KUPITIA magazeti yanayochapishwa na Kampuni ya Global Publishers na Mtandao wa Global Publishers, Kampuni ya Global Publishers LTD iliamua kufanya utafiti kutoka kwa wasomaji kutaka kujua ni mawaziri gani wa serikali ya Rais Dk. John Pombe Magufuli, wanaoongoza kwa kuchapa kazi.
Wasomaji walitakiwa kutuma majina ya mawaziri wanaoona wanachapa kazi kwenda kwenye namba maalum iliyowekwa kwenye magazeti na hatimaye, wasomaji wengi wametoa maoni yao kuhusu mawaziri kumi wachapakazi.
Kwa kuzingatia kura zilizokuwa zikipigwa na wasomaji wetu, wafuatao ni mawaziri kumi waliopata kura nyingi zaidi, hivyo kukidhi kuingia kwenye orodha ya mawaziri kumi wachapakazi.
- WAZIRI MKUU, KASSIM MAJALIWA
Waziri Mkuu, amepigiwa kura na wasomaji wengi, wakieleza kwamba amekuwa mstari wa mbele kuwasimamia mawaziri pamoja na kumsaidia mheshimiwa rais katika majukumu mbalimbali. Muda mwingi anafanya ziara kwenye maeneo mbalimbali nchini, kushughulikia changamoto zinazowakabili wananchi.
- WILLIAM LUKUVI
Waziri wa Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, amepigiwa kura na wasomaji wengi, wakimpongeza kwa jinsi anavyoshughulikia migogoro sugu ya ardhi ambayo kwa kipindi kirefu ilikuwa ikiwatesa wananchi. Pia kutafuta suluhu ya migogoro baina ya wafugaji na wakulima, inayohusu ardhi.
- PROFESA MAKAME MBARAWA
Profesa Makame Mbarawa ambaye awali alikuwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kabla ya kuhamishiwa Wizara ya Maji na Umwagiliaji, naye amepigiwa kura nyingi kutokana na uwajibikaji mkubwa aliouonesha akiwa katika wizara yake ya awali.
Akiwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Waziri Mbarawa alikuwa akiongoza kwa kutokaa ofisini, muda mwingi alikuwa akitembelea na kukagua miradi mbalimbali iliyopo chini ya wizara yake, kama ujenzi wa barabara na miundombinu mingine. Ari hiyo ameendelea nayo hata baada ya kubadilishiwa wizara na kupelekwa Wizara ya Maji na Umwagiliaji.
- UMMY MWALIMU
Waziri wa Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu naye anaingia katika orodha hii kutokana na kura nyingi alizopigiwa.
Wasomaji wengi wameonesha kuridhishwa na utendaji kazi wake, hasa katika kushughulikia matatizo yanayowakabili wanawake na watoto, upatikanaji wa huduma za afya, madawa na vifaa tiba mpaka vijijini sambamba na ubora wa huduma zinazotolewa na hospitali zetu, ikiwemo Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
- SELEMAN JAFO
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Seleman Jafo pia amepigiwa kura, wengi wakionesha kuridhishwa na namna anavyowasimamia watendaji mbalimbali wa serikali, kuanzia ngazi ya chini kabisa, anavyoshughulikia kero za wananchi hasa zinazowahusu watendaji wabovu wa serikali na jinsi anavyotembelea maeneo mbalimbali ya nchi kutatua changamoto zinazowakabili wananchi.
- DKT. HAMIS KIGWANGALLA
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla, naye amepigiwa kura zilizomuwezesha kuingia kwenye orodha ya mawaziri kumi wachapakazi, ambapo sifa yake kubwa ni kutobweteka ofisini, badala yake mara kwa mara amekuwa akitembelea kwenye maeneo mbalimbali nchini, kufuatilia jinsi maliasili na vivutio vya utalii, vinavyotunzwa na kuendelezwa.
Pia amekuwa mstari wa mbele katika vita dhidi ya ujangili, akikutana na maafisa wanyamapori mara kwa mara kujadiliana nao kuhusu changamoto zinazowakabili na namna ya kuzitatua. Hivi karibuni alipata ajali mbaya ya gari, akiwa anatoka kwenye ziara ya kikazi mkoani Arusha, huu ukiwa ni uthibitisho wa namna anavyochapa kazi.
- HARRISON MWAKYEMBE
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe naye ameingia kwenye orodha hii, akitajwa kuwa mstari wa mbele kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili wizara yake, kuanzia kwenye masuala ya habari, sanaa na wasanii mpaka kwenye michezo.
Changamoto iliyotajwa na wengi, ni kwamba waziri huyu bado anayo kazi kubwa kuhakikisha maslahi ya wasanii wa Kitanzania, yanaboreshwa, mikataba ya kinyonyaji wanayoingia wasanii inatafutiwa ufumbuzi haraka na kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili waandishi wa habari, ikiwemo ya vyombo vya dola kutumia nguvu dhidi ya waandishi.
- JOYCE NDALICHAKO
Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi Profesa Joyce Ndalichako, ametajwa kuwa anachapa kazi vizuri na ndiyo maana kwa mara ya kwanza baada ya kipindi kirefu kupita, shule za serikali zimeanza kung’ara kwenye kumi bora za matokeo ya mitihani ya kitaifa, ukiwemo ule wa Kidato cha Sita ambapo Shule za Kibaha na Mzumbe zilizitoa kimasomaso shule za serikali.
- JENISTA MHAGAMA
Mwanamama Jenista Mhagama, Waziri wa Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, naye ameingia kwenye orodha hii kutokana na jinsi anavyoshughulikia changamoto mbalimbali zinazoikabili wizara yake.
- CHARLES MWIJAGE
Ni Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, anatajwa kwenda sambamba na kasi ya mheshimiwa rais ya kuhakikisha ‘Tanzania ya Viwanda’ inatimia.
Jitihada zake mbalimbali za kutengeneza mazingira mazuri ya uwekezaji, kuwatembelea wafanyabiashara sehemu mbalimbali na kuzungumza nao kuhusu changamoto zinazowakabili, pamoja na kuhamasisha ujenzi wa viwanda, ni miongoni mwa sifa zinazombeba.
MAKALA: MWANDISHI WETU
Comments are closed.