Hii ya Msolla ni Rekodi, Yanga Yapata Bilioni 3.93

Mwenyekiti wa Yanga, Mshindo Msolla.

UONGOZI mpya wa Klabu ya Yanga ulioingia madarakani chini ya mwenyekiti wake, Mshindo Msolla na makamu wake, Frederick Mwakaleba umefanikiwa kukusanya shilingi 3,935,000,000 ndani ya miezi minne tangu walipoingia madarakani.

 

Viongozi hao waliingia madarakani Mei 5, mwaka huu baada ya kushinda kwa kishindo katika uchaguzi mkuu wa klabu hiyo.

Msolla na Mwakalebela kabla ya kuingia madarakani katika kampeni zao waliahidi kuipambania klabu hiyo kwa kuhakikisha wanaongeza vyanzo vya mapato kupitia udhamini mbalimbali wa makampuni.

 

Kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa na Championi Ijumaa, Yanga hadi hivi sasa ina udhamini wa makampuni saba ambayo yote yamemwaga mamilioni na mabilioni ya fedha. Makampuni na viwango vya fedha walizomwaga ni Kampuni ya Kubashiri Matokeo ya SportPesa iliyoweka udhamini wa Sh bilioni 1.94 ambao umeboreshwa hivi karibuni baada ya viongozi hao kuingia madarakani wakati awali walikuwa na mkataba wa Sh Mil 970.

Kampuni nyingine ni GSM walioshinda tenda ya uuzaji wa jezi za Yanga iliyotoa Sh bilioni 1.3, pia kampuni hiyo imeongeza fedha kwa kutoa Sh milioni 150 ya udhamini kupitia magodoro yao ya GSM. Wadhamini wengine ni Taifa Gas chini ya mfanyabiashara, Rostam Aziz ambapo wamekubali kutoa Sh 300m kwa ajili ya udhamini, ambapo tayari Yanga wameshaanza kuvaa jezi zenye nembo ya mdhamini huyo begani.

 

Dili lingine ni kuwa Azam TV wanaonyesha kipindi cha Yanga TV ambapo kupitia kipindi hicho Yanga wananufaika kwa kupata Sh milioni 100, udhamini mwingine ni Afya Maji wenye thamani ya Sh milioni 100 huku Vodacom wanaodhamini Ligi Kuu Bara wakiinufaisha klabu hiyo kwa Sh milioni 45.

 

Jumla ya udhamini wote ni Sh bilioni 3.93 ambazo viongozi hao wapya wamezipata ndani ya kipindi kifupi cha miezi minne.

Akizungumzia hilo juzi kwenye kikao cha viongozi wa matawi wa Yanga kilichofanyika kwenye Makao Mkuu ya Klabu ya Yanga, Msolla alisema: “Mpaka hivi sasa Yanga ina mkataba na Sportpesa ambao mwaka huu watatoa Sh bilioni 1.94. “Uongozi umefanikiwa kupata mikataba na Taifa Gas kutoka kwa Rostam ambao watatoa milioni 300, lakini pia ushirikiano na mheshimiwa Rostam bado upo, ndiye aliyetoa Sh milioni 60 kuvunja mkataba wa Kindoki na fedha za kumleta Molinga Yanga.

 

“Mkataba wa kwanza na GSM ni ule wa jezi ambao klabu itapata shilingi 1,300 kwa kila jezi itakayouzwa na lengo ni kuhakikisha jezi milioni moja zinauzwa ili klabu ipate Sh bilioni 1.3, pia mkataba unahusisha ukarabati wa Jengo la Yanga.

 

“Mkataba wa pili na GSM unahusisha magodoro ya GSM mkataba huu una thamani ya milioni 150, pia klabu ipo mbioni kuongeza mdhamini mwingine kutoka kampuni ya vinywaji atakayetoa fedha kama ilivyofanya SportPesa na kukarabati ‘pitch’ ya Uwanja wa Kaunda uwe wa kisasa kutumika katika mazoezi, ndiyo maana zoezi la kuweka kifusi linaendelea kwa kasi,” alisema Msolla.

Stori na Wilbert Molandi, Dar es Salaam


Loading...

Toa comment