The House of Favourite Newspapers

Joto la Mapenzi 52

0

ILIPOISHIA:

“Yaani nakumbuka wakati nimelala nilipapaswa na kufumbua macho na kumuona Ambe na kuzungumza naye, toka hapo sikulala mpaka nilipokuja kwako. Sasa jamani kuna ndoto ya mtu kuota akiwa macho?”

“Kwa kweli bado umenipa wakati mgumu wa kujua ilikuwa ndoto au kweli!”

SASA ENDELEA…

Lakini naweza kuamini ilikuwa kweli kutokana na simu iliyopigwa na wewe kusema haikuwa yake. Lakini naamini aliyepiga simu alikuwa shemeji wala si mtu mwingine.”

“Inawezekana eeh!”

“Inawezekana kabisa, kama amesema anajua baba amefariki na kwenye mazishi alikuwepo huoni jambo hili ni kweli si ndoto.”

“Ester hapo ndipo panaponitia shaka, hawezi kuhudhuria mazishi ya baba kwa vile asingeweza kufika bila kukamatwa.”

“Unajua jambo hili tulitakiwa kuliacha kulizungumzia kwa vile hata mimi kuna sehemu linanichanganya sana.”

Wakiwa katikati ya mazungumzo mteja mmoja alisogea na kulipa fedha ndani ya fedha alizolipa kulikuwa na karatasi. Koleta aliichukua ajabu mtu aliyetoa karatasi hiyo baada ya kulipitia na kupewa stakabadhi hakusimama, alitoka nje na bidhaa zake alizonunua.

Koleta alikisoma kile kikaratasi kilichokuwa kimeandikwa:

Mzigo huo upeleke kwenye pikipiki iliyoegeshwa nje ya duka lako.

Kwa haraka alibeba ule mzigo alioagizwa na kutoka nao nje.

Japo nje kulikuwa na pikipiki zaidi ya nne, lakini mtu aliyempa kikaratasi alikuwa kwenye pikipiki iliyokuwa ipo tayari kuondoka. Alimsogelea na kumsalimia.

“Habari yako kaka!”

“Samahani dada huu si muda wa kusalimiana toa ulichoagizwa,” kijana aliyekuwa amevaa kofia ngumu ya pikipiki na miwani alimjibu kwa mkato.

“Aliyekuagiza yupo wapi?” Koleta alimuuliza kwa sauti ya upole.

“Hiyo si juu yangu kujua yupo wapi zaidi ya kumfikishia alipo.”

“Mbona kaka yangu umekuwa mkali, kumbuka mi ni shemeji yako, ipo siku utanionea aibu kwa maneno yako makali.”

“Dada sikuja kupata mahubiri, dunia hii sijawahi kupendwa kwa hiyo hata wewe ukinichukia sitashangaa.”

“Basi samahani kama nimekuudhi ila msalimie sana mwambie nampenda mpaka siku mauti yatakapochukua uhai wangu.”

“Dada mbona si muelewa.”

“Kwa vile aliyekutuma ndiye furaha yangu pumzi yangu, huwezi kuja kama mtoa roho. Mimi ni shemeji yako lazima uwe mstaarabu.”

“Mmh! Ipo kazi, haya nipe huo mzigo niondoke,” ilibidi yule jamaa awe  mpole.

“Naomba ufikishe ujumbe wangu.”

“Sawa umefika.”

Koleta alimpa bahasha kisha yule kijana bila kuongeza neno aliondoka kwa mwendo mkali. Koleta alijikuta njia panda alie au afurahi baada ya fumbo lake kufumbuliwa. Alirudi ndani na kujikuta akibubujikwa machozi kitu kilichomshtua Ester na kutaka kujua nini kimemsibu ndugu yake ambaye kila dakika alikuwa na jambo jipya.

“Vipi tena da’ Koleta?”

“Hata sijielewi.”

“Kwa nini?”

“Kwa nini lakini Ambe ananifanya hivi?”

“Kivipi?”

“Yaani huyo aliyekuja kuchukua mzigo hana kauli nzuri hata kidogo.”

“Kwa nini?”

“Majibu yake tu si mazuri, yaani utafikiri labda Ambe ni adui yangu.”

“Dada nafikiri tuachane na hayo la muhimu kushukuru Ambe kuwa salama hata ndoto yako ni kweli wala si kama ulivyokuwa ukifikiria.”

