The House of Favourite Newspapers

Haya Mabasi ya Mwendo Kasi, Acha tu

0

DART (7)

Wiki mbili hizi jambo jipya limezuka katika Jiji la Dar es Salaam, jiji ambalo mambo mapya huzuka kila kukicha. Kumekuja aina mpya ya usafiri inaitwa mabasi ya mwendo kasi.

Wenye mabasi yao walitoa ofa ya kusafirisha abiria bure wiki nzima ili wakazi wa jiji hili waonje utamu wa usafiri huu. Wengi tulizunguka na mabasi haya bila kuwa na safari maalum ili tu kufaidi mabasi haya mapya, msema ukweli mpenzi wa Mungu.

Hili lilifanya wambeya waongee sana eti oo kuna watu hawataki kushuka, sasa ndiyo tulikuwa hatushuki nyie inawahusu nini? Nilikuwa naamka mapema napanda daladala kutoka kwetu mpaka kwenye kituo cha mabasi haya mapya ya bure, napanda na kuzunguka nayo siku nzima bila kushuka ili nifaidi usafiri wa bure, kuna raha yake kuzunguka Jiji la Darisalama.

DART (6)Lakini kuna mambo ambayo niliyakuta ambayo ni lazima niwataarifu ndugu zangu, hii itawasaidia kujua kitu cha kutegemea kukikuta kwenye usafiri huu mpya. Kwenye usafiri huu utawakuta watu ambao wananuka kikwapa, hawa huwa wanakuwa na maneno mengi na hawapendi kukaa kwenye viti wanang’ang’ania kusimama ili watanue mikono wakati wanashika bomba, bahati mbaya ukijikuta pua yako imebanwa kuelekea kwapa la mtu kama huyu, ujue uwezekano wa kuzimia kwa kukosa hewa safi ni mkubwa, wagomvi sana hawa ukiwaambia kuwa wananuka kikwapa.

DART (1)Wako wale ambao wameanza siku kwa kula mayai ya kuchemsha au walikula ugali kwa kabichi jana yake, hawa huwezi kuwatambua kwa kuwaangalia usoni, unaweza kukuta wamevaa vizuri tena kama mayanki kidogo utakuta wameweka iafon masikioni, suruali nusu mlingoti, hawa ni hatari sana, wanaweza kuchafua hali ya hewa ukataka kukimbilia nje ya basi wakati liko katika mwendo wa kasi.

DART (1)Wako hawa ndugu zangu ambao wana simu mpya,  usishangae kujikuta uko karibu na mtu ambaye anapiga simu kwa sauti kubwa akisimulia mambo yasiyowahusu kabisa.

Ukiingia kwenye usafiri huo jitayarishe kwa lolote.

Leave A Reply