The House of Favourite Newspapers

Hatuwezi Kuishi Jana, Simba Inastahili Mabadiliko Ya Ukweli

0
Wachezaji wa Simba

KLABU ya Simba ipo kwenye mchakato wa mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji wa klabu hiyo hasa katika idara ya uongozi, ni jambo zuri kwa kuwa nimekuwa mmoja wa wanaounga mkono mchakato huo kwa muda mrefu. Ninaunga mkono siyo kwa kuwa ninamuunga mkono mtu fulani au kwa kuwa ninataka fulani achukue hiyo nafasi, kitu kikubwa kama mdau wa soka ni kuona Simba na klabu nyingine zikipiga hatua nzuri katika maendeleo ili kuwafurahisha mashabiki wao.

Haki namba moja wa shabiki wa soka kwa timu yake ni kushangilia au kuzomea, anapoona timu haiendi sawa ana haki ya kukosoa na kulalamika kwa kuwa yeye ndiye anayetoa fedha ya kuifanya klabu hiyo ijiendeshe, masuala ya uongozi kwa mashabiki huwa hayatakiwi kuhusika sana japo wana haki ya kutoa maoni.

Tunaona mifano mingi Ulaya na kwingineko, kuna mashabiki wengi tu hawawataki wamiliki wa Manchester United au wale ambao hawawapendi wamiliki wa Klabu ya Arsenal, lakini haki yao ya kwanza wanayotakiwa kuipata ni kuona timu zao zikifanya vizuri. Tumewahi kuona maandamano mengi tu ya mashabiki hao wakipinga umiliki wa baadhi ya mabosi wa klabu lakini hakuna chochote kinachofanywa, kwa kuwa haki yao namba moja ni kuona timu inafanya vizuri.

Hivyo, ikitokea Elius Kambili au Lucy Mgina akanunua hisa za Simba na kutimiza vigezo vyote ambavyo vinatakiwa, anaweza kuendelea kuongoza klabu hiyo bila kujali mashabiki hawamtaki au wanamtaka, anachotakiwa ni kutimiza majukumu yake inavyotakiwa ya kiuongozi tu na kuipa klabu maendeleo.

Nimeanza na mfano huo sababu kuna hofu kubwa kuwa yawezekana wapo watu wanaoweza kununua hisa ndani ya Simba na wakawa hawakubaliki lakini kwangu mimi kama wanatimiza vigezo vyote vinavyotakiwa basi ni vema wakapewa mzigo huo kwa kuwa hapo wao watakuwa wamewekeza fedha na hawatataka zipotee.

Tunasikia kuwa kina Mohamed Dewji ‘Mo’ na wenzake wapo tayari kutoa zaidi ya mabilioni ya shilingi ili wapate haki ya kununua hisa na kuwa sehemu ya umiliki wa klabu hiyo, ikiwa hilo litatimia, Mo hatakubali kuona Simba ikipotea wakati yeye anawekeza ‘mzigo’ wa kutosha. Hakuna mfanyabiashara ambaye huwa anataka kufanya biashara ya hasara, ikitokea hivyo ujue ni bahati mbaya lakini kila mmoja mwenye nia ya kuwekeza ujue anataka kupata faida. Ndiyo maana naunga mkono mabadiliko ya mfumo kwenye klabu zetu.

Leo tunaona wamiliki wa Azam FC ambavyo wamekuwa na mikakati mizuri ya kuona timu yao inapiga hatua, wanafanya hivyo kwa kuwa wanajua wamewekeza fedha nyingi, hivyo wataitumia kutangaza bidhaa zao au timu kufanya vizuri ili hizo biashara wanazotangaza ziweze kufika kwa walengwa wengi.

Yawezekana kinachowakwamisha ni kwa kuwa wao Azam FC hawana mtaji wa watu kama zilizo timu hizo kubwa, sasa kama kuna uwezekano wa kubadilika na kuwapa watu wanaotaka kutupa maendeleo kwa nini tusiwape. Simba na Yanga kwa miaka mingi kumekuwa na ubabaishaji mwingi, licha ya kuwa na mtaji mkubwa wa watu ambao wanaunga mkono klabu hizo bado zimeendelea kuishi maisha ya kimasikini kwa kuwa hakuna mfumo sahihi wa kuziendesha klabu. Kinachotokea kwa sasa ni kuwa wale ambao wanaona mabadiliko hayo yakipita ndiyo wamekuwa mstari wa mbele kupinga, lakini kama kweli tuna nia ya maendeleo ni vema tukawa na moyo wa chuma na kukubali hata kama tutakosea lakini lazima tufike tunapokwenda.

Tumekuwa wagumu kubadilika wakati tunao uwezo wa kufanya hivyo, hata wale wanaotaka kuwa na uthubutu wanazuiliwa kwa faida au maslahi ya watu wachache kitu ambacho ni kibaya kwenye maendeleo ya faida ya soka letu. Kama kweli tunataka maendeleo basi tunatakiwa kukubali kubadilika kutokana na maisha ya sasa yalivyo, kuendelea kutegemea maisha ya kuungaunga kisa tu babu zetu au wazee wetu walifanya hivyo ni sawa na kujiangusha wenyewe na kamwe hatutaendelea.

Na John Joseph Vuvuzela Mawasiliano +255 713 393 542

Okwi Ameshindikana Apewa Mihela Alindwa na Polisi

Leave A Reply