“Ester siyo ndoto bali kilichotokea kilikuwa kweli.”

“Nilijichanganya, kwa hiyo dada tuombe Mungu aliyokueleza Ambe yatimie.”

“Amina.”

Pamoja na majibu mabaya aliyopewa Koleta alijawa na furaha baada ya ule wasiwasi kupata ukweli kuwa mpenzi wake yupo salama. Alimuombea kwa miungu yote ili alichomuahidi kitimie.

Baada ya kazi alirudi nyumbani akiwa na furaha ya kuonana tena na mpenzi wake Ambe.

 

* * *

Ambe baada ya kuzipata zile fedha walimueleza swahibu wake Mabina.

“Fedha imepatikana tufanye mchakato wa kutafuta passport.”

“Lakini nimepata wazo, lazima ile familia itakuwa na passport, ulitakiwa uzipate ili wewe utafute visa.”

“Basi itanibidi usiku wa leo nimzukie tena kwao.”

“Ndiyo maana yake, tumalize suala hili tuishi maisha mengine.”

“Basi usiku nitakwenda kufanya hivyo.”

“Sikiliza si unataka kumuoa Koleta ndoa ya Kiislamu?”

“Ndiyo.”

“Unajua nimepata wazo ndoa za Kiislamu ni rahisi sana, kwa nini usiku wa leo tusifanye sapraizi?”

“Una maana gani?”

“Usiku wa leo tunamchukua shehe tunakwenda naye, mkeo anasilimishwa mnafunga ndoa kisha tunatoweka ila unawaeleza kutakuwa na safari ya fungate ambayo itakuwa ya dharura ili upange na mpenzi wako mhame mji.”

“Hilo wazo zuri, sasa kuhusu shehe itakuwaje?”

“Hiyo kazi niachie mimi, nitatangulia mjini ukija usiku utakuta kila kitu nimeandaa.”

“Hapo sina neno.”

Baada ya makubaliano Mabina alitangulia mjini kufanya mipango ya shehe na kumwacha Ambe akijipanga kwenda kufunga ndoa na Koleta.

 

* * *

Majira ya saa tatu usiku magari mawili yalipiga honi nje ya nyumba ya mzee Mtoe.

“Samahani mna shida gani?” mlinzi aliwauliza baada ya kufika pembeni ya gari.

“Hebu fungua mlango, ina maana tutakuja hapa bila shida?” Mabina alimjibu mlinzi.

“Sina taarifa ya ujio wenu.”

“Sikiliza ndugu, kutuchelewesha kwako kuingia ndani inaweza kuwa ndiyo siku yako ya mwisho kufanya kazi hapa. Hatupendi kiburi chako kikufukuzishe kazi, tunapenda kijana mwenzetu uendelee na kazi kwa vile sisi ni wageni wa leo tu!” Ambe alimjibu.

“Lakini…”

“Sikiliza au tumwite Koleta atufungulie?” Ambe alimuuliza kwa sauti ya ukali kidogo.

“Basi jamani.”

Mlinzi ilibidi afungue geti na gari kuingia ndani, alishangaa kuona watu sita wakiteremka kwenye gari wakiwa wamevaa kanzu wakielekea ndani. Walipofika mlangoni alibonyeza kengele na mlango ulifunguliwa, aliyefungua alikuwa Ester, alishangaa kuwaona watu wamevaa kanzu na kujiuliza wale akina nani. Macho yake yalishtuka kumuona Mabina alimfahamu ni rafiki wa Ambe.

“Karibuni.”

“Asante, mama yupo?” Mabina aliuliza.

“Amekwenda kulala muda si mrefu.”

“Koleta?”

“Amekwenda chumbani kwake mara moja.”

Wakati huo Koleta alikuwa akirejea sebuleni alishtuka kuwaona watu wamevaa kanzu, jicho lake lilitua kwa Mabina ambaye ndiye alikuwa mbele na Ambe alikuwa nyuma.

“Ha! Shemu, karibu.”

“Asante.”

“Mbona usiku?”

“Kuna ubaya mtu kuja kwao?”

“Hakuna ubaya, karibuni,” wakati huo jicho lake lilitua kwa Ambe aliyekuwa nyuma. Kama mwendawazimu alikurupuka na kwenda kumvamia.

“Wawooo bebiii.”

Je, kilifuatia nini? Usikose kwenye Risasi Mchanganyiko siku ya Jumatano.

Leave A Reply