The House of Favourite Newspapers

Jaji Mkuu Atembelea Chumba Cha Mrejesho wa Taarifa za Kielektroni za Mahakama

0
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (wa kwanza kulia) akipata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi wa TEMAHA, Mahakama ya Tanzania, Bw. Kalege Enock (katikati). Mhe. Prof. Juma ametembelea Chumba cha Mrejesho wa Taarifa za Kielektroni za Mahakama kilichopo Mahakama Kuu Dar es Salaam

 

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma leo tarehe 29 Julai, 2022 ametembelea Chumba cha Mrejesho wa Taarifa za Kielektroni za Mahakama kilichopo Mahakama Kuu Dar es Salaam ambapo ameipongeza Kurugenzi ya TEHAMA kwa kutekeleza ahadi waliyoitoa mbele ya Benki ya Dunia katika kuboresha Teknolojia mahakamani.

Akizungumza na watumishi wa Kurungenzi hiyo, Mhe. Prof. Juma amesema ana imani kubwa na wao kuwa wataendelea na ubunifu ili kuboresha huduma wanazotoa ili kukidhi matarajio yanayokusudiwa kwa kuzingatia moja ya vipimo vya Benki ya Dunia kuhusu mafanikio ya Mradi wa Uboreshaji ni kwa kiasi gani Chumba hicho cha Mrejesho ‘Dashboard’ zake zinafanya kazi na zinasaidia katika uamuzi wa Kisera na Kiutendaji unaofanywa na viongozi wa Mahakama.

 

“Kazi mnayofanya ina umuhimu mkubwa katika kuwezesha uongozi wa Mahakama kufanya uaamuzi (katika masuala mbalimbali, ikiwemo ya) Kisera, Kiutendaji na Uboreshaji wenye tija na faida kubwa zaidi kwa Mhimili na nchi. Matarajio yetu kwa Idara ya TEHAMA na watumishi wake ni makubwa mno, binafsi sina wasiwasi na timu yenu,”  amesema Jaji Mkuu.

 

Hivyo, amekitaka Chumba hicho cha Mrejesho kujenga na kuendesha mfumo wa kitaasisi utakaotumia TEHAMA kutenganisha ukusanyaji wa Data za Kijinsia na kuzifanyia uchambuzi wa kina, kutumia mfumo wa uendeshaji wa mashauri (JSDS2) kufanya uchambuzi wa kina wa Data na Takwimu ili usaidie kuelewa mapungufu ya kijinsia na vizuizi vya kijinsia na pia kuwezesha uongozi wa Mahakama kufanya uamuzi wa Kisera na Kiutendaji kwa kuzingatia Data na Takwimu hizo za kijinsia.

 

“Kwa mujibu wa Andiko la Mradi, Benki ya Dunia itafanya tathmini ya huduma za Chumba cha Mrejesho wa Taarifa za Kielektroni za Mahakama, watapenda kujua idadi za uamuzi wa Kisera na Kiutawala uliojulishwa na mfumo wa ‘Dashboard‘ wa Chumba cha Mrejesho,” Mhe. Prof. Juma amesema.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akielekeza jambo kupitia hotuba yake aliyoandaa wakati alipotembelea Chumba cha Mrejesho wa Taarifa za Kielektroni za Mahakama. Waliosimama kulia kwa Jaji Mkuu ni sehemu ya Maafisa TEHAMA wa Mahakama.

 

Chumba cha Mrejesho wa Taarifa za Kielektroni za Mahakama ni mfano wa matokeo ya ziara ya kujifunza iliyofanyika Ufaransa na Kazakhstan iliyofanywa na viongozi mbalimbali wa Mahakama ili  kujiongezea maarifa na uzoefu katika utoaji mafunzo kwenye shughuli za utoaji haki, uboreshaji wa huduma za utoaji haki na huduma za utoaji haki kwa njia za mtandao na kuboresha miundombinu za usogezaji wa huduma za haki karibu zaidi na wananchi.

 

“Ziara katika nchi ya Ufaransa ililenga kujifunza dhana ya Vituo Jumuishi vya Utoaji Haki (Integrated Justice Centres), njia bora za utoaji wa mafunzo endelevu kwa watumishi wa Mahakama, mikakati ya uboreshaji wa miundombinu ya Mahakama kuleta faida za ufanisi, uwazi na upatikanaji wa haki kwa urahisi na wepesi,” alisema.

 

Amebainisha pia kuwa, msisitizo katika ziara ya Kazakhstan ulikuwa kujifunza miundombinu ya kisasa ya kiteknolojia kupitia Chumna maalumu cha Mrejesho ambacho kinatumia Dashboard kutoa taarifa za kitendaji, takwimu za utendaji kazi zinazoweza kutumika katika uamuzi wa kisera, ufuatiliaji na kutathmini, ufuatiliaji wa huduma za haki-mtandao, kuboresha shughuli za utawala, uendeshaji, utendaji katika ngazi zote za mahakama pamoja na matumizi ya utatuzi mbadala wa migogoro.

 

Naye; Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani ameitaka Kurugenzi hiyo kuboresha zaidi mazingira ya kuhifadhi chumba hicho muhimu kwa uendeshaji wa Mahakama huku akiainisha kuwa na eneo kubwa zaidi la kuhifadhi vifaa vya TEHAMA vinavyotumika katika jengo la Makao Makuu-Dodoma pamoja na kuwa wabunifu zaidi.

 

“Hili ni eneo muhimu sana kwa uendeshaji wa shughuli za Mahakama, hivyo, ni muhimu kulipa uzito wa kipekee kwa kuboresha zaidi, ni rai yangu kuhakikisha pia kuna eneo kubwa zaidi kwenye jengo la Makao ili kuwezesha kuwa na mazingira mazuri zaidi hata ya wengine kuja kujifunza,” amesema Jaji Kiongozi.

 

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa TEHAMA, Mahakama ya Tanzania, Bw. Kalege Enock amesema kuwa chumba hicho ni muhimu na kisaidia upatikanaji wa taarifa mbalimbali za Mahakama, huku akimuhakikishia Jaji Mkuu kuwa wanaendelea kuboresha zaidi ili kuendana na kasi ya teknolojia.

 

Na Mary Gwera, Mahakama

Leave A Reply