The House of Favourite Newspapers

Insane (Mwendawazimu)-14

Theo akaelekea nyumbani kwao huku akiwa na furaha tele, kile alichokuwa amekipanga kwa muda mrefu hatimaye alifanikiwa na muda huo ulikuwa wa kujipongeza kwa kazi kubwa aliyokuwa ameifanya.

Alipofika nyumbani, akaelekea katika chumba cha kupumzikia alipokuwa baba yake kwa lengo la kumjulia hali. Alipofika huko, macho yake yakatua kwa watu wawili, Esther na mwanaume ambaye hakuwa akimfahamu.

Hakuwasalimia zaidi ya kumsogelea baba yake na kumjulia hali. Alimchukia Esther, alimuacha na kuwa na mwanaume ambaye alikuwa na uhakika kwamba kipindi hicho alikuwa marehemu. Hakumwangalia usoni, akajifanya kama hakumuona.

Akasomewa mashitaka juu ya kile kilichokuwa kimeletwa. Kwanza hakujibu, akatulia kwa muda na kisha kumwangalia Esther. Alichukia, ni kweli alifanya hivyo lakini hakutaka kujionyesha.

“Nimteke Fabian, ili iweje?” aliuliza Theo huku akionekana kuwa na hasira.

“Nisikilize kijana. Hatujaja hapa kukutuhumu bali tuna uhakika kwamba umehusika kwa asilimia mia moja, ninakwambia hivi, ninamtaka kijana wangu vinginevyo nitakufanyia kitu kibaya sana,” alisema Mzee Boniface huku akionekana kukasirika.

“Utanifanya nini wewe mzee?” aliuliza Theo kwa kiburi, tena huku akitunisha kifua chake mbele kama bata.

Wakaanza kugombana kwa maneno, Theo hakutaka kukubali, alimtukana sana mzee Boniface kwani alijua fika kwamba mzee huyo asingeweza kumfanya kitu chochote kile, tena nyumbani kwao.

Mzee huyo alilalamika sana, moyo wake ulimwambia kwamba alikuwa na uhakika kwamba Theo ndiye ambaye alihusika kumteka Fabian kwa kile kilichokuwa kimetokea nyuma.

Alitamani kumpiga, moyo wake ulikuwa na hasira tele na muda wote alikunja sura. Theo hakuogopa, bado alijiona kuwa mbabe mpaka watu hao walipoondoka nyumbani hapo huku wakimpa siku mbili tu, vinginevyo wangemuua.

Theo hakuogopa, alibaki nyumbani hapo huku akimuuguza baba yake aliyeonekana kuwa na hali mbaya, mama yake, Bi Rachel  alikuwa pembeni, muda wote alionekana kuwa na huzuni tele.

Hizo zilikuwa siku za mwisho kuwa na mumewe, alimpenda mno na alikuwa kila kitu kwake, furaha yake, tumaini lake lakini katika kipindi hicho ugonjwa wa kisukari uliendelea kumtafuna kitandani pale.

Moyo wake uliumia lakini hakuwa na jinsi, walijitahidi kutafuta matibabu kila kona lakini walishindwa, pamoja na fedha zao zote hawakuweza kupata dawa kitu kilichowashangaza sana.

“Theo…” aliita mzee Edson.

“Ndiyo baba!”

“Nitakufa hivi karibuni,” alisema mzee huyo.

“Usiseme hivyo. Ninaumia baba.”
“Huo ndiyo ukweli! Siwezi kuishi zaidi. Nimetafuta dawa kila kona lakini imeshindikana, nitakufa, ila kabla ya kufa ni lazima uujue ukweli,” alisema Mzee Edson huku akimwangalia Theo aliyekuwa karibu yake kabisa.

“Kitu gani baba.”

“Sisi si wazazi wako,” alisema mzee huyo kwa sauti ndogo kabisa huku mkewe akiwa pembeni akilia tu.

“Unasemaje?” aliuliza Theo huku akionekana kushtuka.

Mzee Edson akarudia zaidi na zaidi. Theo hakuamini kile alichokisikia, aliuliza tena na tena na jibu lilikuwa lilelile kwamba hawakuwa wazazi wao. Alishangaa sana, mzee Edson akaanza kumuhadithia kila kitu kilichokuwa kimetokea, jinsi alivyopata ajali mpaka kupewa majibu kwamba asingeweza kupata mtoto.

Hilo lilimuuma sana Theo, kila kitu alichokuwa akikisikia kilikuwa kigeni masikiooni mwake. Alimwambia kwamba vijana wake ndiyo waliokwenda Posta kwenda kumletea mtoto, hakujua walimtoa wapi ila waliwaletea hospitalini.

Moyo wake ulimuuma mno. Kwa miaka yote hiyo alijua kwamba watu hao ndiyo walikuwa wazazi wake. Hakuzungumza kitu zaidi ya kulia tu, akaenda pembeni, akakaa chini na kuanza kulia. Moyo wake ulimuuma mno kwani kwa miaka yote hiyo alijua kwamba hao walikuwa wazazi wake.

“How is this possible?” (inawezekanaje hii?) alijiuliza huku akionekana kushtuka.

Theo akachanganyikiwa, hakutaka kubaki nyumbani hapo, moyo wake uliumia mno, akatoka ndani na kueleka nje, Bi Rachel akaanza kumfuata huku akimuita, alihisi kwamba kijana wake alikuwa akienda kufanya kitu kibaya.

Alipofika katika eneo la kuegesha magari, akaingia ndani ya gari lake, akaliwasha na kuondoka mahali hapo huku akilia. Hakujua alikuwa akienda wapi, alichanganyikiwa, kile alichoambiwa kilionekana kuwa ukatili mkubwa, alitakiwa kufahamu kila kitu kilichokuwa kimetokea nyuma na si kipindi hicho.

Akapata wazo kwamba ilikuwa ni afadhali kwenda hotelini kupumzika. Huko, akabaki akilia tu, kila alipokumbuka maneno ya baba yake moyo wake ulimuuma kupita kawaida. Usiku mzima akabaki akilia tu, wale hawakuwa wazazi wake, je, wazazi wake walikuwa wapi? Akajiuliza na kukosa jibu kabisa.

Aliyakumbuka maneno ya mzee Edson aliyomwambia kwamba alichukuliwa kutoka Posta, hakutaka kupoteza muda, asubuhi ya siku iliyofuata, moja kwa moja akaelekea huko, katika kituo kikuu cha polisi, alitaka kujua kile kilichokuwa kimetokea.

