuri na ulikuwa mkubwa kama mtu anayefanya mazoezi.

Nikamuona akichukua sindano moja nene iliyounganishwa na mrija kwa nyuma ulioenda hadi kwenye kibegi kidogo cha plastiki cha kuhifadhia damu. Kiukweli sikuwahi kuchomwa sindano hata mara moja kwenye maisha yangu, kule kijijini kwetu mtu ukiumwa zipo dawa za mitishamba kibao. Ukizingatia baba alikuwa mtaalamu wa mambo hayo, alikuwa akizijua dawa za magonjwa karibu yote. Hata hivyo, sikutaka kuonekana mshamba, ikabidi nijikaze kiume, akanichoma taratibu na kuiingiza ile sindano kwenye mshipa, akanifunga na

bandeji kwa juu kisha akafungua ule mpira, damu ikaanza kutiririka kwa kasi kufuata ule mrija mpaka kwenye kile kimfuko. “Mh! Hii damu yako ikoje?” alisema huku akikiinua kile kimfuko cha damu na kuanza kukitazama kwa karibu. Tofauti na damu za watu wengine mle ndani, yangu ilionesha kuwa nyeusi sana mpaka nikawa najishtukia.

“Ina nini kwani?”

“Ni nyeusi sana na inaganda humu kwenye huu mfuko, sijawahi kukutana na hali kama hii,” alisema huku akinitaka nitulie, akaenda kuwaita wenzake na muda mfupi baadaye, walinizunguka, kila mmoja akiwa ananishangaa. “Unaitwa nani?” “Togo.” “Umewahi kuchangia damu kabla ya leo?” “Hapana, leo ndiyo mara ya kwanza.” “Mbona damu yako iko hivi?” aliniuliza daktari mmoja, ikabidi amuelekeze yule aliyenichomeka ile sindano, harakaharaka wakanitoa ile sindano, wakawa wanaendelea kujadiliana kuhusu damu yangu.

“Tunaomba utusubiri pale nje tutakuita,” alisema yule daktari ambaye ndiye aliyenipeleka kwenye chumba kile, nikainuka huku na mimi nikiwa na maswali mengi kuliko kawaida, nikatoka huku nikiwa nimebana pamba pale kwenye jeraha la sindano ili damu isiendelee kutoka. “Ulikuwa wapi tunakutafuta huku?” baba alinidaka juujuu, macho yake yakatua kwenye pamba niliyokuwa nimeikandamiza pale kwenye jeraha la sindano.

 

“Na hiki ni nini?” alisema huku akinishika mkono kwa nguvu. “Nilikuwa natoa damu.” “Mungu wangu, hivi wewe mtoto una akili timamu kweli?” alisema baba huku akionesha kushtuka mno, akageuka na kumuonesha ishara baba yake Rahma kwamba aje, harakaharaka akaja mpaka pale tulipokuwa tumesimama.

Je, nini kitafuatia? Usikose next issue au tembelea Simulizi za Majonzi.

 

===

Usipitwe na Matukio, Download na Install ==> Global Publishers App

NA: MWANDISHI WETU NA MITANDAO| UWAZI JUMANNE

Maajabu ya Dunia! Mti Ukikatwa Upande Unatoa Damu, Upande Unatoa Utomvu

Leave A Reply