The House of Favourite Newspapers

Insane (Mwendawazimu) 13

Theo akaelekea nyumbani kwao huku akiwa na furaha tele, kile alichokuwa amekipanga kwa muda mrefu hatimaye alifanikiwa na muda huo ulikuwa wa kujipongeza kwa kazi kubwa aliyokuwa ameifanya.

Alipofika nyumbani, akaelekea katika chumba cha kupumzikia alipokuwa baba yake kwa lengo la kumjulia hali. Alipofika huko, macho yake yakatua kwa watu wawili, Esther na mwanaume ambaye hakuwa akimfahamu.

Hakuwasalimia zaidi ya kumsogelea baba yake na kumjulia hali. Alimchukia Esther, alimuacha na kuwa na mwanaume ambaye alikuwa na uhakika kwamba kipindi hicho alikuwa marehemu. Hakumwangalia usoni, akajifanya kama hakumuona.

Akasomewa mashitaka juu ya kile kilichokuwa kimeletwa. Kwanza hakujibu, akatulia kwa muda na kisha kumwangalia Esther. Alichukia, ni kweli alifanya hivyo lakini hakutaka kujionyesha.

“Nimteke Fabian, ili iweje?” aliuliza Theo huku akionekana kuwa na hasira.

“Nisikilize kijana. Hatujaja hapa kukutuhumu bali tuna uhakika kwamba umehusika kwa asilimia mia moja, ninakwambia hivi, ninamtaka kijana wangu vinginevyo nitakufanyia kitu kibaya sana,” alisema Mzee Boniface huku akionekana kukasirika.

“Utanifanya nini wewe mzee?” aliuliza Theo kwa kiburi, tena huku akitunisha kifua chake mbele kama bata.

Wakaanza kugombana kwa maneno, Theo hakutaka kukubali, alimtukana sana mzee Boniface kwani alijua fika kwamba mzee huyo asingeweza kumfanya kitu chochote kile, tena nyumbani kwao.

Mzee huyo alilalamika sana, moyo wake ulimwambia kwamba alikuwa na uhakika kwamba Theo ndiye ambaye alihusika kumteka Fabian kwa kile kilichokuwa kimetokea nyuma.

Alitamani kumpiga, moyo wake ulikuwa na hasira tele na muda wote alikunja sura. Theo hakuogopa, bado alijiona kuwa mbabe mpaka watu hao walipoondoka nyumbani hapo huku wakimpa siku mbili tu, vinginevyo wangemuua.

Theo hakuogopa, alibaki nyumbani hapo huku akimuuguza baba yake aliyeonekana kuwa na hali mbaya, mama yake, Bi Rachel  alikuwa pembeni, muda wote alionekana kuwa na huzuni tele.

Hizo zilikuwa siku za mwisho kuwa na mumewe, alimpenda mno na alikuwa kila kitu kwake, furaha yake, tumaini lake lakini katika kipindi hicho ugonjwa wa kisukari uliendelea kumtafuna kitandani pale.

Moyo wake uliumia lakini hakuwa na jinsi, walijitahidi kutafuta matibabu kila kona lakini walishindwa, pamoja na fedha zao zote hawakuweza kupata dawa kitu kilichowashangaza sana.

“Theo…” aliita mzee Edson.

“Ndiyo baba!”

“Nitakufa hivi karibuni,” alisema mzee huyo.

“Usiseme hivyo. Ninaumia baba.”
“Huo ndiyo ukweli! Siwezi kuishi zaidi. Nimetafuta dawa kila kona lakini imeshindikana, nitakufa, ila kabla ya kufa ni lazima uujue ukweli,” alisema Mzee Edson huku akimwangalia Theo aliyekuwa karibu yake kabisa.

“Kitu gani baba.”

“Sisi si wazazi wako,” alisema mzee huyo kwa sauti ndogo kabisa huku mkewe akiwa pembeni akilia tu.

“Unasemaje?” aliuliza Theo huku akionekana kushtuka.

