The House of Favourite Newspapers

Hiki Ndicho ‘Kinachokula’ Afya ya Ruge na Seth

DAR ES SALAAM: Walipofikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Juni 19, 2017, Harbinder Seth na James Rugemalira, wengi walishtuka; ‘hee! vigogo hawa nao wamepanda kizimbani?’ ikawa gumzo kila kona.

 

Seth na Rugemalira waliwashangaza wengi tena Juni 21 mwaka huu, mara hii si kwa kufikishwa kwao mahakamani bali muonekano dhoofu wa miili yao.

Kutokana na hali ya huzuni waliokuwa nayo, baadhi ya watu wakiwemo ndugu ambao wachache kati yao walionekana kububujikwa na machozi walipowaona watuhumiwa hao wa uhujumu uchumi, Wikienda likaona kuna ‘uzi’ wa kufuatilia kujua nini kinachodhoofisha afya yao.

 

MSHTUKO MAHAKAMANI

“Heee! Jamani mbona wamekonda hivyo. Yaani wanatia huruma.”

“Wanasema Seth anaumwa; vyombo vya habari vimekuwa vikiripoti kuwa ana puto tumboni.”

“Wote walikamatwa wakiwa na hali nzuri tu, kama ni magonjwa basi watakuwa wameyapata huko mahabusu, wanasikitisha kwa kweli.”

Hizi ni kauli zilizotolewa na baadhi ya watu waliofika mahakamani, Alhamisi iliyopita kusikiliza mashtaka 12 ya uhujumu uchumi yanayowakabili Rugemalira na Seth ambapo masikitiko ya wengi yalikuwa kwenye afya zao.

 

WIKIENDA LACHIMBA SABABU

“Ukisema mahabusu ni kubaya moja kwa moja kwa kila anayeingia kusingekuwa na watuhumiwa wanaotoka huko wakiwa hai, lakini mbona wengine wako ‘fiti’ na maisha yanakwenda; kwa nini Rugemalira na Seth wadhoofike namna hiyo?” alihoji Kassim mmoja kati ya wachangiaji kwenye moja ya mtandao wa kijamii wa Twitter uliojadili pia afya za watuhumiwa hao.

 Wikienda lilipoona hoja zinakuwa nyingi likaona limtafute mwanasaikolojia ili azungumzie kitaalamu hali ya afya wa Rugemalira na Seth ambao mwaka mmoja uliopita walikuwa wakitumbua maisha kifahari uraiani.

 

“Yako mambo mengi yanayoweza kumfanya mtu aliyefugwa au kuwepo mahabusu kudhoofika kiafya; mojawapo unaweza kuwa ni ugonjwa au matatizo mengine yatokanayo na msongo wa mawazo.

“Mtu asipokuwa huru kufanya atakavyo anaweza kudhoofu mwili, akikosa chaguo la chakula, kuwa mbali na awapendao, kuondolewa mamlaka na kuwa chini ya amri ni mambo yatakayomfanya apatwe na msongo wa mawazo.

 

“Msongo huo ukikomaa, atapoteza hamu ya kula, atachoma seli nyingi za mwili, atapungua uzito kwa kasi na kujikuta mwili unapoteza kinga kwa kiwango kikubwa ambacho ni rahisi kwake kupatwa maambukizi mapya au kufumuka kwa magonjwa ambayo yalikuwa yakidhibitiwa na seli kinga za mwili ambazo kwa wakati huo zinakuwa zimeshuka,” alisema Mwanasaikolojia Dk. Chriss Mauki, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

 

USHAURI WA WOTE

Mwanasaikolojia huyo alitoa ushauri kwa si kwa Rugemalira na Seth tu bali kwa wote wanaopatwa na matatizo kwamba, wanapojikuta kwenye wakati mgumu njia pekee ya kujiweka salama kiafya ni kukubaliana na maisha mapya bila kujiona mnyonge kupita kiasi.

Jambo jingine aliloshauri ni kuacha kuishi kwa hisia zilizo nje na hali halisi hasa inayozunguka mazingira yaliyopo karibu kwani kufanya hivyo kunaweza kukusababishia majibu tofauti na uweli uliopo.

 

HITIMISHO

Kesi ya Rugemalira na Seth watuhumiwa wanaooneka kuanza kupata sehemu ya huruma za baadhi ya wananchi hasa kutokana na kudhoofu afya zao kusikokuwa kwa kawaida, bado inaendelea kunguruma kwenye Mahakama ya Kisutu, Dar ambapo mpaka sasa wamekaa mahabusu kwa takriban mwaka mmoja.

 STORI: Mwandishi Wetu,  IJUMAA WIKIENDA

Comments are closed.