The House of Favourite Newspapers

Joseph Shaluwa Ang’ara Tamasha la Mjue Mtunzi 2022, Atunukiwa Ngao ya Heshima

0
Joseph Shaluwa akiwa na msanifu kurasa wake mkuu, Upendo Haule ambaye pia ni mkewe.

 

MWANDISHI wa habari ambaye pia ni mtunzi nyota wa riwaya za Kiswahili nchini Tanzania, Joseph Shaluwa ameng’ara katika Tamasha la Mjue Mtunzi 2022, baada ya kutunukiwa Ngao ya Mtunzi.

Tamasha hilo lilifanyika jana Julai 3, 2022 katika Ukumbi wa NSSF MAFAO HOUSE, Ilala Boma, jijini Dar es Salaam, ambapo Shaluwa pamoja na watunzi wengine wawili; Ibrahim Gama na Elizabeth Mramba wametunukiwa ngao hizo.

 

Shaluwa akiwa na mwandishi mwandamizi wa magazeti ya Championi, Wilbert Molandi (kushoto).

 

Shaluwa na wenzake hao wawili walitunukiwa ngao hizi na Umoja wa Waandishi wa Riwaya Wenye Dira Tanzania (UWARIDI) ambapo walikabidhiwa na mgeni rasmi, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Profesa Adolph Mkenda.

Mjue Mtunzi ni tamasha la kila mwaka linaloandiliwa na UWARIDI, likiwakutanisha wapenzi wa riwaya nchini kwa lengo la kufahamiana na watunzi wao, kupiga picha na kubadilisha mawazo.

Miongoni mwa waandishi wakubwa waliohududhuria tamasha hilo lililoongozwa na mshereheshaji mkongwe nchini, Taji Liundi ni pamoja na Adam Shafi ambaye anaendelea kuteka hisia za wengi na vitabu vyake vya KULI na VUTA NIKUTE ambacho kwa sasa kimetengenezwa filamu inayosumbua duniani.

 

Shaluwa akipongezwa na Mhariri wa Gazeti la Ijumaa, Sifael Paul (kulia).

 

Mara baada ya Shaluwa kupewa ngao hiyo, aliamua kuirudisa nyumbani Global Publishers, kampuni ambayo kwa maneno yake mwenyewe anasema, ‘imemlea, ikamkuza na kumfikisha hapa alipo’.

 

“Nilipotunukiwa hii ngao jana, nikasema hapana, lazima ije Global, maana hii ni mali yetu sote. Tumeipigania hakika. Nimejiunga na Global tangu mwaka 2006, wakati huo tukiwa Kariakoo.

 

Shaluwa akipongezwa na Aziz Hashim, Mhariri wa Maudhui ya Mtandaoni wa Global Publishers (kulia).

“Mkurugenzi (Eric Shigongo) aliniamini, akaniruhusu nionyeshe kipaji changu hapa ofisini. Mpaka leo nina jina kubwa, nimeandika vitabu vingi na ninashirikiana na wengi katika kazi hii, lakini lazima heshima ya Global ibaki palepale. Wamenitoa mbali na kwa hakika tuzo hii ni yao. Hii ndiyo sababu nimeileta hapa nyumbani,” Shaluwa alimwambia Mhariri Mtendaji wa Global, Saleh Ally wakati akimkabidhi ngao hiyo ofisini kwake.

 

Akizungumzia ngao hiyo, Meneja Mkuu wa Global Group, Abdallah Mrisho, alimpongeza Shaluwa kwa heshima hiyo, lakini zaidi akamshukuru kwa kukumbuka kurudisha ngao nyumbani.

 

Shaluwa akipongezwa na Wahariri wa Magazeti ya Championi. Kutoka kushoto ni Lucy Mgina, Omary Mdose, Shaluwa na Said Ally. 

 

“Nakupongeza sana Shaluwa, hii sasa inaonyesha dhahiri kwamba ukifanya kazi kwa bidii, ubunifu na ubora unaotukuta, jasho lako haliendi bure. Nakupongeza pia kwa kukumbuka kitovu chako. Huu ni mfano wa kuigwa. Kwa hakika najivunia sana wewe, kwa sababu nakufahamu tangu ukiwa kijana mdogo kabisa. U msikivu, unajifunza kila siku na una bidii sana. Usichoke, utapata kikubwa zaidi ya hiki siku moja,” alisema Mrisho.

Leave A Reply