Mzee Edson akarudia zaidi na zaidi. Theo hakuamini kile alichokisikia, aliuliza tena na tena na jibu lilikuwa lilelile kwamba hawakuwa wazazi wao. Alishangaa sana, mzee Edson akaanza kumuhadithia kila kitu kilichokuwa kimetokea, jinsi alivyopata ajali mpaka kupewa majibu kwamba asingeweza kupata mtoto.

Hilo lilimuuma sana Theo, kila kitu alichokuwa akikisikia kilikuwa kigeni masikiooni mwake. Alimwambia kwamba vijana wake ndiyo waliokwenda Posta kwenda kumletea mtoto, hakujua walimtoa wapi ila waliwaletea hospitalini.

Moyo wake ulimuuma mno. Kwa miaka yote hiyo alijua kwamba watu hao ndiyo walikuwa wazazi wake. Hakuzungumza kitu zaidi ya kulia tu, akaenda pembeni, akakaa chini na kuanza kulia. Moyo wake ulimuuma mno kwani kwa miaka yote hiyo alijua kwamba hao walikuwa wazazi wake.

“How is this possible?” (inawezekanaje hii?) alijiuliza huku akionekana kushtuka.

Theo akachanganyikiwa, hakutaka kubaki nyumbani hapo, moyo wake uliumia mno, akatoka ndani na kueleka nje, Bi Rachel akaanza kumfuata huku akimuita, alihisi kwamba kijana wake alikuwa akienda kufanya kitu kibaya.

Alipofika katika eneo la kuegesha magari, akaingia ndani ya gari lake, akaliwasha na kuondoka mahali hapo huku akilia. Hakujua alikuwa akienda wapi, alichanganyikiwa, kile alichoambiwa kilionekana kuwa ukatili mkubwa, alitakiwa kufahamu kila kitu kilichokuwa kimetokea nyuma na si kipindi hicho.

Akapata wazo kwamba ilikuwa ni afadhali kwenda hotelini kupumzika. Huko, akabaki akilia tu, kila alipokumbuka maneno ya baba yake moyo wake ulimuuma kupita kawaida. Usiku mzima akabaki akilia tu, wale hawakuwa wazazi wake, je, wazazi wake walikuwa wapi? Akajiuliza na kukosa jibu kabisa.

Aliyakumbuka maneno ya mzee Edson aliyomwambia kwamba alichukuliwa kutoka Posta, hakutaka kupoteza muda, asubuhi ya siku iliyofuata, moja kwa moja akaelekea huko, katika kituo kikuu cha polisi, alitaka kujua kile kilichokuwa kimetokea.

Alipofika, akaelekea mpaka mapokezi ambapo huko akajitambulisha, kila polisi alimfahamu, alikuwa mtoto wa bilionea mkubwa Tanzania, walimuheshimu mzee huyo.

“Nimekuja kuuliza,” alisema Edson.

“Kuhusu nini?”
“Kuna tukio liliwahi kutokea kipindi fulani hapa Posta,” alisema Edson.

“Mwaka gani?” aliuliza polisi, akawaambia mwaka husika, ilikuwa zamani kidogo.

“Ndiyo!”

“Siku hiyo kulikuwa na tukio lilitokea hapa Posta, kuna mwanamke aliibiwa mtoto, hivi mliipata kesi ya hivyo?” aliuliza Theo.

“Subiri kwanza.”

Alichokifanya polisi huyo ni kwenda katika chumba kilichojaza mafaili mengi, akapekua mafaili hayo na kutoa faili moja kuukuu, lililokuwa na vumbi jingi kisha kwenda nalo pale mapokezi.

Alipofika hapo, akalifungua. Alitaka kuangalia kile alichoambiwa na Theo kama taarifa ile iliwahi kufika kituoni hapo. Akaangalia siku husika, akaiona taarifa hiyo kwamba kulikuwa na mtoto aliibwa kutoka Posta Mpya, mtoto wa mwanamke kichaa aliyejulikana kwa jina la Miriam Mwendawazimu.

