The House of Favourite Newspapers

HALI YA DIMPOZ NI DARASA KWA WASANII

MARA nyingi matatizo huwaunganisha watu na kuwafanya kuwa kitu kimoja, hata kama katikati yao kulikuwa na tofauti kubwa kiasi gani wengi hujirudi nyuma na kuwa kitu kimoja, huu ndiyo ubinadamu!

Tumeona namna wasanii walivyojitoa na kuwa kitu kimoja angalau hata kwa kuonyesha kuwa wanajali na kumuombea mwanamuziki Omary Nyembo ‘Ommy Dimpoz’ afya yake iweze kuimarika na ikiwezekana apone kabisa.

Miongoni mwa watu walioonesha kuguswa na kuumwa kwa Dimpoz ni mwanamuziki Nasibu Abdul ‘Diomond Platnumz’.

Ikumbukwe kuwa, hapo mwanzo wawili hawa hawakuwa wakielewana na waliwahi kulipuana mpaka mitandaoni, lakini matatizo yamewakutanisha, pia mbali na Diamond hata meneja wa zamani wa Dimpoz anayejulikana zaidi kwa jila la Mubenga, ambaye hawakuwa sawa, amerudi kundini na kwenda kumjulia hali mwanamuziki huyo Afrika Kusini.

Hivi ndivyo maisha yalivyo, kuna ‘ups and downs’ pamoja na mikwaruzano ya aina mbalimbali.

Hata hivyo pamoja na watu mbalimbali kuungana kwa ajili ya kumpa pole Dimpoz, tatizo lake limekuwa suala la watu kujifunza.

Wasanii kadhaa wamezungumza na Ijumaa na kueleza nini walichojifunza kutokana na tatizo lake. Lakini kabla ya kukumegea waliyosema, fahamu kwanza nini kimemsibu Dimpoz mpaka kuwa kwenye hali hiyo aliyopo kama ulikuwa hufahamu!

TATIZO LAKE NI HILI

Dimpoz kupitia mahojiano yake ya karibuni amesema kwamba amepitia wakati mgumu sana na ilikuwa nusu kufa, nusu kupona katika tatizo lililokuwa linamkabili la kusinyaa kwa koo lake kiasi cha kushindwa kula. Ambapo katika vipimo vya awali aliambiwa kwamba ana kansa, jambo lililomuogopesha kiasi cha kuwaza kuwa ‘angeondoka’.

Lakini baada ya vipimo zaidi nchini Kenya na Afrika Kusini, iligundulika kwamba si kansa inayomsumbua, madaktari walimwambia inawezekana alikula chakula au kunywa kinywaji chenye sumu. Mkali huyu wa Wimbo wa Yanje, alianza kusumbuliwa na tatizo hili hasa mwezi Mei, muda mfupi tu baada wa harusi ya swahiba wake, ambaye ni mwanamuziki wa Bongo Fleva, Ali Kiba.

Katika matibabu ya tatizo lake Dimpoz alifanyiwa upasuaji mkubwa kuanzia tumboni hadi shingoni na ikatengenezwa njia nyingine ya chakula, ila ya kwanza ya mfumo wa kawaida wa binadamu madaktari waliiua. Baada ya hapo hali yake ilikuwa mbaya kwani mapafu yake yalikuwa hayafanyi tena kazi vizuri, ikabidi awekwe kwenye kitengo cha uangalizi maalumu (ICU) kwa muda wa wiki tatu.

Mungu akasaidia jamaa akatoboa na baadaye akaenda Kenya kujiangalizia hali na kwa sasa ametakikuwa kuwa anahudhuria kliniki za mara kwa mara ili kuangaliwa anaendeleaje. Hawa chini ni baadhi ya wasanii ambao wamezungumzia hali ya mwanamuziki huyo na ‘pindi’ walilojifunza, shuka nao;

LULU DIVA

Kiukweli ninakosa hata neno la kuzungumza kutokana na hali ya kaka yangu Dimpoz. Kikubwa ninamuombea kwa Mungu apone, lakini kama kweli alikula sumu ni jambo la wasanii kuwa na tahadhari sana katika kila kitu tunachokuwa tunakula.

G NAKO

“Ni Mungu tu ndiye anaweza kutusaidia. Unajua Watanzania tumezoea kuishi kwa ujamaa na umoja. Wakati mwingine kutokana na maisha tunayoishi ni vigumu kufahamu nani ni adui na yupi si adui. Mtu yeyote anaweza kukudhuru tena wakati wowote. Kwa hiyo kama nilivyosema ni suala la kumuachia Mungu ingawa nimejifunza mtu unaweza kuwa na adui mahali popote pale.

DAYNA NYANGE

“Mungu amsaidie Dimpoz aweze kupona. Kwa upande wangu tatizo lake linafundisha sana na linafikirisha mno. Mtu unaweza kuondoka hivihivi bila kujua. Wewe ona mtu kala sumu na kaishi bila kugundua tatizo muda mrefu na akaja gundua tatizo tayari lilikuwa limekwisha leta madhara ya kutisha. Kwangu nimegundua ni vyema mtu unapohisi mwilini mwako kuna matatizo fulani ni vema ukafanya uchunguzi mapema wa mwili wake.

SABBY ANGEL

“Ni muhimu kuwa makini sana kila tunapotembelea na kila tunachokula hasa pale tunapokuwa na watu. Ni kweli siyo jambo la kusaidia asilimia mia lakini linaweza kusaidia kwa namna moja au nyingine ya kuepusha kula vitu vya hatari na afya yetu.

BILL NAS

“Ninaungana na watu wote wanaomtakia pole ndugu yangu Dimpoz kwa sababu maradhi tumeumbiwa binadamu. Kuhusu nilichojifunza ni kwamba kuna sababu nyingi zinaweza kubadilisha maisha ya mwanadamu, sababu nyingine hatuwezi kuzifahamu, ni vyema kuwa makini katika kila hatua kwenye maisha yetu,” alimalizia Bill Nas.

Comments are closed.