Alipofika, akaelekea mpaka mapokezi ambapo huko akajitambulisha, kila polisi alimfahamu, alikuwa mtoto wa bilionea mkubwa Tanzania, walimuheshimu mzee huyo.

“Nimekuja kuuliza,” alisema Edson.

“Kuhusu nini?”
“Kuna tukio liliwahi kutokea kipindi fulani hapa Posta,” alisema Edson.

“Mwaka gani?” aliuliza polisi, akawaambia mwaka husika, ilikuwa zamani kidogo.

“Ndiyo!”

“Siku hiyo kulikuwa na tukio lilitokea hapa Posta, kuna mwanamke aliibiwa mtoto, hivi mliipata kesi ya hivyo?” aliuliza Theo.

“Subiri kwanza.”

Alichokifanya polisi huyo ni kwenda katika chumba kilichojaza mafaili mengi, akapekua mafaili hayo na kutoa faili moja kuukuu, lililokuwa na vumbi jingi kisha kwenda nalo pale mapokezi.

Alipofika hapo, akalifungua. Alitaka kuangalia kile alichoambiwa na Theo kama taarifa ile iliwahi kufika kituoni hapo. Akaangalia siku husika, akaiona taarifa hiyo kwamba kulikuwa na mtoto aliibwa kutoka Posta Mpya, mtoto wa mwanamke kichaa aliyejulikana kwa jina la Miriam Mwendawazimu.

“Ni kweli tukio hilo lilitokea,” alisema polisi huyo.

“Kuna mwanamke aliibiwa mtoto!”
“Mwanamke gani? Anaitwa nani? Huyo mtoto aliitwa nani?” aliuliza Theo maswali matatu mfululizo.
“Aliitwa Jackson! Mwanamke huyo alikuwa mwendawazimu!”
“Mwendawazimu?”
“Ndiyo!” alijibu polisi yule, Theo akashusha pumzi na kuinama chini, alipoyainua macho yake, machozi yalikuwa yakimtiririka mashavuni mwake.

Hakutaka kuendelea kubaki kituoni hapo, alichokifanya ni kuondoka na kuelekea huko Posta. Alitaka kujua ukweli asubuhi hiyohiyo juu ya huyo mwanamke ambaye aliamini kwamba alikuwa mama yake.
Alipofika huko, kila mtu aliyemwangalia alionekana kuwa mgeni machoni mwake, hakujua ni mahali gani alitakiwa kuuliza. Alibaki mahali hapo akiwa amesimama pembeni ya gari yake, kwenye kuangaliaangalia, macho yake yakatua kwa mzee fulani aliyekuwa fundi viatu mahali hapo, akahisi kwamba inawezekana mzee huyo alikuwa akifahamu kitu kwani kutokana na umri wake, alionekana kuwa hapo kipindi kirefu.

“Samahani mzee wangu! Huu ni mwaka wa ngapi upo hapa?” aliuliza Theo mara baada ya kusalimiana na huyo mzee na kupiga stori kadhaa.

“Ni miaka mingi sana. Kama thelathini nipo hapa,” alijibu mzee huyo.

“Sawa. Hivi kulikuwa na mwanamke Mwendawazimu hapa zamani, enzi hizo ukiwa kijana?” aliuliza Theo.

“Zamani sana. Namkumbuka alikuwa mwendawazimu mmoja hapa aliitwa Miriam, alikuwa mzuri sana. Baada ya huyo hakukuwa na mwendawazimu yeyote yule,” alijibu mzee huyo, aliposema mzuri, hasa uso wake ulionyesha jinsi alivyofurahi kulitaja neno hilo.

“Alikwenda wapi?”
“Mmh! Sijui kwa kweli. Ila kuna watu walisema kuna mwanaume alimchukua na kumpeleka hospitali,” alijibu.

“Alikuwa akiumwa?”
“Ni stori ndefu sana. Yule mwendawazimu kuna kipindi alipewa mimba na mtu asiyejulikana, mtoto wake akaibwa, stori zilizagaa sana hapa. Baada ya miezi kadhaa, akabeba tena mimba, tukashangaa sana. Wakati tukiwa tunasubiri ajifungue, akachukuliwa na kupelekwa hospitali!” alijibu mzee huyo.

“Hospitali gani?”
“Wala sijui, hakukuwa na mtu anayejua chochote kile,” alisema mzee huyo.

“Kwa hiyo yupo hai au alikufa?”
“Sijui kwa kweli kwani ni kipindi kirefu sana, tangu siku hiyo, sikumuona tena!” alijibu.
“Sawa mzee!” alijibu Theo kisha kuondoka mahali hapo. Kichwa chake kilichanganyikiwa, ugumu uliokuwepo ni mahali ambapo angeweza kumpata mwanamke huyo, alipelekwa hospitali, hospitali gani? Hakujua.

“Kumbe alipata mimba nyingine? Bila shaka alijifungua, mtoto yupo wapi? Alikufa au? Kama yupo hai, yupo wapi kwa sasa? Mungu, nataka kumuona mama yangu, ninataka kumuona na ndugu yangu pia,” alisema Theo huku akiliegesha gari pembeni na kuanza kuulia kama mtoto.

****

Theo alichanganyikiwa, hakutaka kurudi nyumbani, alishinda hotelini kwa siku mbili mfululizo, moyo wake ulikuwa na hamu ya kumuona mama yake, hakutaka kuona akirudi nyumbani na wakati hakujua mama yake alikuwa wapi, hata kama alikuwa amekufa, ilikuwa ni lazima alione hata kaburi lake aridhike.

Mzee Edson na mkewe, Bi Rachel walichanganyikiwa, hawakujua mahali alipokuwa kijana wao, walijaribu kutoa taarifa polisi na kuwaambia wamtafute lakini ndani ya siku mbili hawakuweza kugundua chochote kile.

Ugonjwa wa kisukari aliokuwa akiumwa mzee Edson ukaongezeka, mkewe alimuonea huruma na aliona kwamba mumewe angeweza kufa kitandani hapo. Ilimtia hofu moyoni mwake, hivyo kilichofanyika ni kuwaambia polisi waendelee kumtafuta kwani Theo alikuwa muhimu kuliko kitu chochote kile.