“Ni kweli tukio hilo lilitokea,” alisema polisi huyo.

“Kuna mwanamke aliibiwa mtoto!”
“Mwanamke gani? Anaitwa nani? Huyo mtoto aliitwa nani?” aliuliza Theo maswali matatu mfululizo.
“Aliitwa Jackson! Mwanamke huyo alikuwa mwendawazimu!”
“Mwendawazimu?”
“Ndiyo!” alijibu polisi yule, Theo akashusha pumzi na kuinama chini, alipoyainua macho yake, machozi yalikuwa yakimtiririka mashavuni mwake.

Hakutaka kuendelea kubaki kituoni hapo, alichokifanya ni kuondoka na kuelekea huko Posta. Alitaka kujua ukweli asubuhi hiyohiyo juu ya huyo mwanamke ambaye aliamini kwamba alikuwa mama yake.
Alipofika huko, kila mtu aliyemwangalia alionekana kuwa mgeni machoni mwake, hakujua ni mahali gani alitakiwa kuuliza. Alibaki mahali hapo akiwa amesimama pembeni ya gari yake, kwenye kuangaliaangalia, macho yake yakatua kwa mzee fulani aliyekuwa fundi viatu mahali hapo, akahisi kwamba inawezekana mzee huyo alikuwa akifahamu kitu kwani kutokana na umri wake, alionekana kuwa hapo kipindi kirefu.

“Samahani mzee wangu! Huu ni mwaka wa ngapi upo hapa?” aliuliza Theo mara baada ya kusalimiana na huyo mzee na kupiga stori kadhaa.

“Ni miaka mingi sana. Kama thelathini nipo hapa,” alijibu mzee huyo.

“Sawa. Hivi kulikuwa na mwanamke Mwendawazimu hapa zamani, enzi hizo ukiwa kijana?” aliuliza Theo.

“Zamani sana. Namkumbuka alikuwa mwendawazimu mmoja hapa aliitwa Miriam, alikuwa mzuri sana. Baada ya huyo hakukuwa na mwendawazimu yeyote yule,” alijibu mzee huyo, aliposema mzuri, hasa uso wake ulionyesha jinsi alivyofurahi kulitaja neno hilo.

“Alikwenda wapi?”
“Mmh! Sijui kwa kweli. Ila kuna watu walisema kuna mwanaume alimchukua na kumpeleka hospitali,” alijibu.

“Alikuwa akiumwa?”
“Ni stori ndefu sana. Yule mwendawazimu kuna kipindi alipewa mimba na mtu asiyejulikana, mtoto wake akaibwa, stori zilizagaa sana hapa. Baada ya miezi kadhaa, akabeba tena mimba, tukashangaa sana. Wakati tukiwa tunasubiri ajifungue, akachukuliwa na kupelekwa hospitali!” alijibu mzee huyo.

“Hospitali gani?”
“Wala sijui, hakukuwa na mtu anayejua chochote kile,” alisema mzee huyo.

“Kwa hiyo yupo hai au alikufa?”
“Sijui kwa kweli kwani ni kipindi kirefu sana, tangu siku hiyo, sikumuona tena!” alijibu.
“Sawa mzee!” alijibu Theo kisha kuondoka mahali hapo. Kichwa chake kilichanganyikiwa, ugumu uliokuwepo ni mahali ambapo angeweza kumpata mwanamke huyo, alipelekwa hospitali, hospitali gani? Hakujua.

“Kumbe alipata mimba nyingine? Bila shaka alijifungua, mtoto yupo wapi? Alikufa au? Kama yupo hai, yupo wapi kwa sasa? Mungu, nataka kumuona mama yangu, ninataka kumuona na ndugu yangu pia,” alisema Theo huku akiliegesha gari pembeni na kuanza kuulia kama mtoto.

 

Je, nini kitaendelea?
Tukutane Jumatatu

Comments are closed.