The House of Favourite Newspapers

Joh Makini Atoboa Siri ya Kuwa Bachela!

0

MUZIKI wa Bongo Fleva uliasisiwa na wakongwe mbalimbali kwa kuutangaza na kuujenga.Miongoni mwa wakongwe ambao wamejua kulijenga gemu la muziki wa kufokafoka (Hip Hop Bongo) ni Joh Makini.

 

Huyu ni memba wa kundi kubwa la wagumu kutoka A City au R Chuga la Weusi.Jina halisi ni John Simon ambaye yuko pamoja na memba wengine wa kundi hilo, Nickson Simon ‘Nikki wa Pili’, George Mdemu ‘G Nako’ na Isaac Waziri ‘Lord Eyez’.Joh Makini ni msanii maarufu kutoka pande za Arusha Eneo la Daraja-Mbili.

 

Ni kioo cha heshima katika muziki wa Hip Hop, mtunzi na mtengenezaji wa muziki Bongo.Joh Makini ana sifa ya kipekee katika matumizi ya sitiari na ubunifu wa kutupia free style na uwezo wa kucheza na ngeli.

 

Mwamba huyu ana mvuto wa kipekee kwenye jukwaa ambao unawakuna mashabiki wa Hip Hop Bongo kwani amewahi kupanda jukwaani na wanamuziki maarufu na wakubwa wa Afrika kama Nonini, Chameleone, P-Square, D’Banj, Diamond, Juliana, Wyre na Prezzo.

 

Mbali na hilo, Joh Makini anasifika kwa kuwahi kufanya maonesho na wasanii wa kimataifa kama Jay-Z, Ja Rule, 50 Cent, Fat Joe, Eve, Busta Rhymes, Sean Kingston, Fabulous na Kat Deluna.

 

Mwanzoni mwa miaka ya 2000, mashabiki wa Hip Hop Bongo, walitambua uwepo wa Joh Makini kwenye gemu.Joh Makini alisikika na anasikika mno na mikwaju yake mikali kama Karibu Tena, Stimu Zimelipiwa, XO, Don’t Bother, Perfect Combo, Mipaka, Simwachii Mungu, Niaje Nivipi na nyingine kali.Akiwa na Weusi, Joh Makini amesikika na mikwaju mingine kama Bei ya Mkaa, Nje ya Box, Gere, Show Time, Madaraka ya Kulevya, Swagire, Ni Come, Wapolo, Hawatuwezi na nyingine kibao.

Weusi wamekuwa wakisifika kwa kuamsha kwenye majukwaa ya matamasha makubwa ndani na nje ya nchi huku Joh Makini akitisha kama mwandishi wa mashairi makali ya ngoma zake na hata za kundi.

 

Kwa sasa, huyu mwamba anatisha na ngoma zake mpya kama Dangerous akiwa na Nahreel na Wembe akiwa na mwanadada mkongwe kwenye Bongo Fleva, Judith Wambura ‘Lady Jaydee’ au ‘Jide’.

 

IJUMAA SHOWBI

Zimefanya mahojiano maalum (exclusive interview) na Joh Makini ambaye amefunguka mengi ikiwemo kuanzisha lebo yake mpya ya muziki nje ya Kundi la Weusi inayojulikana kwa jina la Makini Records na zaidi ni siri aliyoiweka wazi juu ya swali linaloulizwa zaidi la kwa nini umri umekwenda, lakini bado ni bachela IJUMAA SHOWBIZ: Hongera kwa uzinduzi wa lebo yako ya Makini Records…

JOH MAKINI: Nashukuru sana, hii ilikuwa ndoto yangu ya muda mrefu ila kwa sasa imetimia.

 

IJUMAA SHOWBIZ: Umesema ni ndoto yako ya muda mrefu, mashabiki wangependa kujua imekuchukua muda gani hadi kutimia?

JOH MAKINI: Tangu nimeingia kwenye muziki, hii ilikuwa ni ndoto yangu ninayoiota kila siku ya kuja kuwa na record lebo yangu mimi kama mimi.