Baada ya siku tatu, Theo akarudi nyumbani, kama alivyoondoka ndivyo alivyorudi, alionekana kuwa na mawazo tele, wazazi hao walipomuuliza, aliwaambia kuhusu mama yake kwamba alikuwa kichaa aliyekuwa Posta jijini Dar es Salaam na jina lake aliitwa Miriam Mwendawazimu.

“Nitakusaidia kumtafuta Miriam,” alisema mzee Edson.

Alichokifanya ni kuwasiliana na waandishi wa habari na kuwaambia kile kilichokuwa kimetokea hivyo walitakiwa kutoa tangazo kwenye magazeti kuhusu mwendawazimu ambaye alivuma sana miaka ya nyuma huko Posta Mpya na yeyote ambaye angefanikisha kujua alipo basi kulikuwa na zawadi nono.

Tangazo hilo lilitolewa katika magazeti mbalimbali, watu wengi hawakumfahamu ila kwa wachache ambao walimkumbuka, walikumbuka baadhi ya matukio lakini baada ya siku chache alitoweka hapo Posta, alipoelekea, hakukuwa na aliyepafahamu.

Hilo likawa gumzo na mmoja wa watu walioona tangazo hilo alikuwa Mzee Boniface, hakujua ni kitu gani kilikuwa kimetokea mpaka mwanamke wake kutafutwa namna hiyo. Akawa na hofu, akahisi kwamba kulikuwa na mtu mbaya ambaye alikuwa akitaka kumuona mwanamke huyo amdhuru hivyo alihakikisha anakuwa naye karibu kwa kwenda kumtembelea Dodoma mara kwa mara.

Wakati tangazo likiwa limetolewa kwa muda wa wiki moja kabla ya kupata chochote kile, ndipo likamfikia Dk. Fabian ambaye jina lake lilipewa mtoto aliyekuwa amejifungua Miriam Mwendawazimu kipindi hicho.

Alipoliona, akamkumbuka mwanamke huyo, yeye ndiye aliyempeleka leba na kujifungua na hivyo kumshauri Boniface ampeleke mwanamke huyo katika hospitali ya vichaa iliyokuwa Dodoma.

“Hallo!” aliita kwenye simu.

“Hallo!” sauti ya mwanaume mmoja ikasikika.

“Samahani! Namba hii nimeikuta kwenye gazeti. Naitwa Dk. Fabian,” alisema daktari huyo huku simu ikiwa sikioni mwake.

“Ndiyo!”

“Ninataka kujua ni kiasi gani mtatoa kwa mtu atakayefanikisha kupatikana kwa huyo mwanamke mnayemuulizia,” alisema Dk. Fabian.

“Unajua alipo?”
“Kwanza hujajibu swali langu.”
“Imeandaliwa milioni tano!”
“Haitoshi, Kama mna ishirini, semeni niwaambieni alipo,” alisema daktari huyo.

Kwanza simu ikakatwa, baada ya muda akapigiwa tena na sauti nzito ya mwanaume ikawa inasikika kwenye simu, wakazungumza kidogo na kuambiwa aelekee katika jumba la kifahari la Bwana Edson ambaye kipindi hicho alikuwa hoi.

Hakujua nii kitu gani kilikuwa kikiendelea, alichokifanya ni kwenda huko, alipofika, akakaribishwa na kuingia ndani. Alimuona mzee huyo akiteseka kitandani, moyo wake ulimuuma mno kwani pamoja na mzee huyo kuwa na kiasi kikubwa cha fedha lakini bado hazikuweza kumrudisha kwenye hali ya kawaida.

“Umesema unajua mahali mwanamke huyu alipo?” aliuliza mzee Edson huku Theo akiwa pembeni, moyo wake ulikuwa na hamu ya kufahamu mahali mama yake alipokuwa.

“Ndiyo! Mimi ndiye niliyemzalisha watoto wake. Wa kwanza aliitwa Jackson ambaye aliibwa na wa pili aliitwa Fabian. Ninamjua baba wa watoto hawa, ni mwanaume anayeitwa Boniface, alikuwa akiishi na mtoto wake anayeitwa Fabian, sijui kwa sasa wapo wapi, ila mwanamke huyo alichukuliwa na kupelekwa katika Hospitali ya Mirembe mkoani Dodoma,” alisema Dk. Fabian.

“Sawa. Nashukuru sana. Ni lazima twende huko!”

“Hapana baba! Hali yako si nzuri, acha niende na mama!”

“Hapana! Ninataka kumuona mwanamke huyo. Kama yupo hai, basi nimuombe msamaha kwa kile kilichotokea, hata kama ni mwendawazimu, naamini atanielewa,” alisema mzee Edson.

Hawakuwa na jinsi, siku iliyofuata wakaanza safari ya kuelekea mkoani Dodoma Muda wote Theo alikuwa na furaha, hakuwahi kumuona mama yake, wale aliokuwa akikaa nao kila siku alihisi kwamba walikuwa wazazi wake kumbe ukweli wenyewe hawakuwa wazazi wake.

Walipofika huko, tena huku wakiongozana na Dk. Fabian, wakaelekea mpaka katika ofisi ya daktari na kuambiwa wamsubiri. Macho ya Theo hayakutulia, yalikuwa yakiangalia huku na kule yakimtafuta mwanamke aliyehisi kwamba alikuwa humo, alitaka kuona kama alifanana naye au la.

Daktari alikuwa na mgeni hivyo walitakiwa kusubiri kwa nje pia. Baada ya dakika ishirini, mlango ukafunguliwa, mwanaume aliyetoka, walimfahamu vilivyo, alikuwa mzee Biniface.

Kitendo cha Theo kumuona mwanaume huyo, akahisi hasira ikimkaba kooni, aliumia kumuona mahali hapo kwani ndiye yuleyule ambaye Esther alikwenda naye nyumbani kwao na kumtuhumu kwa kumteka Fabian.

“We mwanaume mbona unatufuatilia sana?” aliuliza Theo, tayari alisimama, hakumpenda mzee Boniface, alimchukia kwa sababu tu alikwenda kumuharibia nyumbani kwao.

Mzee Boniface ambaye machozi yake yalikuwa mekundu hali iliyoonyesha kwamba alilia sana dakika zilizopita, hakuzungumza kitu, alisimama tu akimwangalia Theo, ila alipopiga macho pembeni, yakakutana na mwanaume ambaye alihisi kwamba alikwishawahi kumuona sehemu fulani.

