The House of Favourite Newspapers

Jamani Antiii…Nishushe Ununio..!-3

0

ILIPOISHIA KWENYE RISASI MCHANGANYIKO: “Acha mambo yako bwana, ngoja niondoke,” Vivian alisema huku akikanyaga mguu kwenye kigingi cha kukanyagia kabla ya kukaa vyema kwenye kiti cha pikipiki, ambapo yule kijana hakuwa na muda wa kupoteza zaidi ya kutia gia na kuondoka kwa kasi na kumuacha Bigambo akikodoa macho huku akicheka na kujisifia moyoni kwa namna ambavyo ameweza kumpata Vivian kwa urahisi na wepesi wa namna hiyo. Kwa upande wa Vivian, kichwani alikuwa na maswali mengi ambayo hayakuwa na majibu kwa wakati huo. “Hivi kweli mimi Vivian nimekuwa mtu wa kupatikana kwa mwanaume kirahisi namna hii? Ama kweli Bigambo ni kiboko lakini hata hivyo amesaidiwa sana na utundu wake pamoja na ile hali ya kunijali, maana nina siku nyingi sana sijaoneshwa upendo wa namna hii kwenye mapenzi, Bigambo ananifaa sana kwenye maisha yangu ya ndoa, tena ni mtu mwelewa kwa mambo mengi ya kimaisha,” Vivian alikuwa akiwaza kabla ya kufika nyumbani kwake ambpo alikuta mtu amesimama wima akimngoja kwa hamu na shauku kubwa.

 

CHECHEMEA NAYO SASA… VIVIAN alishtuka sana, kitendo cha kuona mtu amesimama wima mlangoni mwake, kilimgutua kutokana na ukweli kwamba hakutarajia kabisa, licha ya kwamba hadi wakati huo hakuwa amejua ni nani alikuwa amesimama mlangoni kwake. “Aaah, jamani umenishtua sana sasa mbona hujaniambia kama unakuja au simu yangu huna?” Vivian alisikika akimlalamikia mtu huyo baada ya kujua ni nani. Jamaa aliyekuwa amesimama mlangoni kwa Vivian alikuwa mzazi mwenzake na mwanamke huyo, ambaye uhusiano wao ulishaanza kuyumba ingawa ana haki zote za kuja nyumbani kwa Vivian wakati wowote kwa lengo la kumjulia hali mtoto ingawa wakati mwingi huwa yuko shule.

 

“Kwani jamani kila nikija hapa ni lazima nitoe taarifa au kuna mabadiliko mapya tena kwenye mji huu, halafu muda kama huu unatoka wapi Mama Edson au unataka kutumia mwanya wa kutofautiana kwetu kama njia ya kujipatia uhuru uliopitiliza, haiwezekani nakuambia,” mwanaume huyo alianza kutiririka maneno mengi tena bila kuzingatia vituo na koma kama siyo nukta. “Hivi Raphael, tangu lini tukaanza kuwekeana masharti nyumbani kwangu? Wewe si una kanuni ya kuja hapa Jumamosi na kuondoka Jumapili ili upate nafasi ya kuzungumza na mwanao, sasa leo kimekuleta nini? Yaani unataka nikose hata uhuru wa kazi zangu za kiofisi kwa sababu ya kukuwahi wewe ambaye sina mkataba na wewe zaidi ya kuja hapa kumjulia hali mwanao?”

 

Kwanza nataka tuanze utaratibu mpya wa kumsalimia Edson, kwani kwa mtindo huu hapana kabisa jamani, aaah,” Vivian naye alijibu kwa maneno mengi na sentensi ndefu zenye kuchosha kusikiliza. “Utaratibu gani unaotaka uanzishe kuhusu mimi kumjulia hali mwanangu?”

 

“Uwe unakuja na kuondoka, masuala ya kulala hapa wakati mimi na wewe siyo mke na mume sitaki tena kwa kweli,” Vivian alikazia tena huku akiwa amesimama wima karibu kabisa na mwanaume huyo ambye jina lake ni Raphael kama alivyomtaja. “Unasemaje wewe nyang’au?” “Unaniitaje Raphael?” “Wewe nyang’au tu, tena usinipandishie nisije nikakubadilikia sasa hivi nikakuwasha makofi bure, umenielewa?” “Babu wee, achana na mimi bwana, mwanaume gani usiulizwe, yaani kuniijia usiku nyumbani kwangu tena bila taarifa wakati namba yangu ya simu unayo halafu unataka usiulizwe, ulishawahi kutoa hata senti tano yako kwenye kulipia kodi ya hii nyumba? Tena angalia kabisa usije ukanitibua usiku huu,” Vivian alisema huku akipiga hatua kuingia ndani akimuacha Raphael peke yake nje ya mlango. Wakati Vivian akiingia ndani, ghafla simu yake iliita na alipotupa macho kwenye kioo, aliona jina la Bigambo wangu, bila kujiuliza mara mbilimbili alipokea na kupeleka sikioni tena kwa sauti ya kudeka kulikopitiliza.

 

“Yes, baby wangu jamaniiii,” Vivian alianza kwa maneno hayo huku akizidisha kuibana sauti yake isitoke kwa ufasaha kwenye mdomo na badala yake ibanane kwenye zile tundu mbili za pua. “Niambie mama.” “Nipo baby wangu, niambie unafanya nini kwa sasa?” “Niko tu nyumbani Vivian, wewe umeshafika,” Bigambo aliuliza akiwa amekaa ndani kitandani kwake, muda mfupi baada ya kutoka bafuni kujiweka sawa kwa uchovu wa mechi kali aliyotoka kupiga na Vivian. “Ndiyo naingia sasa hivi lakini kuna mtu ameniudhi sana baba yangu.”

