The Graves of The Innocents (Makaburi ya Wasio na Hatia)- 58

ILIPOISHIA:

Sikuyaamini macho yangu kugundua kwamba tulikuwa Mlandizi, tena jirani kabisa na pale ile ajali ilipotokea. Nilipotazama upande wa pili wa barabara, niliwaona watu wengi wakiwa wamekaa na kuuzunguka moto, pale kwenye ile nyumba iliyokuwa na msiba wa kwanza wa yule mtoto, moyo ukashtuka sana nikikumbuka kilichotokea.

“Mbona umeshtuka,” baba aliniuliza.

SASA ENDELEA…

Sikumjibu zaidi ya kumuonesha kidole kwenye ile nyumba ambapo bado watu walikuwa wakiendelea kuota moto huku wakipiga stori za hapa na pale msibani. Baba wala hakuhangaika hata kugeuka, akanitaka kuelekeza akili zangu kwenye jambo lililotupeleka pale kwani muda ulikuwa umetutupa mkono.

Ilionesha baba alikuwa anaelewa kila kitu kilichokuwa kikiendelea, nikawa najiuliza ameyajuaje yote hayo? Kiukweli sikupata jibu, baba Rahma naye wala hakujishughulisha na chochote na wale watu kama baba.

“Onesha aliangukia wapi? Unatupotezea muda,” alisema baba, nikawa najaribu kuvuta kumbukumbu, nikawa natembea pembeni ya barabara kuelekea pale yule dereva wa bodaboda alipodondokea, wakawa wananifuata kwa nyuma.

“Nadhani ni hapa.”

“Unadhani? Kwani huna uhakika?”

“Nilipomgonga aliyumbayumba kwa mita kadhaa, akaja kudondokea hapa, sina uhakika kwa sababu mimi nilikuwa nimesimama kule mbali.

“Hebu nenda ulipokuwa umesimama,” alisema baba. Ilionesha hakuwa akitaka majibu ya kubahatisha, nikageuka na kutazama tena kule msibani. Bado moyo wangu ulikuwa na hofu, nikiamini wale wazee wanaweza kuwa miongoni mwa watu waliokesha pale msibani halafu nikayazua mengine tena.

Nilirudi kwa hofu mpaka pale nilipokatiza barabara nikiwa spidi kali kama kiberenge, nikasimama na kuwageukia akina baba. Niliweza kupata ramani halisi, nikatembea harakaharaka kuelekea mpaka pale nilipokuwa nimewaacha.

“Ni hapa,” nilisema huku nikioneshea kidole katikati ya barabara. Ni kweli nilipatia kwa sababu bado palikuwa na alama za damu na vioo vya ile bodaboda, baba akainama pale katikati ya lami kisha akawa ni kama anaokota vitu fulani hivi.

Baada ya hapo alikuja upande wa pili tulipokuwa tumesimama, akawa anatazama chini kisha akainua uso na kunitazama:

“Walipomtoa pale katikati ya barabara walimlaza hapa,” alisema huku akionesha, ni kweli pale pembeni napo palikuwa na alama za damu nyingi zilizokaukia, kwa kutumia mikono miwili, alizoa udongo uliokaukia damu, kisha akapiga magoti na kuuinua juu, akazungumza maneno fulani kama anayenuiza jambo kisha akausogeza ule udongo puani kwake, akaunusa kisha akapiga chafya mfululizo.

Hakusema chochote baada ya hapo zaidi ya kuinuka na kuanza kutembea kwa haraka kuelekea upande wa kusini, kama anayetafuta kitu, baba yake Rahma alinipa ishara kwamba tumfuate, akawa anatembea kwa kasi huku akiongea maneno ambayo sikuwa nayaelewa.

Alivuka barabara, na sisi tukawa tunamfuata, akawa anazidi kuongeza kasi kiasi kwamba nililazimika kuwa nakimbia ili kwenda nao sawa. Bahati nzuri ni kwamba tulikuwa tukielekea upande tofauti kabisa na kule kulikokuwa na msiba.

Ilifika mahali akachepuka na kuingia vichakani, safari hii akaanza kutimua mbio, sote tukawa tunakimbia kumfuata. Japokuwa ilikuwa ni usiku, tulikimbia vichakani kwa muda mrefu sana, baadaye tukatokezea kwenye makaburi mengi, baba akawa anazunguka huku na kule na mwisho aliishia kwenye kaburi moja lililoonesha kuwa jipya.

“Amezikwa hapa,” alisema baba huku akigeuka huku na kule, nikawa natetemeka kwa hofu, sikujua nini kinachoenda kutokea.

“Simama kwa kule,” alisema baba huku akinielekeza kusimama upande uliokuwa na msalaba ambapo kimsingi ndiyo kichwani. Nilifanya hivyo, baba yake Rahma akasimama upande wa miguuni na baba akasimama katikati, juu ya kaburi.

Baada ya kusimama hapo, aligeuka huku na kule kama anayetafuta kitu kisha akashuka kutoka pale juu ya kaburi na kunifuata, akawa ananiongelea sikioni.

