The House of Favourite Newspapers

HALOTEL YAREJESHA FAIDA KWA JAMII

Mkurugenzi wa kampuni ya Halotel, Nguyen Van Son(wa kwanza kushoto) akikabidhi hundi ya shilingi milioni 20.6 kwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Binilithi Mahenge (wa kwanza kulia) kwa ajili ya kuanzisha kiwanda cha kufyatua matofali cha kikundi cha vijana wa Dodoma, akishuhudia makabidhiano ni Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye (katikati).
Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye (wa kwanza kulia) akikabidhi vifaa mbali mbali vya hospitali vilivyotolewa na kampuni ya Halotel kwa Mganga Mkuu Mfawidhi wa Hospitali ya Makole, Dodoma Dkt. George Matiko ( wa pili kushoto) Mkurugenzi wa kampuni ya Halotel, Nguyen Van Son (wa pili kulia) kwa niaba ya Serikali kutoka kwa kampuni ya Halotel kwa ajili ya kuhudumia wagonjwa. Wa kwanza kushoto ni Katibu Mkuu wa Mawasiliano, Wizarani Mhandisi Dkt. Maria Sasabo

KATIKA kuhakikisha inatekeleza agizo la Serikali ya kurejesha faida kwa jamii Kampuni ya Simu ya Halotel  imemkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Dodoma kiasi cha zaidi ya Sh Milioni 20 kwa ajili ya kuwawezesha vijana wa mkoa huo kujiajiri kupitia sekta ya ujenzi.

 

 

Mbali na fedha hizo, Halotel pia imekabidhi vifaa mbalimbali vya hospitali kwa ajili ya kuhudumia wagonjwa vikiwemo vitanda, neti, mashuka na aproni vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni sita katika Hospitali ya Makole iliyopo Dodoma mkoani humo.

 

 

Akikabidhi misaada hiyo kwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Binilithi Mahenge mbele ya Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Atashasta Nditiye, Mkurugenzi Mtendaji wa Halotel, Tanzania Nguyen Van Son alisema pamoja na mambo mengine, misaada hiyo imelenga kuunga mkono juhudi mbalimbali za maendeleo zinazofanywa na Serikali ya awamu ya tano.

 

 

Son alisema  katika kuhakikisha inaunga mkono jitihada hizo za Serikali, Kampuni hiyo ya simu ya Halotel imekuwa mstari wa mbele kurudisha faida kwa kile inachokipata kwa kuisaidia jamii mambo mbalimbali  kwa lengo la kukabiliana na changamoto zinazowazunguka.

 

Alisema hatua hiyo imelenga kutoa shukrani kwa wananchi kwa hatua yao ya kuwaunga mkono kwa kutumia huduma za kampuni hiyo iliyosambaa nchi nzima ikitoa huduma mbalimbali  na hasa katika  maeneo na hasa vijijini.

 

 

“Tunaamini misaada hii itakwenda kuwa chachu ya maendeleo katika sekta ya afya na ujenzi, hususani kwa kuwawezesha vijana kujiajri katika sekta za ujenzi unaoendana na kukua kwa mji wa Dodoma” alisema Son.

 

Aidha aliishukuru Serikali kwa kuweka mazingira wezeshi na rafiki yaliyowavutia kuweza kwenye Sekta ya Mawasiliano nchini na kuongeza kuwa dhamira yao ni kuendeleza ushirikiano na kuhakikisha kuwa huduma za mawasiliano zinakuwa za viwango, ubora na gharama nafuu kwa mtumiaji.

 

Aidha akizungumza wakati wa makabidhiano ya misaada hiyo, mbali na kuipongeza Halotel kwa hatua hiyo, alizitaka kampuni zingine kuiga mfano huo ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Serikali linayozitaka kampuni za simu kurejesha sehamu ya faida kwa jamii.

 

 

“Nitoe wito kwa kampuni zingine za simu za mkononi ziige mfano wa Halotel wa kurudisha shukrani kwa wananchi” alisema Nditiye na kuwataka wananchi kuthamini mchango wa mawasiliano katika maisha yao ya kila siku kwa uchumi na maendeleo ya Taifa.

 

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Binilithi Mahenge, pamoja na kuipongeza Halotel alisema msaada huo umekuja wakati muafaka hususani wakati huu ambao mkoa huo unaendelea na mikakati yake ya kuwasaidia vijana.

 

“Vijana wa Dodoma mtanufaika na Serikali kuhamia Dodoma, kupitia fedha hizi tumeona tuanzishe kikundi cha vijana ili waweze kuanzisha kiwanda cha kufyatua matofali na mradi huo utakuwa na vijana wa kutoka Jeshi la Kujenga Taifa ili wawasaidie ili baadae vijana waweze kuanzisha na kuendeleza viwanda vyao,” amesema Dkt. Mahenge.

 

Naye Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Makole Dkt Geogre Matiko, aliishukuru Halotel kwa msaada huo na kwamba kutokana na mahitaji mbalimbali yaliyopo katika hospitali hiyo ya Makole huku akizitaka taasisi zingine kuiga mfano huo.

 

 

Alisema pamoja na  jitihada mbalimbali zinazofanywa na Serikali kuinua sekta ya afya, bado kuna changamoto baadhi ambazo kama wadau watajitokeza na kusaidia kama ambavyo Halotel imefanya, zitaweza kupungua ama kuisha kabisa.

Comments are closed.