INASIKITISHA! MWANAFUNZI ATEKWA, AUAWA – VIDEO

MOROGORO: Maskini mtoto wa watu! Ndivyo walivyosikika mashuhuda wa tukio la mwanafunzi Doricka Majeshi anayesemekana kutekwa kisha kukutwa akiwa ameuawa na watu wasiojulikana ndani ya nyumba inayoendelea kujengwa na kuibua simanzi nzito, Ijumaa Wikienda lina ripoti.

Kwa mujibu wa mashuhuda hao, Mtoto Doricka mwenye umri wa miaka nane aliyekuwa anasoma darasa la kwanza katika Shule ya Msingi ya Lukobe mjini hapa, alidaiwa kukutwa na mkasa huo tangu Jumanne ya wiki iliyopita kisha kusakwa kwa siku tatu bila mafanikio, kabla ya mwili wake kukutwa ukiwa na majeraha Alhamisi iliyopita nyuma ya nyumba hiyo.

 

 

MTAA WAZIZIMA

Mauaji hayo yaliyosababisha mtaa kuzizima yalijiri kwenye nyumba hiyo iliyopo Mtaa wa Tushikamane katika Kata ya Lukobe nje kidogo ya Mji wa Morogoro.

Mtoto huyo alikuwa akiishi jijini Mwanza na wazazi wake kabla ya kuchukuliwa na mama yake mkubwa aitwaye Upendo, mwishoni mwa mwaka jana kwa lengo la kusoma mkoani hapa ambapo Januari, mwaka huu alianza darasa la kwanza katika shule hiyo.

 

 

ASAKWA KILA KONA

Baada ya walezi hao kuripoti kwenye serikali ya mtaa na polisi kisha kumsaka Doricka kila kona bila mafanikio na kukata tamaa ndipo Alhamisi iliyopita, wasamaria wema walipoushuhudia mwili wa mtoto huyo akiwa ameshauawa na kuachiwa majeraha ya kipigo huku damu zikiwa zimesambaa eneo la tukio.

 

 

UMATI ENEO LA TUKIO

Baada ya kuushuhudia mwili huo, wasamaria wema hao ndiyo waliotoa taarifa kwa mwandishi wetu ambaye alifika eneo la tukio na kushuhudia umati mkubwa ukiangua vilio huku mwili wa mtoto Doricka ukionekana kuchuruzika damu nyingi.

Likiwa eneo la tukio, Ijumaa Wikienda liliwashuhudia polisi wakiwasili na kuuchukua mwili wa mtoto Doricka kisha kwenda kuuhifadhi Mochwari ya Hospitali ya Mkoa wa Morogoro kwa ajili ya uchunguzi (post-mortem).

Wakati polisi wakiondoka na mwili huo, mama mkubwa wa mtoto huyo aliamua kulifukuza kwa miguu kwa uchungu, akitaka kumuona mwanaye.

Hata hivyo, mama huyo alijikuta akianguka na kupewa msaada na majirani.

 

 

MAMA ASIMULIA MKASA

Huku akiwa na simanzi kubwa, Ijumaa Wikienda lilizungumza na mama huyo juu ya mkasa huo ambapo alikuwa na haya ya kusema:

“Nina mdogo wangu wangu anaitwa Mariam Majeshi, anaishi Mwanza. Nilimuomba anipe Doricka, aje asome huku.

“Kweli, mwaka jana mdogo wangu alimleta Doricka na Januari, mwaka huu alianza darasa la kwanza kwenye Shule ya Msingi Lukobe.

 

“Kama unavyojua, Wakristo tupo kwenye mfungo wa Kwaresma hivyo Jumanne (wiki iliyopita), majira ya saa 10:00 nilijiandaa kwenda kanisani kwenye maombi.

“Nilimpa maagizo dada wa kazi kuwa ikifika saa 12:00 amuandae Doricka, aende tuisheni.

 

“Cha ajabu, hadi giza linaingia, Doricka hakurudi ndipo tukaanza kumtafuta bila mafanikio.

“Baada ya kumtafuta usiku kucha, kulipokucha Jumatano, tulitoa taarifa kwenye serikali ya mtaa ambao nao walitoa matangazo sehemu mbalimbali ikiwemo msikitini kisha polisi.

 

“Juhudi hizo hazikuzaa matunda hadi mchungaji wangu alipokuja nyumbani kunieleza kwamba, kuna mtoto wa kike ameuawa kwenye nyumba inayojengwa. Niliposikia hivyo nilijua tu ni Doricka wangu.

 

“Nilijikaza na kwenda eneo la tukio, nilipokaribia nilimshuhudia kaka yangu akiwa ameinamisha kichwa akiangua kilio. Moja kwa moja nikajua ni Doricka. Kweli niliposogelea zaidi, nikamuona mwanangu asiye na hatia na ni mgeni hapa Morogoro akiwa ameuawa kinyama.”

 

Baadhi ya mashuhuda waliozungumza na Ijumaa Wikienda walilihusisha tukio hilo na matukio ya utekaji huku wengine na mmoja wa wajumbe wa serikali ya mtaa wakidai ni ushirikina.

Akizungumzia tukio hilo, mwenyekiti wa serikali ya mtaa huo, Saidati Kitinde alithibitisha kutokea kwa mauaji hayo kwenye mtaa wake.

Mama mtoto.

 

 

KAMANDA WA POLISI

Juzi Jumamosi, Ijumaa Wikienda lilimtafuta Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, ACP Ulrich Matei ili kujua kama kuna mtu yeyote aliyekamatwa juu ya mauaji hayo ambapo alisema yupo safarini Mikumi, lakini akirejea Morogoro atalitolea ufafanuzi tukio hilo.

STORI: Dustan Shekidele, IJUMAA WIKIENDA

MASKINI MTOTO HUYU! Atekwa na Kuuawa, Mama Mzazi Hoi!

Loading...

Stori zinazo husiana na ulizosoma

Toa comment