IJUMAA SHOWBIZ: Vipi kuhusiana na Kundi la Weusi ndiyo unatengana nalo au bado mpo pamoja?

JOH MAKINI: Hapana, bado nipo nao na tunafanya kazi kwa pamoja, hii lebo yangu ni kwa ajili ya kusaidia kuinua vipaji vya wasanii ili kutimiza ndoto zao.

IJUMAA SHOWBIZ:Wasanii wenzako kwenye Kundi la Weusi wana mchango gani kwenye hili?

JOH MAKINI: Niseme tu, nashukuru sana wananisapoti na pia na wao wamefurahi kwenye hili.

 

IJUMAA SHOWBIZ:Tumeona umeanza kumsaini msanii wa kiume na tunafahamu kwamba lady is first, kuna siri gani nyuma ya pazia?

 

JOH MAKINI: Kwa kweli kwa upande wetu hatuangalii suala la gender (jinsia), tunaangalia mtu mwenye kipaji, heshima na utayari katika kufanya kazi.

 

IJUMAA SHOWBIZ:Joh Makini wewe ni msanii mkongwe, unaonaje upepo unavyokwenda kwenye gemu la Hip Hop Bongo ukilinganisha na zamani?

 

JOH MAKINI: Muziki ni kitu ambacho kinazunguka, kama ambavyo siku hazifanani na vitu vilivyokuwa vinafanyika nyuma na sasa ni tofauti kabisa, kwa hiyo muziki wa Hip Hop wa zamani na sasa ni tofauti.

 

IJUMAA SHOWBIZ:Tumeona mdogo wako, Nikki wa Pili ameoa, je, kwa upande wako mipango iko vipi?

 

JOH MAKINI: (anacheka), unajua mimi siwezi kufosi kitu, eti kwa sababu fulani amefanya, yeye ameona muda wake umefika na ameridhia kuoa, muache aoe ila kwangu muda wangu bado haujafika. Kwa sasa mimi ni bachela ila muda ukifika Mungu ataniletea.

 

IJUMAA SHOWBIZ: Kama kundi mna mpango gani wa kuachia album?JOH MAKINI: Album ya Weusi tayari imeshakamilika na muda siyo mrefu tutaiachia, lakini tumeona pia tuiachie baada ya uchaguzi mkuu kuisha ndiyo utakuwa wakati mzuri zaidi.

 

IJUMAA SHOWBIZ:Inakwenda kwa jina gani?

 

JOH MAKINI: Jina la album litakuwa ni surprise kwa mashabiki.

 

IJUMAA SHOWBIZ: Je, ni mjumuiko wa memba wa Weusi tu au kuna ushirikiano wa wasanii wengine?

 

JOH MAKINI: Ndani ya album hiyo, tumeshirikisha baadhi ya wasanii kama Jux (Juma Mussa) na msanii wangu mpya ambaye anaitwa Attu William.

 

IJUMAA SHOWBIZ:Album ina jumla ya ngoma ngapi?

 

JOH MAKINI: Ina nyimbo zaidi ya 20.

 

IJUMAA SHOWBIZ:Baada ya album ya kundi, je, mipango ya kuachia album yako mwenyewe imekaaje? JOH MAKINI: Kwa upande wa album yangu mipango ipo ila baada ya kuachia ya kundi ndipo nitatambulisha ya kwangu mwenyewe.

 

IJUMAA SHOWBIZ: Baadhi ya wanamuziki wa Hip Hop, wamegombea nafasi mbalimbali za uongozi hapa nchini, je, kwa upande wako hukuwaza kufanya hivyo?

 

JOH MAKINI:(anacheka) kiukweli sijawahi kuwaza hicho kitu kabisa, mimi nipo na muziki ila ni watu wengi wananiambia napendeza kuwa mwanasiasa, unajua hiyo ni mipango ya Mungu, akipanga mimi ni nani nipangue?Waandishi:Khadija Bakari na Faudhia Gea (TUDARCo)

MAKALA: WAANDISHI WETU

Leave A Reply