 

“Nani tena huyo jamani mama?” “Aaah nitakuambia wangu, kuna watu duniani wakiingia maishani mwako huwa ni kama laana na kuna wengine wakiungana na wewe maishani mwako kama ulivyofanya kwangu baba huwa ni baraka kubwa, sasa huyu aliyenikera sasa hivi ni wale watu wa kundi la kwanza nililokueleza,” alisema Vivian wakati wote huo Raphael akiwa nje akisikiliza kila kitu kilichokuwa kinazungumzwa na Vivian na Bigambo, kwani simu ya Vivian ilikuwa na sauti kubwa hata kama haijawekwa mfumo wa sauti ya nje (loud speaker). Haisra zilizidi kumpanda Raphael. Ni kweli kabisa hana uhusiano wa ndoa na Vivian baada ya kuachana kwa tofauti za kibinadamu na kukubaliana kulea mtoto wakiwa mbalimbali na kisha baadaye kuzaa suala la kulala pamoja baada ya siku moja kunywa pombe na kupitiliza ambapo waliamua kukumbushia penzi lao na kuanzia siku hiyo walianza tabia ya kulala pamoja kila Raphael alipokwenda kumjulia hali mwanaye.

 

“Unajua nitaonekana mwanaume mjinga sana kama nitatoka hapa bila kumuwasha japo vibao viwili huyu mwanamke, hata kama siishi naye lakini heshima ya kwamba nimezaa naye inabaki palepale na anapaswa kuniheshimu na siyo kunioneshea dharau za wazi namna hii kwa kuzungumza na wanaume kwenye simu ilhali anajua kabisa mimi nipo hapa,” aliwaza Raphael huku akijiandaa kuingia ndani. * * * Wakati Vivian akizungumza na simu, alifunga mlango kwa komeo wakati Raphael akiwa amezama kwenye lindi la mawazo mengi, hivyo hakushtukia wala kujua ni saa ngapi Vivian alifunga mlango wa kuingilia ndani ya nyumba hiyo yenye chumba kimoja na sebule ukichilia mbali chumba cha nje ambacho kiko maalum kwa ajili ya wageni. “Sasa baby, unaonaje kama nitapika kwanza ndipo tuongee baadaye nikiwa kitandani mume wangu?” Vivian alisema akimwambia Bigambo kupitia simu, katika kumalizia mazungumzo yao ya wakati huo. “Sawa mama na mimi ngoja nikaangalie chakula huko nje ndipo nije nilale.”

 

“Jamani baby, hivi huwa haupiki?” “Sipiki na sina mpango huo.” “Ndiyo maana hunenepi mume wangu, sasa hivi nimeingia maishani mwako nitahakikisha unanunua vyombo kama huna ili niwe nakuja kukupikia mwanaume wangu, sawa baba?” “Mmmh…,” Bigambo aliishia kuguna. “Unaguna nini?” “Si maneno yako jamani.” “Yamefanyaje?” “Hayo ya kunipikia, hakika nitanenepeana sana.” “Sana, huo mwili siyo
wako.” “Sawa, tutaona mama.” “Okey, baadaye basi baba, nitakutafuta nikiivisha.” “Sawa mke wangu,” Bigambo alimalizia na maneno hayo bila kujua kwamba anampa wakati mgumu sana Vivian ambaye alikuwa amempenda kupitiliza kutokana na mavituz kama siyo majambozi ambayo alikuwa amemuonesha muda mfupi uliopita, kwa hiyo hata ile jeuri ya kumjibu maneno makali Raphael ilitokana na kuvimbishwa kichwa na penzi tamu la Bigambo. Raphael alihamaki baada ya kuusukuma mlango na kugundua kwamba umeshafungwa kwa ndani, ni hapo ndipo hasira yake ikazidi kupanda maradufu.

 

“Wewe Vivian wewe, hivi unawezaje kunifungia nje wakati unajua kabisa niko hapa kwa ajili yako?” Raphael alianza kulalama tena huku akiutingisha mlango kama anayetaka kujiridhisha kama kweli Vivian alikuwa amemfungia kwa nje. “Bab wee, umekuja kwa ajili yangu au kwa ajili ya mwanao na unajua kabisa kwamba siku kama hizi anakuwa yuko shule, mwenzangu labda ulikuwa na safari zako ndiyo maana ukaamua kunishtukiza kuja kwangu bila kunitaarifu, halafu nakuuliza na badala ya kujibu kistaarabu eti unaanza kunipandishia maneno ya jeuri ya kimfumo dume, sasa wewe si ulianza, mimi namalizia ukurasa,” Vivian alisema huku akitweta na kuhema. Raphael alirudi nyuma na kuukanyaga mlango kwa nguvu huku akitamka maneno ambayo yaliwafanya hata majirani washtuke na kuamka kabisa ili kuja kutuliza soo la varangati ambalo alikuwa amelianzisha Raphael nyumbani kwa Vivian. Je, nini kitafuata? Usikose kufutilia kwenye Gazeti la Risasi Jumamosi kujua nini kilijiri. Kwa maoni na ushauri usikose kuwasiliana nami kupitia namba hizi; 0673 42 38 45. (tuma sms tu).

NA IRENE MWAMFUPE NDAUKA

Leave A Reply