“Dk. Fabian!” aliita huku akiachia tabasamu pana.

“Boniface. Upo hai! Nimefurahi kukuona,” alisema Dk. Fabian huku akisimama, wote wakakumbatiana.

“Mbona upo hivyo?” aliuliza Dk. Fabian.

“Mtoto wangu alitekwa na kuna taarifa zinasema kwamba aliuawa msituni na watu, hatukuweza kuupata mwili wake. Moyo wangu unaniuma, mtoto wangu wa kwanza, Jackson aliibwa na watu wasiojulikana kule Posta, leo hii, watu wenye hasira wanamuua mtoto wangu…kweli wanamuua mtoto wangu, hawajui ni jinsi gani nilihangaika kumpata? Au kwa sababu nilizaa na mpenzi wangu, Miriam?” aliuliza mzee Boniface huku akilia kama mtoto, kila kitu alichokiongea kilimuumiza moyo wake.

Kila mmoja aliyekuwa mahali hapo alibaki akishangaa, Theo akatoa macho yake, hakuamini alichokuwa amekisikia, alikumbuka kwamba aliambiwa kuwa mtoto wa kwanza wa mama yake aliitwa Jackson, na ndiye alikuwa yeye huku wa pili akiitwa Fabian.

Hakuamini kile alichokisikia kutoka kwa mzee Boniface kwamba alikuwa akiwazungumzia watoto wale wale ambao mmoja wapo alikuwa yeye, na wa pili aliitwa Fabian, yule ambaye alituma watu wamteke na kumuua, hapo ndipo alipogundua kwamba inawezekana huyo Fabian alikuwa ndugu yake.

“Unasemaje?” aliuliza Theo huku akisimama, alikuwa akimwangalia mzee Boniface aliyekuwa akilia.

“Kijana! Naomba uniache! Moyo wangu unaniuma sana, naweza nikachukua maamuzi magumu! Nimechanganyikiwa, naomba uniache,” alisema mzee Boniface huku akipiga hatua kuelekea nje, Bi Rachel akamuomba arudi.

“Naomba tuzungumze nawe.”
“Kuhusu nini mama? Mmekuwa mnanifuatilia sana, mtoto wenu kamteka mtoto wangu na kumuua, bado mnataka niwe rafiki yenu?” aliuliza mzee Boniface huku akiendelea kulia.

“Hapana! Naomba utusikilize kwanza.”
“Hapana! Siwezi!”
Aliamua kutokuwasikiliza kabisa, akafungua mlango na kuondoka zake. Theo hakutaka kubaki hapo, si yeye tu, hata watu wengine wakatoka na kuanza kumkimbilia, Mzee Boniface alikuwa mtu muhimu mno.

“Baba..baba..” aliita Theo huku naye akianza kulia.

Mzee Boniface hakuamini, akasimama na kuangalia nyuma, alimuona Theo akija na kumkumbatia, hakuelewa ni kitu gani kilikuwa kimetokea, hakujua sababu iliyomfanya Theo amkimbilie na kumkumbatia na wakati alikuwa adui yake.

“Boniface naomba unisikilize…” alisema Dk. Fabian na kuendelea:
“Unamkumbuka mtoto wako aliyeibia?” aliuliza daktari huyo.

“Ndiyo! Unamzungumzia Jackson?”

“Ndiyo! Ndiye huyo hapo aliyekukumbatia!”

“Huyu mwanaharamu? Hapana! Jackson wangu hawezi kuwa huyu. Amemuua mtoto wangu huyu!” alisema mzee huyo huku akilia.

Hiyo ndiyo ilikuwa nafasi ya kufahamu kila kitu, alichokifanya Bi Rachel ni kumuhadithia kila kitu kilichotokea miaka ya nyuma tangu walipokosa mtoto na kuamua kuwatuma vijana kwenda kuiba mtoto.

Kila kitu alichokisikia, Mzee Boniface hakuamini, historia ilikuwa ileile kwamba walikwenda watu wenye pikipiki na kumuiba mtoto wake. Akamsogelea Theo na kumwangalia vizuri, aliona jinsi kijana huyo alivyokuwa na macho ya mama yake, masikio na pua yake, akamkumbatia.

Mtu aliyemchukia, ndiye mtu aliyempa furaha kipindi hicho. Alilia sana, hatimaye baada ya kupita miaka zaidi ya ishirini, alifanikiwa kuonana na mtoto wake ambaye kila siku alitamani sana kumuona.

****

Walibaki wakiwa wamekumbatiana kwa furaha tele, kila mmoja alikuwa akilia, hakuamini kama mwisho wa siku wangeweza kukutana tena. Walikuwa maadui, walikorofishana lakini ndani ya dakika chache wakasahau kila kitu, wakaungana na kuwa kitu kimoja.

“Baba! Siamini kama nimekutana na wewe!” alisema Theo huku akilia.

“Nyamaza mtoto wangu! Mungu alipanga siku moja tukutane,” alisema Mzee Boniface.

“Naomba unisamehe kwa kila kitu kilichotokea,” alisema Theo huku akiendelea kulia kama mtoto.

Walikumbatiana kwa dakika kadhaa ndipo wakaondoka na kurudi kwa daktari, Mzee Boniface akamwambia kila kitu kilichotokea, yeye mwenyewe hakuamini kama jambo hilo lingeweza kuwezekana namna hiyo.

Kwa sababu Theo alikuwa na kiu kubwa ya kumuona mama yake, wakamchukua na kumpeleka huko, alisimama kwa mbali huku akionyeshewa mwanamke mtu mzima, mwendawazimu aliyekuwa chini huku akiongea peke yake.

Ilimuuma, hakuamini kama yule aliyekuwa akimwangalia alikuwa mama yake, hakutaka kusimama pale alipokuwa, akaondoka na kumfuata mama yake, machozi yalikuwa yakimtoka, hayakuwa machozi ya uchungu, yalikuwa ni ya furaha mno kwani hakukuwa na kitu alichokuwa akitamani kipindi hicho kama kumuona mwanamke huyo.

“Mama! Siamini kama nimekuona,” alisema Theo huku akimwangalia Mariam Mwendawazimu katika hali iliyoonyesha ni jinsi gani alikuwa na furaha moyoni mwake.

