The House of Favourite Newspapers

Unending Love 61

0

Licha ya mapenzi ya dhati aliyonayo Jafet kwa Anna, kiasi cha kufikia hatua ya kutoa figo yake moja na kumpa msichana huyo, anamlipa mabaya kwa kuamua kuanzisha na uhusiano wa kimapenzi na William.

Jambo hilo linamuumiza sana Jafet, analia na kuomboleza lakini baadaye anamsahau na kuendelea na masomo yake. Baadaye anakutana na msichana mwingine mrembo, Suleikha anayeanzisha naye uhusiano wa kimapenzi.

Upande wa pili, Anna anaanza tena kuumwa na kusafirishwa mpaka jijini Dar es Salaam anakoenda kulazwa Muhimbili.

Akiwa hospitalini hapo, Anna anaanza kuwasumbua wazazi wake akishinikiza Jafet atafutwe mahali popote alipo na kupelekwa hospitalini hapo.

Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…

“Anna, nimekuja na ‘sapraizi’ ambayo naamini utaipenda,” alisema baba yake Anna na kumfanya mkewe aache kumnywesha juisi mgonjwa, wote wakawa na shauku kubwa ya kutaka kujua ni sapraizi gani aliyokuja nayo.

Wakiwa katika hali hiyo, baba Anna alitoa ishara kwa Jafet na Suleikha waliokuwa nje, mlango ukafunguliwa kisha wakaingia, Jafet akiwa mbele huku Suleikha akimfuatia kwa nyuma.

“Whaaat? I can’t believe! Jafet! Am I dreaming?” (Niniiii? Siwezi kuamini! Jafet! Naota?”

“You are not dreaming Anna, its me! (Huoti Anna, ni mimi) alisema Jafet lakini siyo kwa sauti ya uchangamfu kama ilivyokuwa kipindi cha nyuma cha mapenzi yao.

“Meet my best friend, Suleikha! Suleikha, this is Anna! (Kutana na rafiki yangu kipenzi, Suleikha! Suleikha, huyu ni Anna) alisema Jafet kwa sauti ya upole, kwa makusudi Suleikha akapitisha mkono  na kumshika Jafet kimahaba kisha mkono mwingine akampungia Anna huku akivaa tabasamu la uongo usoni kwake.

Kwa alichokifanya Suleikha, bila hata kuuliza Anna alielewa moja kwa moja kwamba walikuwa na uhusiano wa kimapenzi, hasa ukichanganya na ukweli kwamba mara ya mwisho alipokutana na Jafet jirani na Chuo cha Udaktari cha Muhimbili alikokuwa anasoma, walikuwa pamoja na msichana huyo na ndiye aliyekuwa akimshinikiza waondoke haraka.

Anna alibaki ameduwaa kwa sekunde kadhaa, akitamani kila kitu kiwe ndoto lakini haikuwezekana. Ni kweli alifurahi sana kumuona Jafet akiwa mbele yake lakini alijisikia vibaya mno kugundua kwamba tayari Jafet yupo na mwanamke mwingine, tena mrembo zaidi yake na anayeonekana kumpenda kuliko kawaida.

“Mnaweza kutuacha wenyewe kwa muda mfupi?” Anna alisema kwa sauti iliyoonesha dhahiri kujawa na huzuni, akawageukia baba na mama yake ambao walitazama kisha wakatingisha vichwa kama ishara ya kukubaliana na alichokiomba binti yao. Wakatoka na kuwaacha Jafet, Suleikha na Anna.

“Dada samahani sana naomba nizungumze na Jafet kwa muda mfupi, nakuomba utusubiri nje,” alisema Anna huku akijilaza vizuri pale kitandani alipokuwa amelazwa, machozi yakianza kumlengalenga. Suleikha alimkazia macho Anna kisha akamgeukia Jafet kama anayesubiri kusikia atamwambia nini.

Jafet akampa ishara ya kutekeleza alichoambiwa na Anna lakini hakuwa mwepesi kukubaliana na alichoambiwa.

“Kwani mna mazungumzo gani ambayo mimi sipaswi kuyasikia?”

“Suleikha nakuomba, unajua Anna anaumwa sidhani kama itakuwa busara kuanza kushindana naye,” alisema Jafet kwa upole, Suleikha akasusa na kutoka akionesha kuwa na hasira. Alipofunga mlango Jafet alishusha pumzi ndefu na kumsogelea Anna pale kitandani.

“Naomba ukae hapa karibu yangu,” alisema msichana huyo, safari hii machozi yakimtoka kupitia kona za macho yake na kutiririkia mpaka kwenye shuka alilokuwa amelalia. Jafet akafanya kama alivyoambiwa.

“Nini kinakuliza tena Anna?”

“Roho inaniuma Jafet, najisikia vibaya sana, natamani siku zirudi nyuma nirekebishe makosa niliyoyafanya,” alisema Anna huku akiendelea kulia kwa kwikwi.

“Huna haja ya kulia Anna, si unajua unaumwa? Utajiongezea matatizo,” alisema Jafet kwa sauti ya upole huku akimpigapiga Anna begani kama ishara ya kumbembeleza, jambo lililomfariji sana msichana huyo.

