The House of Favourite Newspapers

Historia ya Basil Mramba, Uwaziri Mpaka Kufungwa Gerezani

0

MWANASIASA mkongwe aliyewahi kushika nyadhifa mbalimbali za uongozi ikiwemo kuwa Waziri wa Fedha katika Serikali ya Awamu ya Tatu, Basil Mramba amefariki dunia Jumanne ya Agosti 17, 2021 jijini Dar es Salaam wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Regency.

 

Ifuatayo ni historia fupi ya Mramba kuanzia kuzaliwa, elimu, siasa na mambo mbalimbali aliyoyapitia katika maisha yake, ikiwemo kufungwa gerezani. Basil Mramba alizaliwa Mei 15, 1940 na amefariki akiwa na umri wa miaka 81.

 

Alianza elimu ya msingi katika Shule ya Kwaleina Bush School mwaka 1948 na mwaka mmoja baadaye, akahamia katika Shule ya Msingi Shimbi alikosoma mpaka mwaka 1952. Mwaka uliofuatia, 1953 alijiunga na Shule la Mkuu Mission Primary School alikosoma mpaka mwaka 1954 na kuhitimu elimu ya msingi.

 

Mwaka 1955, alijiunga na Shule ya Sekondari Umbwe alikoanza elimu ya sekondari na kusoma mpaka mwaka 1960. Mwaka 1961 alijiunga na Shule ya Sekondari ya Wavulana Tabora (Advance Level) na kusoma kidato cha tano na sita na kuhitimu mwaka 1962.

 

Baada ya kuhitimu elimu ya juu ya sekondari, Mramba alijiunga na Chuo Kikuu cha Makerere, Uganda ambako alisomea shahada yake ya kwanza katika masuala ya siasa kuanzia mwaka 1963 hadi 1967 alipohitimu.

 

Mwaka huohuo, Mramba alijiunha na Chuo Kikuu cha City University Graduate School cha London nchini Uingereza akisomea Shahada ya Uzamili na kuhitimu mwaka 1968.

 

Baada ya hapo, aliajiriwa na Kampuni ya Williamson Diamond, Mwadui Shinyanga akiwa kama msaidizi katika masuala ya utawala, ajira aliyoendelea nayo mpaka mwaka 1969.

 

Mwaka 1969, aliajiriwa na Shirika la Maendeleo (NDC) akiwa kama mkurugenzi wa nguvukazi, akaendelea na kazi hiyo mpaka mwaka 1972. Wakati akiendelea na kazi, Mramba aliamua kujiendelea kielimu, akajiunga na Chuo Kikuu cha Havard Business School cha nchini Marekani, akisomea cheti cha usimamizi wa biashara mwaka 1971.

 

Baadaye, alijiunga na Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogovidogo (SIDO) akiwa kama Mkurugenzi na akaendelea na kazi mpaka mwaka 1980.

 

ALIVYOINGIA KATIKA SIASA

Mramba aliingia kwenye siasa mwaka 1980 na kugombea Ubunge wa Jimbo la Rombo, akadumu mpaka mwaka 1987. Baadaye alirejea tena bungeni mwaka 1995, akateuliwa na Rais Benjamin William Mkapa kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, nafasi aliyoishika mpaka mwaka 2000.

 

Akaendelea kushinda ubunge katika jimbo hilo kwa vipindi kadhaa mfululizo na kwa mara nyingine, aliteuliwa kuwa Waziri wa Fedha, wadhifa alioushika kuanzia mwaka 2000 hadi mwaka 2005.

 

Mwaka 2006, aliteuliwa kuwa Waziri wa Miundombinu, mwaka huohuo akahamishwa wizara na kupelekwa Wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko kuanzia Oktoba 10, 2006 hadi mwaka 2008.

 

ALIVYOPANDISHWA MAHAKAMANI NA KUHUKUMIWA

Mwaka 2015 haukuwa mzuri kwa Basil Mramba na mwenzake, Daniel Yona ambapo walikamatwa na kushitakiwa katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, wakituhumiwa kuisababishia serikali hasara ya shilingi bilioni 11.7 kupitia misamaha ya kodi.

 

Kesi hiyo ilinguruma kwa muda mrefu na hatimaye, mawaziri hao wa zamani walikutwa na hatia kwa kosa la matumizi mabaya ya ofisi na kusababishia serikali hasara, wakahukumiwa kifungo cha miaka mitatu gerezani na faini ya shilingi milioni tano baada ya kukutwa na hatia ya matumizi mabaya ya madaraka.

 

Baadaye walijaribu kukata rufaa lakini Oktoba 2, 2015 Jaji Projest Rugazia alitupilia mbali rufaa yao lakini akawapunguzia adhabu kutoka kifungo cha miaka mitatu gerezani hadi miwili na kufuta faini ya fedha hizo.

 

Baada ya kutumikia sehemu ya kifungo chao gerezani, hatimaye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, iliwabadilishia adhabu na wakatakiwa kutumikia kifungo cha nje sambamba na kufanya usafi katika maeneo ya jamii.

 

Mramba na mwenzake walipangiwa kutumikia adhabu ya kufanya usafi kwenye Hospitali ya Sinza Palestina jijini Dar es Salaam kwa saa nne za kila siku.

IMEANDALIWA NA HASHIM AZIZ | GLOBAL PUBLISHERS

 

Leave A Reply