The House of Favourite Newspapers

HUKU NI ‘KUDAMSHI’ AU KUJICHORESHA?

SINA shaka kabisa na hili suala la fasheni za nguo ambazo kila kukicha zimekuwa zikiibuka huko mtaani. Wanawake wanashindana kwa mishono yao, ikiwa ni katika kutaka waonekane nao wamo na kuzifurahisha nafsi zao.  

Hata hivyo, niwaambie kitu kimoja ambacho yawezekana hamkijui. Wanawake wanapoteza pesa nyingi sana kwenye suala mavazi. Staili mpya ikiingia, wengi wao wanataka waipate kwa gharama yoyote. Watajibana, watacheza michezo, watakopa, watakula ugali na dagaa ili tu wapate pesa za kununulia nguo ambazo zimeingia sokoni.

 

Lakini tunapowazungumzia wanawake, ndani yake wamo hawa mastaa ambao nao wakose yote lakini siyo kupitwa na fasheni za nguo zinazotrend mjini. Ndiyo maana ukifuatilia sana utakuta kuna ambao kwenye makabati yao ya nguo wana kila fasheni, kila staili, kila dizaini, yaani ili mradi tu waonekane wanakwenda na wakati.

 

Mimi kwenye hilo la kwenda na wakati sipingani nalo ila ninachojiuliza ni kwamba, unawezaje kwenda na wakati katika suala mavazi huku ukijidhalilisha? Nasema hivyo kwa sababu wewe msomaji wangu huenda ukawa shahidi wa namna ambavyo hawa mastaa wetu wa kike hawaziheshimu kabisa sehemu zao za siri.

Yaani staa yuko tayari kuvaa mshono unaomuonesha hadi nguo yake ya ndani lakini hajali, ili mradi aonekane amevaa fasheni iliyotoka jana ambayo bei yake iko juu. Huku ni kujichoresha na nikuambie tu kwamba, kama atatokea mtu na kukuambia umedamshi wakati sehemu kubwa ya kifuani iko wazi, mapaja yote umeyaanika basi huyo atakuwa anakusanifu.

 

Naandika makala haya baada ya hivi karibuni kuwashuhudia wadada watatu mastaa ambao wote wanaitwa mama, wakiwa wamevaa mavazi ambayo hayakuwa ya kimama kabisa. Nawazungumzia; Irene Uwoya, Shamsa Ford na Asma Khan ‘Asma Platnumz’. Hii ilikuwa kwenye ile ‘bethidei pati’ ya Wema Sepetu iliyofanyika pale Mlimani City. Walikuwepo mastaa wengi. Nilimuona Jennifer Kyaka ‘Odama’ akiwa amevalia gauni lake refu, Halima Yahaya ‘Davina’ naye akapiga kitu chake cheupe flani hivi, wakawa wamedamshi ile mbaya.

Lakini niliwaona Irene, Shamsa na Esma wakiwa wamevaa magauni marefu yaliyokuwa na mipasuo kama yote. Kwa kifupi, sehemu zao kubwa za miili yao ambazo tusingependa kuziona zilikuwa wazi. Mpasuo wa Irene ndiyo ulikuwa kiboko maana ulikaribia kitovuni.

 

Wote hao niliowataja, hawakuishia kwenye mipasuo, hata fasheni ya vifuani kwao ilikuwa wazi, matiti yamebaki kidogo yawe nje, mgongo kama wote, ikawa ni shida tupu. Inafika wakati unajiuliza, hii yote ni ili iweje? Ndiyo huo ustaa unawataka kuvaa hivyo? Na je, wanakumbuka kuwa wao ni kioo cha jamii?

 

Matokeo yake sasa huko mtaani nako wanakopi na kupesti. Wadada wanatamani kutembea uchi kabisa. Hii ni kuipeleka jamii kusiko. Ifike wakati nyie mastaa mshike adabu zenu, tumechoka na mavazi yenu haya ya ajabuajabu ambayo mtu mwenye akili zake timamu hawezi kukuambia umedamshi ukajiona mjanja, atakuwa anakusanifu huyo! Kikubwa ni kutafakari kila aina ya nguo ambayo utavaa. Utaangalia unakwenda wapi, uvaeje na kuiacha heshima yako kwa jamii iendelee kuwepo.

Comments are closed.