Siku hiyo hakutaka kuondoka mapema, alibaki hospitali hiyo ya vichaa akimwangalia mama yake tu. Moyoni mwake alikuwa na faraja kubwa, alifurahi mno na muda mwingi uso wake ulikuwa kwenye tabasamu pana.

Mama yake alikuwa mwendawazimu lakini alishukuru kumuona kwani alijua kulikuwa na watu wengi waliotaka kuwaona wazazi wao tu lakini hawakuweza, kwake, hiyo ilionekana kuwa bahati kubwa.

Kichwa chake kilimuuma kila alipomkumbuka Fabian, yeye ndiye aliyekuwa amewaamburu watekaji wamuue mara baada ya kumteka na mbaya zaidi walimpigia simu na kumwambia kwamba tayari kazi ilifanyika kwa mafanikio makubwa.

Alilia na kuhuzunika sana, akaanza kumuomba msamaha baba yake kwa kile kilichokuwa kimetokea, hakujua chochote kile, hakujua kama huyo Fabian ambaye kila siku alimuona kuwa adui yake alikuwa ndugu yake, tena wa damu kabisa.

Siku hiyo wakarudi, hakutaka kurudi nyumbani kwao, akaondoka na baba yake mpaka nyumbani, huko hawakutaka kukaa, wakaanza kufanya mipango ya kumtafuta Fabian, hata kama aliuawa, walitaka kuiona maiti yake.

Kitu cha kwanza ni kwenda katika Kituo cha Polisi cha Mbezi kwa Luis ili kuona kama kungekuwa na taarifa iliyomhusu mdogo wake, Fabian. Walipofika huko, polisi wakawaambia kwamba hawakuwa wamepewa taarifa ya mtu yeyote kuuawa huko msituni.

“Kweli?” aliuliza huku akionekana kutokuamini.

“Ndiyo! Kuna mtu ameuawa?” aliuliza polisi.

“Hapana! Kuna ndugu yetu tunamtafuta na hatujui yupo wapi,” alisema Mzee Boniface.

Alichokifanya Theo ni kuwasiliana na watu aliokuwa amewapa kazi ya kumuua Fabian, alitaka kuwauliza mahali ambapo walimuulia, alipoambiwa, hakutaka kusubiri, siku hiyohiyo, yeye na baba yake wakaelekea huko, wakataka kuona kama kweli wangeupata mwili wake au la.

Hawakuchukua muda mrefu wakawa wamekwishafika ndani ya msitu huo na kwenda katika sehemu walipokuwa wameelekezwa, walipofika, walichokutana nacho ni michirizi ya damu iliyokuwa imekauka na nyasi kulala upande mmoja.

Dalili zote zilionyesha kwamba Fabian alikuwa ameuawa mahali hapo. Walichanganyikiwa, muda wote Theo alikuwa akilia tu, moyo wake ulimuuma sana na hakuamini kama kweli kwa kutokujua kwake alikuwa amemuua ndugu yake.

Hawakutaka kuondoka, wakati mwingine walihisi kwamba kulikuwa na watu ambao walifika mahali hapo na kuuchukua mwili wa Fabian na kwenda kuuzika sehemu, kitu cha kwanza kabisa walichotaka kufahamu ni kama jirani na msitu huo kulikuwa na nyumba walizokuwa wakiishi watu.

Hilo halikuwa gumu, walizunguka huku na kule kutafuta kama wangeweza kuona mtaa wowote ule. Kwenye pitapita yao wakajikuta wakitokezea katika eneo lililokuwa na nyumba kadhaa, hawakujua ilikuwa sehemu gani lakini kwa jinsi walivyoangalia, ulikuwa ni mtaa unaokua kadiri siku zilivyokuwa zikisonga mbele.

“Samahani wewe mtot! Unaishi wapi?” aliuliza Theo, walimsimamisha mtoto mmoja kwa lengo la kumuuliza.

“Hapo mbele.”
“Baba yako yupo?”
“Hayupo. Yupo mama tu!” alijibu mtoto huyo.

“Unaweza kutupeleka kuongea naye?”
“Naogopa.”
“Unaogopa nini?”
“Baba alisema mtu yeyote asije nyumbani.”
“Kwa nini?”
“Sijui!”

Hilo halikuwazuia, kitu walichokifanya ni kuanza kuelekea katika nyumba hiyo, walitaka kufahamu kile kilichotokea kipindi ambacho Fabian alipelekwa ndani ya msitu huo, walitaka kujua kama alikuwa hai au aliuawa kama ambavyo agizo lilivyotolewa.

Wakaelekea huko, walipofika, wakagonga hodi na kuisikia sauti ya mwanamke ikiwakaribisha. Hawakuingia ndani, wakamsubiri mwanamke huyo, baada ya sekunde chache, mwanamke mmoja aliyevalia vitenge viwili vya juu na chini kutoka nje.

“Karibuni,” alisema mwanamke huyo.

“Asante!”

Wakaanza kumwambia mwanamke huyo kile kilichokuwa kimewaleta mahali hapo. Alibaki kimya huku akiwasikiliza kwa makini kabisa. Walimwambia wazi kwamba walikuwa wakimtafuta mwanaume mmoja ambaye siku kadhaa zilizopita aliletwa ndani ya msitu wa Pande na kufanyiwa unyama humo.

“Mmh! Kwa kweli sijui chochote kile,” alisema mwanamke huyo.

“Hapana! Unaonekana kabisa kujua. Tuambie ukweli, tumesafiri mbali sana kwa ajili yake, tuambie ukweli, hata kama alikufa na kuzikwa, tuonyeshe kaburi lake,” alisema Theo, macho yakaanza kuwa mekundu na baada ya sekunde chache zilizofuata, machozi yakaanza kutiririka mashavuni mwake, moyo wake ulijisikia uchungu mno.

****

Watekaji walimchukua Fabian na kuondoka naye, ndani ya gari, kila mmoja alikuwa akizungumza lake lakini kila Fabian alipotaka kuzungumza, walimwambia anyamaze tena kwa kumpiga.

Alikuwa akiumia, aliendelea kuomba msamaha lakini hawakumuaha, waliendelea kumpiga mpaka walipofika karibu na msitu wa Pande. Dereva akakata kona upande wa kushoto na kuingia ndani ya msitu huo.

