The House of Favourite Newspapers

The Graves of The Innocents (Makaburi ya Wasio na Hatia)- 57

ILIPOISHIA:

Ni kama fahamu zake zilikuwa zimemrejea kwani alishtuka sana kuniona ndani ya chumba chake, akageuka huku na kule huku akijaribu kujitoa kwenye mikono yangu kwa hofu kubwa.

“Togoo! Umeingiaje humu?” aliniuliza kwa sauti ya juu, nikasikia mlango wa chumba cha pili ukifunguliwa kuashiria kwamba kuna mtu alikuwa amesikia na sasa anatoka.

SASA ENDELEA…

“Nimekwisha!” nilijisema huku nikigeuka huku na kule, sikumuona baba wala baba yale Rahma, Sadoki akanibadilikia na kunishika kwa nguvu ii nisipate nafasi ya kukimbia.

Akili za haraka, zilinituma kutumia nguvu zangu kujiokoa na kwa kuwa nilikuwa na ile kinga yangu ya hirizi mkononi, nilipiga mguu wa kushoto chini huku nikiwa nimevibana vidole gumba na vile vya mwisho. Hii ni mbinu niliyofundishwa ya kutaka kupotea kwenye macho ya watu, yaani unakuwepo sehemu hiyohiyo lakini huonekani.

Nilipofanya hivyo, nilishtukia nikiwa mwepesi kama upepo, Sadoki akabaki ameduwaa kwani japokuwa alikuwa amenishika, alishtukia nikiyeyuka mikononi mwake, giza nene likatanda chumba kizima.

Mara mlango ulianza kugongwa kwa nguvu, Sadoki akaenda kuufungua maana alikuwa amefunga kwa komeo kwa ndani, mama yake Sadoki akaingia mbiombio akiwa ameshika kibatari.

“Una nini Sadoki?”

“Mama! Nimemuona Togo kwa macho yangu, hata sijui ameingiaje humu ndani wakati milango ilikuwa imefungwa.”

“Togo huyu rafiki yako? Wewe utakuwa unaota, Togo ataingiaje humu wakati milango yote imefungwa? Halafu mbona watu wenyewe hawapo hapa kijijini na hakuna anayejua walikohamia?” mama yake Sadoki alisema huku akionesha kumshangaa mwanaye.

“Kweli mama, nimemuona kwa macho yangu!”

“Kwanza umemuonaje wakati hukuwa umewasha kibatari? Acha kutushtua wenzako kwa sababu ya ndoto zako,” alisema mama yake Sadoki huku akimulika huku na kule kwa kibatari. Japokuwa nilikuwa mlemle ndani, hakuna aliyeniona, mwanamke huyo akawa anamtuliza mwanaye na kumwambia kwa kuwa wanalindwa na Mungu hakuna jambo lolote baya linaloweza kuwapata.

Japokuwa mama yake Sadoki aliamini kwamba mwanaye alikuwa ndotoni, mwenyewe aliendelea kushikilia msimamo wake na alipoona mama yake hamuamini, aliamua kunyamaza lakini mara kwa mara alikuwa akigeuka huku na kule, akionesha kuwa na hofu kubwa ndani ya moyo wake.

“Haya sogea huku tusali,” alisema mama yake Sadoki, akamshika mwanaye mikono, wote wakafumba macho. Kabla hata hawajaanza kusali, nilishtukia nikivutwa kwa nguvu kuelekea nje, kutazama vizuri kumbe walikuwa ni baba na baba yake Rahma, tukadondokea kwenye majani pembeni ya nyumba ya akina Sadoki, wote wakiwa wanahema kwa nguvu.

“Mpumbavu sana wewe,” alisema baba huku akinizabua kibao kwa nguvu, nikashangaa kwa nini ananipiga kwa sababu sikuwa nimefanya kosa lolote.

“Kwa nini hukumgeuza kinyumenyume kama wewe?” alisema baba kwa ukali, ni hapo ndipo nilipolitambua kosa langu. Wakati nikitoka na Sadoki, mimi ndiye niliyetanguliza mgongo lakini yeye alikuwa ameelekea nilipo mimi kwa sababu nilikuwa nimemshika mikono nikimvuta, hakutanguliza mgongo.

“Lakini hukuniambia hivyo baba,” nilisema huku nikiugulia maumivu makali ya kibao cha baba. Muda huo tayari walishaanza kusali, wakawa wanakemea na kutaja jina la Mungu kwa nguvu.

Ukweli ambao wengi hawaujui, ambao hata mimi mwenyewe nilikuwa siujui, hakuna sumu mbaya kwa jamii ya watu wa nguvu za giza, kama mtu anayesali na kumuamini Mungu kwa moyo wake wote, bila kujali ni wa dini gani.

Hapa nazungumzia wale watu ambao kweli wanafuatisha amri za Mungu, yaani kama ni Mkristo, awe anafuatisha yale yote aliyoagizwa na dini yake na kama ni Muislam vivyo hivyo.

Watu wa namna hii, huwa hawagusiki kabisa maana hata pale baba aliniambia kama wasingetumia nguvu za ziada kuingia na kunivuta kwa nguvu, maombi ya Sadoki na mama yake yangenidhuru vibaya sana na hata wao hawajui nini kingenipata.

Ila kitu ambacho nilikuja kujifunza baadaye, ambacho ningependa watu wengine wajue, kinga waliyonayo watu wanaomuamini Mungu, haiwahusu wale wanaosali kinafiki, kwamba ukifika kwenye nyumba za ibada unajifanya wewe ni mwema sana lakini kumbe ni mwizi, mwongo, mwasherati au unashinda kwa waganga wa kienyeji.