“Huyu amezikwa leo, katika sheria za jamii yetu, anaruhusiwa kutolewa kafara kwa hiyo tutamchukua huyu badala ya Sadoki, kule tutarudi siku nyingine kwa sababu kuna mambo hayakwenda sawa kwa sababu yako, sasa ukifanya ujinga tena na hapa, hakuna wa kumlaumu,” alisema baba.

Hofu ikazidi kuongezeka kwenye moyo wangu. Kama nilivyoeleza, hakuna sehemu niliyokuwa naiogopa kama makaburini, nikawa nahisi kama mwili na akili vinatengana. Kibaya zaidi ilikuwa ni usiku na nimeshawahi kusikia kwamba makaburini nyakati za usiku kunakuwa na mambo mengi sana ya ajabu, sikuelewa baba anavyosema tunamchukua yule dereva bodaboda aliyefariki kwenye ajali, alimaanisha nini.

Ninavyojua mimi, huwezi kufukua kaburi na kutoa maiti kwa sababu kwanza siyo kazi nyepesi lakini pia, lazima watu watakuona ukiwa unalifukua kwa sababu makaburi mengi huwa yanakuwa na ulinzi, na kama si hivyo, mizimu mibaya iliyopo makaburini lazima itakudhuru tu. Sikuelewa malengo ya baba ni nini lakini kama mwenyewe alivyokuwa anasisitiza kwamba lengo ni kunisaidia mimi, ilibidi nitulie kuona mwisho wake.

Baada ya kuzungumza na mimi, alimfuata baba yake Rahma, wakawa wanajadiliana jambo pale, wakazungumza kwa zaidi ya dakika mbili kwa sauti ya chini kiasi kwamba sikuwa nikisikia walichokuwa wanakisema.

Baada ya hapo, baba yake Rahma alinifuata na kuniambia natakiwa kuvua nguo zote na kukaa juu ya kaburi kwa sababu kazi iliyokuwa inaenda kufanyika, si ya kitoto. Nilishtuka, yaani nivue nguo halafu nikae juu ya kaburi? Mapigo ya moyo yakaanza kunienda mbio tena.

Ni kama baba yake Rahma alinielewa jinsi nilivyokuwa na hofu, akaniambia sitakiwi kuwa na hofu yoyote kwa sababu kwenye jamii yao, kukaa bila nguo ni kitu cha kawaida kabisa, isitoshe wao ni baba zangu ambao wananijua tangu nikiwa mtoto mchanga, kwa hiyo lazima nifanye walichoniambia.

Ilibidi nikubaliane naye maana baba alikuwa akisisitiza kwamba muda unakwenda. Nikasogea pembeni na kuvua nguo zote, nikajiziba sehemu ya mbele kwa mikono yangu na kupanda kwenye tuta la lile kaburi, nikawa natetemeka mno.

Baada ya kukaa juu ya tuta la kaburi, nikiwa nimeupa msalaba mgongo kama nilivyoelekezwa, baba na baba Rahma, mmoja akiwa amesimama upande wa kichwani na mwingine upande wa miguuni, walianza kuimba nyimbo za kutisha kwa kupokezana, akiimba baba, baba yake Rahma anaitikia, wakaendelea hivyo kwa dakika kadhaa kisha wakaanza kulizunguka lile kaburi, kutoka kulia kwenda kushoto.

Walifanya hivyo kwa dakika kadhaa, baadaye baba akaniambia nisimame. Nilifanya hivyo huku nikijiziba kwa soni, akanielekeza kuelekea upande ule wa kichwani niliokuwa nimesimama awali, kisha akaniambia niwe makini kutazama anachokifanya.

Milio ya bundi na ndege wengine wa usiku, iliendelea kusikika na kufanya hali iwe ya kutisha mno pale makaburini. Baba alionesha kwa ishara kwamba natakiwa kupiga makofi na kupiga mguu wangu wa kushoto chini kwa nguvu, na vyote vifanyike kwa wakati mmoja.

Alinihesabia kwa alama za vidole kisha akaniruhusu, nikapiga makofi kwa nguvu na wakati huohuo nikapiga kishindo cha nguvu. Alinionesha kwa ishara kwamba natakiwa kufanya hivyo mara tatu, nikarudia mara ya pili, kisha nikafanya kwa mara ya tatu.

Kilichotokea baada ya kufanya hivyo kwa mara ya tatu, kilinifanya nihisi kama mwili wangu unakufa ganzi kwa hofu, sijawahi kushikwa na hofu kama niliyoipata siku hiyo na kama baba asingeniwahi, huenda ningedondoka kama mzigo chini maana mwili wote uliisha nguvu.

Japokuwa ilikuwa ni usiku, tena nikiwa sina nguo na kulikuwa na baridi kali, nilihisi kijasho chembamba kikinitoka, ama kweli duniani kuna mambo na ukishangaa ya Musa, utayaona ya Firauni.

Je, nini kitafuatia? Usikose next issue au bofya>>>Simulizi za Majonzi kusoma mwendelezo.


Loading...

Toa comment