The House of Favourite Newspapers

Jonas Mkude Aliamsha Jipya Simba SC

KIUNGO mkabaji wa Simba, Jonas Mkude, amezua balaa lingine mara baada ya jana kuchelewa mazoezini na kusababisha awekwe kitimoto na uongozi wa benchi la ufundi. Simba, jana Ijumaa ilifanya mazoezi kwenye Viwanja vya Gymkhana, Posta jijini Dar wakijiandaa na mechi dhidi ya Singida United itakayopigwa kesho na leo Jumamosi Simba itaondoka kwa ndege kuelekea Arusha kwa ajili ya mechi hiyo.

 

Turudi mazoezini; Mkude aliwasili kwenye viwanja hivyo na gari yake binafsi aina ya Toyota Harrier, ikiwa imeshapita zaidi ya nusu saa tangu wachezaji wenzake waanze mazoezi.

 

Baada ya kushuka kwenye gari alikutana na meneja wa timu hiyo, Patrick Rweyemamu ambaye alionekana kuchukizwa na kitendo hicho na kumuonya kabla ya kwenda kukutana na kocha mkuu wa timu hiyo, Mbelgiji, Patrick Aussems.

 

Hata hivyo, baada ya mazungumzo na Aussems, Mkude ambaye ni majeruhi alikutana na jopo la madaktari wa timu hiyo wakiongozwa na Yassin Gembe kisha kuwekwa kitimoto kuhusiana na kuchelewa kwake.

 

Hata hivyo, baada ya mazungumzo jopo hilo lilimpatia programu maalumu kwa ajili ya mazoezi ili kuhakikisha anakuwa fiti huku wakimtaka kuhakikisha anazingatia programu ya mazoezi ya gym. Baada ya hapo, Mkude alianza mazoezi ya kukimbia peke yake kuuzunguka uwanjani.

 

Kutokana na tukio hilo, huo unakuwa ni mfululizo wa matukio ya utovu wa nidhamu ambao Mkude amekuwa akifanya, hivi karibuni anaripotiwa hakusafiri na timu kwenda Kagera kucheza mechi za Kanda ya Ziwa dhidi ya Kagera Sugar na Biashara United.

STORI NA ISSA LIPONDA, ABDULGHAFAL ALLY

Comments are closed.