Ulikuwa ukitisha, ilikuwa ni rahisi kwa mtu asiyekuwa na moyo wa kishujaa kurudi alipotoka. Walikuwa wakiendelea na safari huku wakipita sehemu zilizokuwa na nyasi nyingi, sauti za ndege ndizo zilizokuwa zikisikika sehemu hiyo, walikwenda mpaka walipoanza kuona miti mirefu na mikubwa, wakasimamisha gari na kuteremka.

Ilikuwa ni lazima wamuue Fabian kama walivyoambiwa, hawakutaka kumuacha hai kwani kati ya kazi zote walizokuwa wamefanya kwa miaka mingi, hakukuwa na kazi ambayo hawakufanikiwa, walifanikiwa katika kila kazi.

“Naomba mnisamehe…” alisema Fabian huku akiendelea kuomba msamaha.

“Hatuwezi. Huo msamaha utamuomba Theo na si sisi,” alisema mwanaume mmoja.

“Theo! Yaani amewatuma kuniua kisa mwanamke!” alisema Fabian huku akishangaa, hakuamini kuona kila kitu kilichokuwa kimefanyika kilipangwa na Theo, mwanaume aliyekuwa akichukiana naye tangu kitambo.

Walimlaza chini, kila mmoja alidhamiria kufanya unyama waliokuwa wameambiwa, kumuua huko porini na kisha kumtelekeza na wao kundoka kufanya mambo yao. Jamaa mmoja akachukua bastola yake iliyokuwa na risasi za kutosha ndani yake tayari kwa kumpiga risasi mahali hapo.

“Sali sala yako ya mwisho..” alisema jamaa huyo aliyekuwa kiongozi wao.

Japokuwa alikuwa na hofu tele lakini Fabian hakuwa na jinsi, akaanza kusali sala yake ya mwisho kwani hakuamini kama kweli angeweza kupona kutoka katika mikono ya watu hao ambao kwa kuwaangalia tu walionekana kuwa watu wabaya.

Alipomaliza, alichokuwa akikisubiri kilikuwa kifo tu. Jamaa yule akachukua bastola yake na kuanza kubonyeza kitufe cha bastola ile, kitu cha ajabu ambacho kilimshangaza kila mmoja, bastola haikuwa na kitu.

“Vipi?”
“Eti bastola haina kitu!”
“Unasemaje?”
“Si umesikia nilichokisema, hakuna kitu!”

Kila mmoja alishangaa, halikuwa jambo rahisi hata kidogo kuona bastola haikuwa na kitu, hawakuwahi kufanya uzembe kama huo. Kwa miaka yote waliyokuwa wamewahi kufanya kazi hiyo ilikuwa ni lazima wahakikishe kwamba risasi zipo kwenye bastola na kufanya mauaji yao ila kwa siku hiyo ilionekana kuwa tofauti kabisa.

Hawakutaka kumuacha, walichokifanya ni kuanza kumpiga hapohapo chini alipokuwa. Sharti lao lilikuwa ni kumuua, alipiga kelele za kuomba msamaha lakini hakukuwa na aliyemuonea huruma hata kidogo, walimshambulia, alivuja damu, uso ulivimba lakini hakukuwa na aliyemuacha.

Walichukua dakika ishirini kumshambulia, walipomaliza, wakahakikisha mapigo ya moyo yakidunda kwa mbali sana hali iliyoonyesha kwamba muda wowote ule angekufa, wakamchukua na kumburuza kwenye nyasi ndefu kisha kumtelekeza huko na wao kuondoka huku wakiamini kwamba ndani ya dakika chache mwanaume huyo angekuwa marehemu.

Fabian alikuwa kimya mahali hapo, hakukuwa na msaada wowote ule, macho yake yalikuwa mazito na aliamini kwamba huo ndiyo ungekuwa mwisho wake, pale alipokuwa, alikuwa hoi, mwili uliuma na alishindwa hata kusogeza kiungo chochote cha mwili wake na muda wote alikuwa akimuomba Mungu aichukue roho yake.

Usiku mzima akawa mahali hapo mpaka siku nyingine ilipoingia, alikuwa mahali hapo huku akiwa hajatingisha kiungo chochote cha mwili wake.

Asubuhi hiyo ndipo mwanaume mmoja aliyekuwa akiwinda porini humo akafanikiwa kumuona Fabian akiwa hoi porini hapo. KWanza akashangaa kwa kuwa haikuwa kawaida kumuona mtu yeyote katika sehemu kama porini hapo, alichokifanya ni kuweka mishale yake pembeni na kumfuata mwanaume huyo aliyekuwa akitokwa na damu na nyingine zikiwa zimekauka kabisa.

“Mungu wangu!” alijisemea huku akianza kumbeba.

Hakutaka kubaki naye mahali hapo, akamchukua na kuondoka naye mahali hapo huku akiwa begani mwake. Moyo wake ulikuwa na hofu kubwa, hakujua mwanaume huyo alikuwa nani na aliletwa na nani mahali hapo na kushambuliwa. Kutoka hapo porini mpaka nyumbani kwake hakukuwa mbali, akawa amefika na kumuita mkewe na kumwambia kile kilichokuwa kimetokea huko porini.

Wakaamua kumsaidia. Fabian hakujua alikuwa wapi, aliteseka kitandani, mwili wake ulikuwa na majeraha makubwa, mzee huyo na mkewe ndiyo waliokuwa wakimuhudumia mahali hapo huku kila mmoja akiwa hana uhakika kama angeweza kupona na kuwa mzima kama alivyokuwa.

Mzee huyo aliyeitwa kwa jina la Ezekiel, akawa na kazi ya kwenda katika duka la madawa na kununua dawa huko kwa ajili ya Fabian na alipokuwa akirudi nyumbani, kazi ilikuwa ni kumtibu mpaka kuhakikisha anakuwa sawa.

Hawakutaka kumwambia mtu yeyote juu ya kile kilichokuwa kimetokea, walitaka wafanye kazi yote wao na kama ikiwezekana, apone kukiwa hakuna mtu yeyote anayefahamu kama ndani ya nyumba hiyo kulikuwa na mtu mwingine, tena walimwambia mpaka mtoto wao kutokuzungumza chochote juu ya kilichokuwa kikiendelea ndani ya nyumba hiyo.

Siku ya kwanza ilipokatika, siku ya pili ilipoingia ndipo asubuhi na mapema mzee huyo akaondoka kufuatilia mafao yake ya Afrika Mashariki. Aliondoka huku akijua kwamba mkewe angemuhudumia Fabian kama kawaida.

