The House of Favourite Newspapers

HAUSIGELI ANAYEDAIWA KUMUUA bosi WAKE KWA SHOKA AHENYA

MIONGONI mwa kesi zenye msisimko wa aina yake na simulizi ya kutisha ni ile ya mauaji inayomkabili aliyekuwa mfanyakazi wa ndani (hausigeli), Oliana Shabani (19) (pichani).  Oliana, mwenyeji wa mkoani Arusha, alidaiwa kumuua bosi wake kwa kumpiga kichwani na shoka walilokuwa wakipasulia kuni.

Baada ya tukio hilo kuenezwa kwenye mitandao ya kijamii likiambatanishwa na picha ya mtuhumiwa (iliyotumika ukurasa wa mbele wa gazeti hili) lilizua mshtuko kwa baadhi ya watu wanaoishi na mahausigeli na kuzua mjadala mkubwa.

Bila kumhukumu binti huyo kwa sababu haijathibitishwa mahakamani kuwa amefanya kosa hilo, wengi kati ya wachangiaji walisema kuna haja ya elimu kwa familia jinsi ya kuishi na wafanyakazi wa ndani kutolewa ili kuepuka madhara ambayo yamekuwa yakijitokeza mara kwa mara kuwahusisha wafanyakazi wa ndani na familia ya mabosi wao.

“Ipo haja kwa mahausigeli na mahausiboi pamoja na matajiri wao kupewa elimu ili kuondoa hali ya wafanyakazi wa ndani kujiona kama si sehemu ya familia ya mabosi wao na wao kuonekana hivyo.

“Tatizo hili ndiyo linaloleta wakati mwingine wafanyakazi wa ndani kufanyiwa ukatili au wao kuwafanyia mabosi na familia zao matukio yasiyokuwa ya kiungwana,” alisema mchangiaji mmoja alipotoa maoni yake kwenye mtandao wa kijamii wa Facebook uliokuwa umeweka tukio hilo na kujadiliwa.

MAUAJI YALIYOMTIA MATATIZONI OLIANA

Tukio hilo la mauaji lilijiri Machi 27, 2014 ambapo Oliana alidaiwa kumuua bosi wake wa jinsia ya kike aliyejulikana kwa jina la Slyvester Njau, eneo la Vingunguti-Miembeni wilayani Ilala jijini Dar es Salaam.

TUJIUNGE MAHAKAMANI

Mwishoni mwa wiki iliyopita, wapelelezi wa kesi hiyo ambao ni askari waliieleza mahakama namna walivyofanikiwa kumkamata Oliana.

Askari hao walitoa ushahidi kwa nyakati tofauti katika Mahakama Kuu iliyoketi kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Pamela Mazengo. Askari kutoka kitengo cha upelelezi Mkoa wa Kipolisi wa Ilala, Koplo Ismail aliiambia mahakama hiyo kwamba, walifanikiwa kumkamata Oliana kwa kuwa alikuwa akitumia simu ya marehemu na ilikuwa ikipatikana.

Shahidi huyo ambaye ni mtaalam wa makosa ya mtandao, alidai marehemu alikuwa akiitwa Slyvester Njau na Aprili 9, mwaka 2014 akiwa ofisini kwake, mkuu wake wa kazi alimweleza kwamba kuna mtuhumiwa wa kesi ya mauaji yupo Arusha, hivyo wanatakiwa wakamkamate.

Askari huyo alidai, Aprili 14, mwaka huo, akiwa na Sajenti Silviana, walikwenda jijini Arusha kumtafuta mshtakiwa na kwamba ilikuwa rahisi kwao kumkamata kwa sababu mtuhumiwa aliondoka na simu ya marehemu na ilikuwa ikiendelea kutumika. “Tukiwa Arusha pia tulipata namba ya James Mbise ambaye alikuwa akiwasiliana na mshtakiwa, alitueleza mshtakiwa ni rafiki yake na amemwacha nyumbani anafua nguo.

AKAMATWA KWAMROMBOO

“Tulifanikiwa kumkamata mshtakiwa (Oliana) eneo la Kwamromboo (Arusha) na tulipofanya upekuzi, tulipata vitu mbalimbali kama mtandio, simu aina ya Nokia, mkoba, vyote mali ya marehemu,” alidai afande huyo. Alisema vitu vingine ni kadi ya benki, kamera aina ya Sony, funguo sita za geti na baada ya upekuzi huo walichukua vitu vyote pamoja na mshtakiwa wakarudi naye Dar es Salaam.

SIMULIZI YA MUME WA MAREHEMU

Kwa mujibu wa mume wa marehemu Sylvester, John Thomas wakati akitoa maelezo yake mahakamani hapo hivi karibuni alisema, Machi 27, 2014, majira ya saa 11:00 jioni, alipigiwa simu na dereva aliyekuwa anamrudisha mtoto wake nyumbani na kudai kuwa aligonga geti la nyumbani hapo, lakini halikufunguliwa. Thomas alidai kuwa, kufuatia taarifa hiyo, alikodi pikipiki hadi nyumbani kwake (Vingunguti- Miembeni) na kukuta watu wengi waliokuwa wameizunguka nyumba yake.

ARUKA UKUTA

Alisema alipotaka kuingia ndani, alikuta geti limefungwa na msichana wa kazi (Oliana) ambaye ndiye mshtakiwa, aliondoka na ufunguo wa geti. Alisema alipanda ukuta na kuingia ndani ambapo alimkuta mke wake akiwa kwenye korido hajitambui.

MKE AKATA ROHO

Thomas alidai mke wake alikuwa ameumizwa eneo la kichwani karibu na sikio huku povu likimtoka mdomoni ambapo alimchukua na kumuwahisha Hospitali ya Amana (Hospitali ya Wilaya ya Ilala), lakini wakati anapatiwa matibabu alikata roho. Alisema kuwa waliuchukua mwili na kuupeleka kuhifadhiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na baadaye alirudi nyumbani akiongozana na baadhi ya polisi.

POLISI WAKUTA SHOKA

Alisema, walipofika nyumbani walikuta shoka jipya likiwa na damu na walipoingia chumbani walikuta kabati limevunjwa. “Eneo la sebuleni damu zilikuwa zimetapakaa hadi kwenye mkeka, mito na nguo ya marehemu ikiwa imechanwa na tulipoangalia kabatini tuliona limevunjwa huku nguo zikiwa zimetupwa chini na polisi walipopekua walikuta simu aina Nokia, saa ya mkononi, dhahabu zote na begi la mkononi na baadhi ya nguo zilikuwa zimechukuliwa na Oliana,” alidai Thomas mbele ya mahakama hiyo.

Thomas alisema baada ya kumpumzisha mke wake kwenye nyumba yake ya milele walisafiri pamoja na askari hadi Arusha na kumkuta mshtakiwa akifanya kazi za ndani ambapo walitoa taarifa kwenye uongozi wa mtaa na walipoingia kwenye chumba anacholala kukikagua walikuta vitu vya mke wake marehemu ikiwemo simu ya mkononi aina ya Nokia, funguo za geti, kamera, begi la mkononi, mtandio na vitambulisho vya benki.

AENDELEA KUHENYA

Baada ya kutolewa kwa maelezo ya wapelelezi hao, hakimu aliiahirisha kesi hiyo hadi itakapopangiwa tena tarehe ya kusikilizwa huku Oliana akiendelea kuhenya mahabusu tangu alipokamatwa mwaka 2014 hadi leo. Endelea kufuatilia Magazeti ya Global ili kujua muendelezo wa kesi hiyo.

Comments are closed.