The House of Favourite Newspapers

 MOBETO AUMBUKA NYUMBA ALIYOPEWA NA DIAMOND

DAR ES SALAAM: Ameumbuka! Ndivyo unavyoweza kusema. Wakati tabia ya mastaa kuanika mijengo yao ya gharama ikizidi kushika kasi, mwanamitindo Hamisa Mobeto amejikuta akiumbuka baada mjengo aliodaiwa kununuliwa na mzazi mwenzie Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’, kubainika kuwa hajanunuliwa kama ambavyo mama yake Mobeto, Shufaa Rutiginga amekuwa akidai.

Nyumba hiyo iliyopo maeneo ya Tegeta-Bahari Beach ilizua gumzo mitandaoni mara baada ya gazeti dugu na hili la Amani, kuichapisha kwa mara ya kwanza hivi karibuni.

 

GUMZO LENYEWE…

Kufuatia usiri mzito uliokuwepo juu ya makazi hayo ya Mobeto, mara baada ya nyumba hiyo kupamba ukurasa wa mbele wa Amani, gumzo lilikolezwa mitandaoni kwa watu kuhoji kama ni kweli amepangiwa au amenunuliwa na Diamond.

Wale ambao ni mashabiki wa Mobeto walijitapa kuwa mjengo huo ni maalumu kwa mtoto wa Diamond aliyezaa na Mobeto, Prince Dylan lakini wale wasio mashabiki wake, waliponda kwa kusema mjengo huo wamepangiwa tu.

“Mobeto bwana, kila siku tunamuona anaiposti nyumba hiyo kudhihirisha kwamba ni yake wakati si kweli halafu (Mobeto) ukweli anaujua lakini hataki kuanika licha ya sisi kupiga kelele mitandaoni,” aliponda mdau aliyejitambulisha kwa jina la Kikumba katika mtandao wa Instagram.

MAMA’KE ACHOCHEA MOTO

Wakati kitendawili cha amepangiwa au amenunuliwa kikiwa hakijateguka, mama yake Mobeto, Shufaa Rutiginga aliibuka na kudai nyumba hiyo Diamond amemnunulia mtoto aliyezaa na bintiye, Prince Dylan hali iliyoamsha moto zaidi kwa wafuasi wa mitandao.

Kwenye mahojiano hayo, mama Mobeto alisikika akimshukuru Diamond kwa kumnunulia mjengo huo mjukuu wake ndipo watu walipoanza kumshambulia.

“Mh! Mbona jamani tumesikia hii nyumba amepangiwa na si kwamba amenunuliwa? Hivi hizi kiki jamani tutafika kweli? Kwani mtu ukisema ukweli utapungua nini?” alihoji mdau mmoja katika mtandao wa Instagram.

 

WAUMBUKA

Ili kujiridhisha zaidi na ubuyu huo, Ijumaa Wikienda liliingia mzigoni kuchimbua ukweli wa kauli ya mama pamoja na ukimya wa bintiye katika kusema ukweli, ndipo lilipobaini ukweli kwamba nyumba hiyo Mobeto amepangiwa.

TUMSIKILIZE JIRANI

Jirani mmoja wa Mobeto aliyeomba hifadhi ya jina, alipoibukiwa na wanahabari wetu, aliweka wazi kuwa nyumba hiyo hajanunuliwa na ameshangazwa na habari kwamba amenunuliwa.

“Kwa kweli nimeamini hawa mastaa wanapenda kujikweza, yaani nyumba hii tumeona mchakato wote na mwenye nyumba tunamjua lakini mitandaoni tunaona mama Mobeto anasema Diamond kawanunulia,” alisema jirani huyo huku akitaja jina la mmiliki wa nyumba hiyo (jina tunalihifadhi).

 

JIRANI AZIDI KUFUNGUKA

Jirani huyo alienda mbali zaidi kwa kutaja siku ambayo mmiliki wa nyumba hiyo huwa anafika kwa ajili ya kushughulikia wateja wake kwani mbali na nyumba hiyo aliyompangisha Mobeto, anazo nyumba nyingi alizopangisha maeneo hayohayo.

“Njooni Jumamosi mara nyingi huwa anakuja na mnaweza kuzungumza naye akawapa ukweli wa mambo wote maana nimesikia pia hakufurahishwa na kitendo cha mitandao kuandika kuwa nyumba imenunuliwa wakati ukweli ni kwamba wamepanga,” alisema jirani huyo.

BALOZI ATHIBITISHA

Balozi wa nyumba kumi, Mtaa wa Fahari, Cloud Kayako alipoulizwa na mwanahabari kama nyumba hiyo amepangishiwa na kwamba mwenye nyumba hakufurahishwa na taarifa za Mobeto kununuliwa nyumba hiyo, alikiri kwamba ni kweli mwenye nyumba hakufurahishwa na habari hiyo.

“Huyu ni kweli amepanga hapa sasa zilipokuja hizo taarifa za kwamba amenunua kwa kweli hata mwenye nyumba kashangaa,” alisema balozi huyo huku akiwataka waandishi kuzungumza na mmliki ili kuweza kupata habari zaidi.

 

IJUMAA LAIBUKA NYUMBANI

Baada ya kuelezwa kuwa mmiliki huwa anafika kwenye nyumba hizo siku ya Jumamosi, Ijumaa Wikienda lilitinga nyumbani hapo lakini bahati mbaya lilishindwa kuzungumza naye kutokana na ubize aliokuwa nao.

NDUGU WA MMILIKI ANENA

Mara baada ya mmiliki kufika na kuwa bize na wapangaji wake wengine, ndugu wa mmliki aliyeomba hifadhi ya jina alisema kama familia walishangazwa na habari za kwamba Mobeto amenunuliwa nyumba hiyo.

“Mimi mwenyewe niliona kwenye mtandao kwamba wamenunua, nikashtuka sana ikabidi niende kumuonesha babu (mmiliki), akasema si kweli ndipo wakapuuza tu maana,” alidai ndugu huyo.

Hivi karibuni, mastaa wa kike wa Bongo Muvi akiwemo Irene Uwoya, Aunt Ezekiel, Kajala Masanja na Wema Sepetu wamekuwa na kasumba ya kuinadi mijengo yao mtandaoni na kuzua gumzo.

Watu wamekuwa wakiwakosoa kwa kitendo cha kuinadi mijengo hiyo kwani baadhi yao wamekuwa wakiongopa kwamba ni zao kwa maana wamenunua wakati kiuhalisia si kweli. Kama hiyo haitoshi, kuna wengine wamedaiwa kuvumisha kuwa wanamiliki majengo mazima wakati ukichunguza inakuwa ni upande mmoja na si nyumba nzima.

Ijumaa Wikienda limeanza kuifanyia kazi habari hiyo, soon litawaanika mmoja baada ya mwingine.

STORI: Neema Adrian, IJUMAA WIKIENDA

Comments are closed.