The House of Favourite Newspapers

Simanzi! Wanne wa Familia Moja Wafariki!

SIMANZI nzito imetanda kila kona baada ya watu wanne wa familia moja kupoteza maisha ghafla wakiwa ndani ya nyumba yao, Risasi Jumamosi lina mkasa huu wa kukutoa machozi A-Z.

NI NGARA, KAGERA

 

Tukio hilo la kusikitisha kila anayelisikia lilitokea usiku wa kuamkia Juni 25, mwaka huu katika familia ya Abubakar Ramadhani (41), Mkazi wa Wilaya ya Ngara mkoani Kagera kutokana na ajali ya moto ambao chanzo chake hakikujulikana mara moja.

 

KAMANDA MALIMI

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kagera, ACP Revocatus Malimi alilieleza Risasi Jumamosi kuwa, tukio hilo lilitokea katika Kijiji cha Omulukukumbo, Kata ya Kabanga wilayani Ngara, Kagera na kusababisha vifo hivyo.

 

ANUSURIKA MTOTO MMOJA TU

Alisema kwenye familia hiyo alinusurika mtoto mmoja tu ambaye naye alijeruhiwa mno na sasa amelazwa kwenye Hospitali ya Omulugwanza na hali yake ni mbaya kiasi cha kusikitisha.

Kamanda Malimi alieleza kuwa, tukio hilo liligundulika Juni 25, mwaka huu, majira ya saa moja asubuhi kwani hakukusikika kelele zozote za kuomba msaada usiku huo.

Alisema majirani waligundua hali hiyo asubuhi na kutoa taarifa polisi ambapo walifika eneo la tukio mara moja.

 

WALIOFARIKI DUNIA

Aliwataja waliopoteza maisha kwenye tukio hilo kuwa ni baba wa familia hiyo, Abubakar ambaye alikuwa ni dereva na mkewe, Suzi Abubakari (36) aliyefia hospitalini wakati akiendelea kupatiwa matibabu baada ya kukutwa akiwa mahututi.

Wengine ni watoto wa Abubakar na Suzi, Ramlati Abubakar (4) na Mariam Abubakar (7) ambaye alikuwa ni mwanafunzi wa darasa la kwanza katika Shule ya Msingi ya Kabanga.

Kamanda huyo alimtaja mtoto aliyenusurika kwenye tukio hilo ambaye yupo katika Hospitali ya Omulugwanza akiendelea kupatiwa matibabu, lakini hali yake ikiwa ni mbaya kuwa Ashiraf Abubakari (5).

 

CHANZO HAKIJAJULIKANA

Kamanda Malimi alisema kuwa, chanzo cha tukio hilo lililoacha majonzi kwa wananchi wa eneo hilo hakijajulikana hivyo jeshi hilo bado linafanya uchunguzi wa kina ili kugundua.

 

HAKUNA ALIYEKAMATWA

Pia kamanda huyo wa polisi alisema hakuna aliyekamatwa kuhusiana na tukio hilo huku miili ya wanafamilia hao ikizikwa juzi na ndugu, jamaa na marafiki kijijini hapo.

 

WANAKIJIJI WANASEMAJE?

Abyalimana Pascal, mkazi wa kijiji hicho cha Omulukukumbo alilieleza Gazeti la Risasi Jumamosi kuwa baada ya kugundua tukio hilo walijitahidi kubomoa nyumba kuona kama wangeweza kuwaokoa, lakini ilikuwa bahati mbaya kwani walipofanikiwa kuingia ndani walikuta watoto wawili na baba yao wakiwa wameshafariki dunia huku wakiwa wamekumbatiana.

 

Alisema kuwa, walipotupa macho walimuona mama wa familia hiyo, Suzi na mwanaye mmoja wakiwa katika hali mbaya mno, nao wakiwa wamekumbatiana ndipo wakawakimbiza Hospitali ya Omulugwanza ili kuokoa maisha yao.

Alisema kuwa, hata hivyo, kwa bahati mbaya, Suzi alifariki dunia akiwa anapatiwa matibabu hivyo kukamilisha idadi ya watu wanne wa familia moja kufa kwa siku moja.

 

“Kiuweli inauma sana. Haijawahi kutokea hali kama hii hapa kijijini kwetu. Ni tukio ambalo limeacha sintofahamu kubwa sana.

“Kinachoshangaza ni kwamba hakuna mtu aliyesikia moto huo wala hakuna aliyesikia wanafamilia hao wakiomba msaada.

 

“Kiukweli hakuna mwanakijiji wa Omulukukumbo ambaye hajaguswa na tukio hili.

“Wengine wanalihusisha na ushirikina, lakini wengine wanadai kuna mtu amefanya hivi.

“Lakini sisi tunaamini jeshi letu la polisi litafanya uchunguzi wake na majibu yatapatikana ili kuondoa sintofahamu na taharuki iliyopo kijijini hapa,” alisema Pascal kwa masikitiko makubwa.

KAGAME: Mwanaume Aliyeitoa RWANDA Machinjioni Mpaka PEPONI!

Comments are closed.