Ilibidi tuondoke haraka pale nyumbani kwa akina Sadoki kwa sababu sasa palikuwa hapakaliki tena kutokana na maombi yaliyokuwa yanaendelea ndani, njia nzima baba akawa ananilaumu kwa uzembe nilioufanya. Kwa bahati nzuri baba Rahma alinitetea kwamba ni kwa sababu sikuwa najua.

Kiukweli lawama za baba zilikuwa ni uonevu wa hali ya juu, maelezo aliyokuwa ananipa, alikuwa ananielekeza vitu nusunusu, sasa kwa mfano hapo kwa akina Sadoki, mimi ningejuaje kama natakiwa kumgeuza Sadoki pia atoke kinyumenyume huku nikiwa nimemshikilia bila kupewa maelekezo?

“Sisi tunakusaidia wewe mwenyewe kwa sababu ya upumbavu ulioufanya, kwani sisi ndiyo tulikutuma uende kwenye msiba ambao wewe mwenyewe ndiye uliyeusababisha? Utajuana mwenyewe na Mkuu, we fanya masihara utaona mwisho wake,” alisema baba.

Tayari tulishakaribia pale kwenye uwanja wa shule ya msingi niliyosoma ambapo ndipo tulipofikia.

“Sasa mzee mwenzangu, tukiendelea kufanya mambo kwa hasira, kweli tutampoteza huyu kijana, hapa kinachotakiwa ni kuhakikisha tunamaliza kwanza suala la Mkuu na Togo na kama unavyoona huku ndiyo tayari tumeshakwama na muda unayoyoma,” alisema baba yake Rahma.

Mwanzo nilikuwa nalichukulia suala hilo kama jepesi lakini kwa jinsi mazungumzo hayo yalivyokuwa, niligundua kwamba kweli nipo kwenye hatari kubwa kwa sababu ya makosa niliyokuwa nimeyafanya bila kujua.

“Hivi si kuna yule mtu aliyepoteza maisha kwenye ile ajali ya bodaboda aliyoisababisha huyu mwendawazimu?” baba aliuliza. Baba yake Rahma akamjibu kwa kutingisha kichwa, nikiwa na shauku kubwa ya kutaka kusikia baba atasema nini.

“Taarifa zinaonesha kwamba amezikwa jioni ya leo, ila sijui amezikwa wapi, kama tukifanikiwa kujua, tunaweza kumtumia kama mbadala wa Sadoki ili tulimalize hili tatizo la huyu mwendawazimu,” alisema baba huku akiendelea kunishutumu.

Sikuelewa anamaanisha nini na hata kama tungelijua kaburi lake tungefanya nini.

“Twendeni Mlandizi, tutajua hukohuko tukifika, si unalikumbuka eneo la ajali?” baba aliniuliza, nikatingisha kichwa kwa sababu ilikuwa ni palepale kwenye nyumba iliyokuwa na msiba ndipo hiyo ajali nyingine ilipotokea. Yaani baba alivyokuwa akizungumza, utafikiri kutoka Chunya mpaka Mlandizi ni karibu sana.

Kukukumbusha tu, hapa aliyekuwa anazungumziwa aliyekuwa ni yule dereva wa bodaboda ambaye wakati nikiwa nakimbia kuokoa maisha yangu baada ya wale wazee kunishtukia pale kwenye msiba, nilimgonga wakati nikivuta barabara, yeye akiwa kwenye bodaboda iliyokuwa kwenye kasi kubwa. Pale alipodondoka hakuweza hata kuomba maji, alipoteza maisha palepale na sikuwa najua mpaka nilipokuja kuambiwa na akina baba ambao hata sijui wao walijuaje.

Basi tulienda mpaka pale chini ya ule mti, tukakuta kuna watu wengine wengi wakiwa wanafanya mambo ambayo hata sikuyaelewa lakini yalionesha kuhusiana na nguvu za giza.

Tukakaa na kuweka duara kama tulivyofanya kule Kunduchi wakati tukitaka kuondoka, nikaambiwa nifumbe macho na nisifumbue mpaka nitakapoambiwa, lakini baba akanisisitiza kwamba natakiwa kuwa nalifikiria eneo lile ajali ilipotokea.

Kweli nilifanya hivyo, wao wakafanya tena mambo yao kama kule Kunduchi na muda mfupi baadaye, upepo mkali ulianza kuvuma, sikuelewa tena kilichoendelea mpaka nilipokuja kuzinduliwa na baba aliyekuwa akinitingisha kwa nguvu.

Yaani kilichokuwa kinatokea, inakuwa kama nimepitiwa na usingizi mzito wa ghafla, kisha nikizinduliwa najikuta nipo kwenye mazingira mengine tofauti kabisa. Nilishtukia nikiwa nimelala pembeni ya barabara ya lami, baba aliponiamsha, nikawa nashangaashangaa, nikageuka huku na kule kama ninayejaribu kuvuta kumbukumbu.

Sikuyaamini macho yangu kugundua kwamba tulikuwa Mlandizi, tena jirani kabisa na pale ile ajali ilipotokea. Nilipotazama upande wa pili wa barabara, niliwaona watu wengi wakiwa wamekaa na kuuzunguka moto, pale kwenye ile nyumba iliyokuwa na msiba wa kwanza wa yule mtoto, moyo ukashtuka sana nikikumbuka kilichotokea.

“Mbona umeshtuka,” baba aliniuliza.

Je, nini kitafuatia? Usikose next issue au bofya>>>Simulizi za Majonzi kusoma mwendelezo.

Comments are closed.