The House of Favourite Newspapers

Jaffarai Tusimtafute Yupo ‘Busy’

Jaffari Ali ‘Jaffarai’

WANAMUZIKI walioupandisha muziki wa Bongo Fleva hapa ulipo kwa sasa hata kuupa heshima ulionao ndani ya nchi na nje ni wengi na kila mmoja wao kwa namna moja au nyingine ana mchango wake mkubwa tu kwenye muziki huo, kiasi kwamba inakuwa ngumu kwa mashabiki kuwasahau moja kwa moja kutokana na kile walichokifanya.

 

Listi ipo ndefu lakini mmoja wao ni huyu jamaa Jaffari Ali ‘Jaffarai’ ambaye ngoma iliyomtambulisha kwenye gemu ni Niko Busy, aliyofanya na mwanamuziki kutoka Kundi la Daz Nundaz anayefahamika zaidi kwa jina la Daz Baba.

 

Kwa wafuatiliaji wa muziki bila shaka wanamfahamu vyema Jaffarai, kwani amedumu kwenye gemu kwa zaidi ya miaka 18. Hata hivyo pamoja na kazi nzuri aliyoifanya mshikaji huyu kwa sasa hasikiki tena, yapata miaka mitatu hajaachia ngoma yoyote, ngoma yake ya mwisho ni Wakati aliyofanya na Kassim Mganga, na Risasi Mchanganyiko limeweza kumtafuta ili mashabiki wake waweze kufahamu yupo wapi na anafanya nini. Huyu hapa akifanya mahojiano;

Risasi: Jaffarai mambo vipi, kimya sana mzee!

Jaffarai: Mambo poa, nipo naendelea tu na maisha kama kawaida.

Risasi: Tangu mwaka 2015 hatujasikia lolote lile kutoka kwako, ndiyo umeamua kuupiga chini muziki?

Jaffarai: Hapana, siwezi kuacha muziki, nipo tu busy na biashara zangu kwa sasa. Mungu akijaalia nitarudi tena.

Risasi: Siyo kwamba changamoto za gemu ndizo zimekukimbiza?

Jaffarai: Hapana, ni mambo tu ya kimaisha, unafika wakati mtu unaangalia ufanye mambo gani mengine. Kumbuka nimefanya gemu hili la muziki kwa miaka zaidi ya 18, kuna changamoto gani ambayo siifahamu. Kama ninaifahamu kwa namna yoyote ile ninafahamu namna ya kuitatua, kwa hiyo siyo kwamba nimekimbia gemu ila nipo tu ‘busy’ mashabiki wasinitafute sana.

Risasi: Sawa, ingawa upo nje ya gemu lakini bila shaka unasikiliza muziki, ni wanamuziki gani ambao kwa sasa unawasikiliza na kuwakubali?

Jaffarai: Kiukweli wanaofanya vizuri wapo wengi akiwemo, Bill Nas, MwanaFA, Fid Q bado wanawakilisha na wengine wengi.

 

 

Risasi: Umefanya ‘hit song’ nyingi na wanamuziki wengi, akiwemo Q Chief wimbo Hawapendi, Sio Kweli na Lady Jay Dee, Unapenda Nini na Fatuma pamoja na nyingine nyingi, nini ilikuwa sababu hasa ya wewe kupenda kufanya kolabo?

Jaffarai: Unajua mimi ni mwanamuziki wa kuchana na sifahamu kuimba. Nilikuwa ninatafuta watu wa kuimba ili kulainisha kidogo nyimbo zangu na kama ukisikiliza vizuri nyimbo zangu nilikuwa ninaimba kwa mistari ya kawaida inayoeleweka ili kumpa nafasi mtu yeyote kuishika.

Risasi: Kati ya nyimbo zako zote ni wimbo upi ulikupa mafanikio zaidi?

Jaffarai: Wengi wanafikiri ni Wimbo wa Nipo Busy. Lakini ukweli ni kwamba wimbo niliofanya na Q Chief uitwao Hawapendi ndiyo ulinitambulisha zaidi kwenye gemu na kunifanya nipate shoo kibao kuliko ngoma zangu zote.

Risasi: Kipi ambacho huwezi kusahau kwenye gemu?

Jaffarai: Yapo mengi, ikiwemo upendo kutoka kwa mashabiki, kuwa na ngoma kali halafu hupati shoo na mengine mengi.

Risasi: Kwa upande wa familia vipi, tayari ushavuta jiko?

Jaffarai: Bado. Nina mtoto mmoja lakini sijaoa bado.

Risasi: Mashabiki wako unawaachia nini kwenye makala hii?

Jaffarai: Nitarudi nikiweka mambo yangu ya kibiashara vizuri, kwa sasa nipo busy lakini watambue kwamba nipo.

MAKALA: BONIPHACE NGUMIJE

Comments are closed.