Baada ya saa kadhaa, mkewe akapata ugeni wa watu wawili, walifika mahali hapo na kumuulizia Fabian, mwanaume ambaye alipigwa vibaya porini na kisha kutelekezwa. Aliwaficha kwamba hakuwa akimfahamu mwanaume huyo lakini baada ya kumwambia kwamba walikuwa watu wazuri, mwanamke huyo hakuwa na jinsi, akawakaribisha mpaka ndani.

Kitendo cha Theo kumuona mdogo wake, moyo wake ulimuuma mno, alibaki akilia kama mtoto mdogo, aliumia moyoni mwake kwani alijua yeye ndiye aliyesababisha Fabian kuwa katika hali hiyo aliyokuwa nayo.

“Huyu ni mtoto wangu,” alisema Bwana Boniface huku akimwangalia mwanamke yule.

“Kumbe ni mtoto wako, ilikuwaje mpaka kuwa pale porini?” aliuliza mwanamke huyo.

“Alitekwa!”
“Na kina nani?”
“Hakuna anayejua!”
“Sasa ilikuwaje mkajua kwamba alipelekwa katika msitu huu?” aliuliza mwanamke huyo.

“Ni habari ndefu sana.”
“Na huyu ni nani?”
“Kaka yake anaitwa Theo.”
“Poleni sana.”
Watu hao wakakaa nyumbani hapo, kila walipomwangalia Fabian kitandani pale alionekana kuzidiwa na hakukuwa na matumaini kama kweli angeweza kupona. Walitamani kuondoka naye ili kumpleka hospitali lakini kila walipomwambia mwanamke huyo kuhusu jambo hilo, alikataa, akawaambia kwamba ingekuwa vizuri sana kama wangemsubiri mumewe.

Saa sita mchana, mzee Ezekiel akarudi nyumbani hapo akiwa na mfuko wa dawa. Alipoingia ndani, alishangaa kuuona ugeni huo, alimwambia mkewe kwamba hakutakiwa kuingia mtu yeyote ndani ya nyumba hiyo lakini kitu cha ajabu kabisa, aliwakuta watu hao ndani.

Akaanza kuwatambulisha kwamba walikuwa ndugu wa kijana yule. Hakukataa kwani kila alipomwangalia Bwana Boniface, alifanana na Fabian hivyo kuanza kuzungumza na kuangalia kitu gani walitakiwa kufanya kuyaokoa maisha ya kijana huyo kitandani hapo.

“Nataka nimpeleke hospitali,” alisema Bwana Boniface huku machozi yakianza kumlenga.

“Hakuna tatizo, lakini iwe chini ya uangalizi wangu!”
“Sawa.”

Wakakubaliana na kilichofuata baada ya hapo ni kuanza kumpeleka Fabian hospitali. Alikuwa hoi na hakuwa akijitambua, hakuwa amepata nafuu, mwili wake ulivimba sana na kila mtu aliyemwangalia alihisi kwamba tayari mwanaumee huyo alikuwa amefariki dunia kwa jinsi alivyokuwa.

Wakaingia ndani ya gari na kuanza kuelekea katika Hospitali ya Mtumishi iliyokuwa hapo Mbezi kwa Luis, walipofika huko, wakapokewa mgonjwa wao na moja kwa moja kumuingiza ndani ya chumba cha upasuaji.

“Jamani! Ni ajali au?” aliuliza nesi mmoja, kwa jinsi Fabian alivyokuwa, alikuwa na uhakika kwamba alipata ajali mbaya ya gari.

“Si ajali!”
“Kumbe nini?”
“Wewe mtibu kwanza. Maswali mengine utauliza baadaye,” alisema Bwana Boniface kwa sauti yenye ukali kidogo iliyomfanya nesi huyo na wenzake kumuita daktari harakaharaka ili aende kumtibu Fabian.

****

Kila mmoja alikuwa na mawazo, walikaa kwenye benchi huku wakilifikiria kile kilichokuwa kimetokea, kwa Theo, alikuwa na huzuni tele, hakuamini kama ujinga wote aliokuwa ameufanya kwa mtu asiyekuwa akimpenda, kumbe alikuwa ndugu yake wa damu.

Machozi hayakumuisha, yalikuwa yakimtoka tu, alihisi maumivu makali moyoni mwake na muda wote alisikia sauti ikimuhukumu kwamba alifanya jambo baya ambalo halikutakiwa kufanywa na mtu kama yeye, tena kwa ndugu wake wa damu.

Madaktari walikuwa ndani wakiendelea kumuhudumia Fabian, alikuwa kwenye hali mbaya sana, alipoteza kiasi kikubwa cha damu na muda wote mwili wake ulikuwa umevimba.

Madaktari wakawa na kazi ya kuingia na kutoka ndani ya chumba hicho, waliendelea kumtibu kijana huyo aliyekuwa kwenye hali mbaya mno, hawakuwa na matumaini kama kweli angepona au la.

“Dokta tuambie ukweli,” alisema Bwana Boniface huku akimwangalia daktari, alikwishasimama, alitaka kusikia chochote kutoka kwa daktari huyo.

“Ukweli gani?”

“Kuhusu mtoto wangu!”
“Subiri kwanza. Bado tunaendelea kumpatia matibabu!”
“Atapona lakini?”
“Hilo tuachie sisi,” alisema daktari huyo na kuondoka.

Walikaa hospitalini hapo lakini hawakuambiwa kitu chochote kile kuhusu Fabian, mioyo yao ilikuwa na hofu tele kwa kudhani kwamba madaktari walijua kuwa Fabian alikufa ila hawakutaka kuwaambia ukwelio.

Bwana Boniface akampigia simu Esther na kumtaka kufika hospitalini hapo haraka iwezekanavyo. Ndani ya dakika arobaini msichana huyo alikuwa hospitalini hapo. Kitendo cha kuingia ndani na kumuona Theo, uso wake ukawa kwenye hasira mno, hakutegemea kumuona Bwana Boniface akiwa na mwanaume huyo aliyekuwa akimchukia mno.

Harakaharaka Theo akasimama na kuanza kumsogelea msichana huyo, alipomfikia, Esther akasonya na kisha kuelekea kwenye benchi na kuanza kuzungumza na Bwana Boniface ambaye akaamua kumwambia Esther kila kitu kilichokuwa kimetokea.

“Haiwezekani!” alisema msichana huyo huku akionekana kutokuamini.

