The House of Favourite Newspapers

Breaking News: Mahakama Yatoa Dhamana Kwa Mbowe na Viongozi Wake

03:00pm: Hatimaye Hakimu ametoa dhamana kwa washtakiwa! Kila mshtakiwa anatakiwa kuwa na wadhamini wawili ambao watasaini bondi ya Sh. Milioni 20 na wawe na barua toka kwa viongozi wao wa vijiji ama S/Mtaa na wawe na nakala za vitambulisho vyao.

Maamuzi hayo yametolewa leo na hakimu Wilbrad Mashauri baada ya kupitia maelezo kutoka pande zote mbili huku akibaini kuwa watuhumiwa hao walikua na uhalali wa kupata dhamana kwa kuwa makosa yao yanadhaminika.

02:25pm: Wakili wa Jamhuri anamuomba mkuu wa Logistics za kuleta wafungwa Kisutu, aliyemtaja kwa jina moja la Shaban aeleze sababu za watuhumiwa kutofika mahakamani. Shaban anasema asubuhi aliwasiliana na mkuu wa gereza la Segerea ambaye alisema gari limeharibika.

 

2:00pm: Hakimu amewaita mawakili. Waendesha mashitaka hawapo, aijulikani wameenda kula au vipi…

1:58pm: Watu wameshaondoka katika ukumbi wa mahakama. Huenda wanasubiri kujua hatua inayofuata, wengi wapo nje ya ukumbi.

Muonekano wa Chumba cha mahakama.

12:26pm: : Baada ya Mawakili wa Mbowe na wenzake kuzungumza na Hakimu Mkuu Mkazi, Wilbard Mashauri, Wakili Kihwelo amesema kuwa Hakimu Mashauri ameamua kusoma uamuzi mdogo kuhusu dhamana ya akina , hata kama watuhumiwa hawapo mahakamani..

 

12:01pm: Mpaka saa 6:30 mchana, Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe na wenzake watano, hawajafikishwa katika eneo la Mahakama ili kuendelea na kesi yao. Inadaiwa gari lililokuwa liwapeleke mahakani limeharibika.

11:50am: Askari wenye silaha za kivita wameanza kuitana, wanajikusanya. Hatujui walikuwa wanapanga nini. Baadae wamesambaa; baadhi wameelekea getini huku wengine wakijipanga tena kuzunguka viunga vya mahakama.

 

11:45am: Mawakili wa Jamhuri – Patrick Mwita, Mutalemwa Kishenyi na Mawakili wa washitakiwa Peter Kibatala na Hekima Mwasipu wameingia ofisini kwa Hakimu Mkuu Mkazi, Wilbard Mashauri.

 

11:34am: Baadhi ya Viongozi wa juu wa CHADEMA waliokuwa wamefika mahakamani wameondoka mahakamani Kisutu. Wanaenda kushiriki msiba wa marehemu Kimesela ambaye anazikwa makaburi ya Kinondoni jijini Dar.


11:30am: Wananchi na makada wa CHADEMA wameanza kukosa uvumilivu baada ya kuzuiliwa nje ya lango kuu la mahakama na Polisi. Wameanza kuimba nyimbo za kudai haki, Wakili Kibatala amewasihi waondoke lakini dalili hazionyeshi kama wataondoka eneo hili.

 

11:20am: Mpaka muda huu, Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe na wenzake watano, hawajafikishwa katika eneo la Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar. Tetesi zinadai kuna mikakati ya kuhakikisha wanakula Pasaka wakiwa gerezani. Kisingizio kinachodaiwa kutumika ni kuwa “Magereza hawana gari la kuwaleta mahakamani”

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, limeimarisha ulinzi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ili kudhibiti umati wa watu wanaodhaniwa kuwa ni wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambao wamekusanyika nje ya mahakama, wasiingie kusikiliza kesi inayowakabili mwenyekiti wa Chama hicho, Freeman Mbowe na viongozi wenzake watano.


Mbowe na wenzake wanataraiwa kufikishwa mahakamani hapo wakitokea mahabusu ya Segerea wakikabiliwa na mashtaka manane yakiwemo kufanya maandamano yaliyosababisha kifo cha mwanafunzi wa Chuo cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwiline, Februari 16, mwaka huu, uasi na kuhamasisha chuki.

 

Kesi ya Mbowe, Chadema: Lowassa Atinga Mahakamani, Ulinzi Mkali!

Wabunge wa Chadema, wafuasi na wananchi wengine wakiwa mahakamani kufuatilia kesi hiyo.

Baadhi ya wabunge wa Chadema, wafuasi wa chama hicho na wananchi wengine waliofika mahakamani kufuatilia kesi hiyo ni  Waziri Mkuu Mstaafu na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Edward Lowassa, Waziri Mkuu Mstaafu, Fredrick Sumaye, Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Prof. Abdallah Safari, Mbunge Joseph Haule ‘Prof. Jay.


Inasemekana baada ya kuzuiliwa kuingia mahakamani, wananchi na makada wa CHADEMA wameanza kukosa uvumilivu na kuanza kuimba nyimbo za kudai haki. Wakili Kibatala amewasihi waondoke lakini dalili hazionyeshi kama wataondoka eneo hili.

VIDEO: WASIKIE HAPA CHADEMA WAKIFUNGUKA

Comments are closed.