The House of Favourite Newspapers

Joshua: Nilishiriki Ufuska, Ushirikina!

0

Na GLADNESS MALLYA

MAFANIKIO ya mtu yeyote huambatana na simulizi nyingi za kusisimua, zinazoambatana na mikasa isiyofikirika, kama unavyoweza kuipata unaporejea historia ya mwimbaji maarufu wa muziki wa Injili nchini, Joshua Mlelwa, anayetamba na albamu yake ya Ni Wewe.

Kabla ya kufika hapo alipo, amewahi kupitia katika maisha ya uchafu ambayo yalimtesa kimwili na kiroho.

Miongoni mwa mambo aliyofanya ni pamoja na kuamini na baadaye kushiriki vitendo vya kishirikina baada ya kuugua tumbo kwa muda mrefu. Kwa sababu hiyo, alienda kwa waganga mbalimbali wa kienyeji kwa ajili ya kupata tiba, mpaka ikafikia hatua ya kuchimbiwa kaburi na kuogeshwa humo na kuacha nguo ndani yake, lakini bado hakupona.

Historia yake fupi ya uimbaji

Alianza kuimba tangu akiwa mdogo lakini rasmi alianza kwenye Kwaya ya KKKT, Sumbawanga mwaka 1992. Mwaka 1998 alihamia Moshi na kujiunga na Kwaya ya KKKT Tangazeni, Usharika wa Moshi Kati kabla ya kuhamia kwaya ya Uinjilisti Majengo.

Mwaka 1999 alienda Dar ambako akiwa na wenzake, walianzisha Upendo Group ambalo lilidumu mpaka mwaka 2010 alipoamua kuimba nyimbo zake mwenyewe na kutoa albamu yake ya Ni Wewe mwaka 2011.

Kitu kibaya alichofanya kabla ya kuokoka

Kabla ya kuokoka, Joshua anasema alikuwa mshirikina na mzinzi, kwani wakati akiimba kwaya, alitumia nafasi yake ya ualimu kuwarubuni wasichana wadogo waimba kwaya na kufanya nao uzinzi kila baada ya mazoezi.

Kilichosababisha kuokoka

Aliamua kuokoka baada ya ushiriki wake kwenye ushirikina kushindwa kumaliza maumivu ya tumbo, hivyo kuachana na waganga wa aina mbalimbali za kienyeji na kwenda kwa Mchungaji wa Kanisa la Pentekoste, Rafael maeneo ya Kiluvya, Dar ambaye alimuombea na kupona. Tangu hapo, akaachana na maisha ya dunia.

Anasemaje juu ya wanaoimba Injili kwa ajili ya fedha?

Anawasihi waingie katika huduma ya uimbaji wa Injili kwa kumtafuta Mungu kwanza halafu baadaye ndiyo fedha zije, kwani wanaoingia kwa lengo hilo wataacha tu mara moja maana huduma hii ni ya kiroho zaidi.

Ni kweli muziki wa Injili unalipa?

Siyo kwamba muziki wa Injili unalipa isipokuwa Yesu ndiye anayelipa, hivyo ukiingia kwa ajili ya kuutangaza utukufu wa Mungu na kuponya roho za watu utafanikiwa lakini kinyume cha hapo utapotea mara moja.

Vipi skendo za waimbaji wa Injili?

Unajua siyo kila anayeimba anampenda Mungu, bali wengine wanaimba kwa sababu wana sauti ya kuimba, ila kwa upande mwingine skendo zinamtokea mtu kama inavyoweza kumtokea yeyote, haihusiani na Injili.

Kuna tofauti gani ya nyimbo za sasa na zamani?

Nyimbo za zamani waandaaji walikuwa wakiandaa kwa ajili ya kuhubiri tu, ila kwa sasa hivi wanaandika ili watoke kimaisha, wapate umaarufu, magari au nyumba, mtu anatumia akili zake anaangalia watu wanapenda nini kwa wakati huo. Kwa watu wa namna hiyo, anawataka waimbaji watulie na kuutafuta utukufu wa Mungu katika kumtumikia badala ya kutaka fahari za dunia.

Yuko katika ndoa kwa muda gani?

Amedumu katika ndoa yake yenye watoto wawili kwa miaka 13 sasa na siri kubwa ya kudumu kwake ni kitendo chake cha kuifanyia ‘servisi’ kila mara kwa kuipeleka gereji ambayo ameitafsiri kama maombi yake kwa Yesu!

Ana malengo gani mwaka 2016?

Malengo yake ni kukamilisha albamu mpya itakayokwenda kwa jina la Simama, pia ni kwenda kimataifa zaidi kwa sababu alikuwa akifundisha kwaya mbili London, hivyo anahitaji kuendelea na zoezi hilo.

Ana ujumbe gani kwa waimba Injili?

Uimbaji wa Injili siyo usanii, ukiimba kama msanii utafeli, anawashauri waimbe kama watumishi wanaomtumikia Mungu, waamue na wakusudie kuwa watumishi kwani wasanii huwa wanaburudisha tu mwili wakati mtumishi anahudumia roho za watu, akimaliza kuimba anasababisha roho wa Mungu kukutana na roho za watu.

Nini mafanikio yake?

Mafanikio yake makubwa ni kiroho, mali siyo kipaumbele chake katika kumtumikia Mungu, kwa vile hata fisadi na changudoa nao wana mali, anapenda zaidi mafanikio ya kiroho badala ya kimwili.

Leave A Reply