“Ndiyo hivyo! Esther…huyu Theo ni mtoto wangu pia,” alisema mzee huyo huku akimwangalia msichana huyo aliyekuwa na huzuni tele.

“Esther! Naomba unisamehe! Sikujua kama Fabian alikuwa ndugu yangu wa damu, nilifanya hivyo pasipo kujua, ninajuta, moyo wangu umeniuma sana, Esther! Naomba unisamehe,” alisema Theo huku akionekana kweli kuomba msamaha wa dhati.

Msichana huyo hakuwa na jinsi, mwanaume aliyesimama mbele yake alikuwa na chuki kali dhidi yake lakini kitendo cha kumuomba msamaha, hakuwa na kipingamizi chochote kile, akakubali na kumsamehe mwanaume huyo.

Siku hiyo hawakufanikiwa kumuona Fabian, wakaondoka na kurudi nyumbani. Theo akarudi nyumbani kwa mzee Edson ambaye hakuwa kwenye hali nzuri kiafya. Alipofika, akamuomba msamaha kwa yote yaliyotokea, alikuwa na kiu ya kuwafahamu wazazi wake na hatimaye aliwafahamu.

“Theo! Tulijua kwamba wewe haukuwa mtoto wetu, tumekulea kama mtoto wetu, tukakuheshimu na kukupa kila kitu, bado wewe ni mtoto wetu hata kama leo umekutana na wazazi wako. Tusamehe kwa kutokukwambia hili ukweli,” alisema mzee Edson huku akimwangalia Theo, pale alipokuwa, mzee huyo hakuweza hata kusimama.

“Usijali baba! Ninakupenda. Siku zote nimekuwa nikifikiri nyie ni wazazi wangu. Nimewaona wazazi wangu lakini kila siku nyie bado mtaendelea kuwa wazazi wangu,” alisema Theo na kisha kuwakumbatia.

Fabian aliendelea kuwa hospitalini, kidogo hali yake ilianza kutengemaa na baada ya wiki moja wakamchukua na kumpeleka katika Hospitali ya Marie Stoppes iliyokuwa Msasani jini Dar es Salaam.

Huko, matibabu yaliendelea zaidi na baada ya mwezi mmoja, akapata nafuu na hata kuanza kuzungumza. Alishangaa kumuona Theo mahali hapo, alimjua mwanaume huyo, alikuwa adui wake mkubwa, hakumpenda kwa sababu alijua hata kile kilichokuwa kimetokea alikisababisha yeye, ndiye aliyewatuma watu wale wamteke na kumpeleka porini kwa ajili ya kumuua.

Alihuzunika sana, alitaka Theo atoke ndani ya chumba hicho lakini alichokifanya Bwana Boniface ni kumwambia kile kilichokuwa kimetokea. Hakuamini kama kweli huyo alikuwa kaka yake, moyo wake uliumia kwani alifanyiwa mambo mengi na mtu huyo lakini kumbe nyuma ya pazia alikuwa kaka yake wa damu.

Baada ya wiki kadhaa, akatoka ndani ya hospitali hiyo, akawa mzima kabisa, moyo wake ukawa na msamaha, akamsamehe Theo na kuanza maisha mapya huku kila mmoja akiwa na furaha tele.

Kwa Bwana Edson, ugonjwa wa kisukari uliokuwa ukimtesa kitandani hatimaye akafariki dunia. Ilikuwa taarifa ya kuhuzunisha sana, kila mtu alihuzunika kwani mzee huyo alikuwa bilionea mkubwa, mwenye kampuni nyingi ambazo zote hizo akaziacha mikononi mwa mke wake na mtoto wake, Theo.

Upendo wa Theo kwa Bi Rachel haukupungua, kila siku alikuwa na mwanamke huyo na siku nyingine akiondoka na baba yake, Fabian kwenda kumuona mama yao katika Hospitali ya vichaa iliyokuwa Dodoma.

Wote walijisikia uchungu mioyoni mwao, walitamani kuzungumza na mama yao, wacheze naye na kufanya mambo mengine lakini haikuwezekana. Alizaliwa akiwa hivyo na kila mmoja aliamini kwamba angekufa akiwa katika hali hiyohiyo.

Theo hakutaka tena kuendelea kusoma, utajiri aliokuwa ameachiwa yeye na Bi Rachel ulikuwa mkubwa. Akaacha ujinga na kujikita katika biashara, hakutaka kuona mali hizo zikiteketea, alihakikisha kunakuwa na faida katika kuziendeleza.

Si yeye peke yake, akamchukua Fabian na kumuweka katika kampuni nyingine na kumfanya kuwa mkurugenzi huko. Mali hazikuwa zake peke yake, alikuwa na Bi Rachel ambaye kila siku alimuita mama lakini pamoja na hayo, zilikuwa za Fabian pia.

Alimpenda ndugu yake, walikuwa marafiki wakubwa, walisaidiana katika kila kitu, walipambana katika kila walilokuwa wakilifanya na baada ya miaka mitatu Fabian akamuoa msichana Esther katika Kanisa la Pentekoste lililokuwa Mwenge jijini Dar es Salaam.

“Ni mwisho wa kila kitu! Hongera sana, wewe umeanza na mimi nitafuata,” alisema Theo huku akimwangalia Fabian.

“Tutegemee lini?”
“Siku yoyote. Nitafanya saplaizi kubwa.”
“Kweli?”
“Niamini! Nimekamilisha kila kitu. Hoteli mtakayofikia ni The Amazon, ipo katikati ya Jiji la Las Vegas nchini Marekani. Ila mkiwa katika fungate hilo, hakikisha hauchezi kamari huko,” alisema Theo huku akicheka.

“Hahah! Siwezi bwana! Mimi si mcheza kamari”

“Basi sawa. Mtakaporudi, nataka huyu mwanamke tumbo liwe limevimba, sawa?” alisema Theo na kuuliza. Wote wakaanza kucheka.

Baada ya kumaliza sherehe ya harusi, siku iliyofuata Theo na Fabian wakaondoka zao na kuelekea nchini Marekani kwa ajili ya kula fungate. Kwa kila kitu kilichotokea baada ya hapo, kikawa historia, utajiri wao ukaongezeka maradufu huku upendo wa dhati ukiendelea kukua mioyoni mwao.

 

MWISHO

 

 

 

 

 

Comments are closed.