“Baba amenifuata chuoni na kuniambia unahitaji kuonana na mimi.”

“Ni kweli Jafet lakini sikutaka uje na mtu yeyote, nilitaka uje peke yako.”

“Nisamehe kwa hilo lakini Suleikha ni mpenzi wangu na tuna malengo mengi pamoja, sikuona kama kuna ubaya wowote kuja naye, kwanza ndiyo imekuwa vizuri kwa sababu mmefahamiana,” alisema Jafet kwa sauti ya upole lakini iliyoonesha kwamba anamaanisha kile alichokisema.

Anna akaanza kumueleza kila kitu kilichotokea mpaka akaletwa Muhimbili na kulazwa.

“Kwani umeletwa lini hapa?”

“Tumekuja jana kwa ndege.”

“Kwani siku ile tulipokutana ulikuwa unatoka wapi? Na mbona ulikuwa unaonesha kubadilika sana?” alihoji Jafet, swali ambalo lilienda kuutonesha moyo wa Anna, akaanza tena kulia.

“Naomba unisamehe Jafet, kwa kuwa leo umekuja nataka nikueleze kila kitu kilichotokea, sioni sababu ya kukuficha chochote,” alisema Anna huku akijifuta machozi na kukaa vizuri pale kitandani.

Akaanza kueleza upya kila kilichotokea, kuanzia jinsi wazazi wake walivyomtafutia chuo nchini Marekani na kumuondoa bila ridhaa yake.

“Lakini hayo si ulishaniambia siku ile?”

“Ndiyo nilikwambia lakini nimeamua kurudia kwa sababu nahisi hukuniamini na isitoshe sikukueleza kila kitu,” alisema Anna, Jafet akatingisha kichwa kama ishara ya kumtaka aendelee kueleza.

Akaendelea kumueleza kila kitu kilichofuatia, jinsi alivyokutana na William na kuanzisha naye urafiki wa kawaida ambao baadaye ulibadilika na kuwa uhusiano wa kimapenzi. Akaendelea kueleza jinsi alivyojitahidi kukwepa suala la kukutana kimwili na kijana huyo mpaka siku watakayofunga ndoa.

Katika hali ambayo hata Anna mwenyewe hakuitegemea, alishangaa kumuona Jafet akijiinamia na kuanza kutokwa na machozi.

“Kwa nini uliamua kunitesa kiasi hicho Anna? Kwa sababu ya umaskini wangu? Nimejitoa sadaka mambo mangapi kwa ajili yako? Unakumbuka kwamba nilitakiwa kwenda kusomea upadri lakini nikakataa kwa sababu yako? Nimekufanyia mambo mangapi mazuri mpaka kustahili kufanyiwa ulichonifanyia?” alihoji Jafet huku akilia.

Anna naye akaanza kuangua kilio kwani ni kweli alikuwa amemkosea sana Jafet, wote wakawa wanalia kama wamepokea taarifa za msiba. Hakukuwa na wa kumbembeleza mwenzake tena.

“Nipo chini ya miguu yako Jafet, naomba unisamehe, bado nakupenda mwenzio.”

“Muongo wewe, wala hunipendi, najua unazungumza hayo kwa sababu unaumwa, mbona siku zote ulipokuwa mzima hukuwa na habari na mimi?”

“Nilipoteza mawasiliano yako Jafet, nilikuwa natamani japo nikupigie simu niisikie sauti yako lakini haikuwezekana, nilikuwa natamani japo nikutumie barua au kadi lakini pia haikuwezekana,” alisema msichana huyo na kuendelea kumueleza Jafet kila kilichoendelea mpaka muda huo walipokuwa ndani ya wodi hiyo.

“Kwa hiyo Anna ulifikia hata hatua ya kumbebea mwanaume mwingine ujauzito?”

“Alikuwa ananilewesha kisha ananiingilia kimwili bila ridhaa yangu.”

“Muongo wewe, kama ni hivyo mbona hukuwahi kuripoti sehemu yoyote?” alihoji Jafet, Anna akakosa cha kujibu zaidi ya kujiinamia.

“Halafu ulikuwa unakubali vipi kunywa pombe wakati unajua vizuri kwamba una matatizo? Unaona kilichotokea sasa?”

“Huu siyo muda wa kulaumiana Jafet, nahitaji msaada wako.”

“Msaada gani tena Anna?”

“Naomba turudiane tuishi kama zamani, sijawahi kupenda kama ninavyokupenda Jafet.”

“Its too late Anna, im now dating Suleikha!” (Umechelewa sana Anna, tayari nipo kwenye uhusiano wa kimapenzi na Suleikha) alisema Jafet, kauli iliyosababisha Anna aanze kuangua kilio kwa sauti kubwa, kiasi cha kuwashtua wazazi wake waliokuwa nje, ikabidi waingie wodini kutaka kujua kulikoni.

Je, nini kitafuatia? Usikose Jumatano kwenye gazeti la Risasi Mchanganyiko.

Leave A Reply