The House of Favourite Newspapers

JPM Ampa Mkurugenzi NIDA Maagizo Mazito Kuhusu Vitambulisho – Video


RAIS John Magufuli amemuagiza Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) kufika mkoani Morogoro leo na ikiwezekana akae  humo hata siku tatu ili kushughulikia tatizo la watu wengi kukosa vitambulisho vya taifa ambapo mkoa huo una ofisi moja tu ya NIDA.

 

“Nimemtaka Mkurugenzi Mkuu NIDA afike hapa Morogoro ashughulikie hii changamoto ya vitambulisho na nataka huduma hii iende kila wilaya, haiwezekani watu wasafiri kutoka wilayani kuja mjini, basi  muwape kabisa nauli na hela ya gesti,” alisema Magufuli akizungumza na wananchi katika kituo cha mabasi cha Msamvu mjini Morogoro leo ambapo alitaka suala hilo litazamwe na kushughulikiwa ipasavyo nchini nzima.

 

Aliongeza: “Watu wanataka kusajili laini zao za simu na mambo mengine lakini zoezi la vitambulisho linacheleweshwa na watu wachache na polepole sana… Mkurugenzi Mkuu wa NIDA nitahitaji unipe na tathmini ya zoezi lote nchi nzima.”

 

Aidha,  amesisitiza kuwa katika kipindi chake cha uongozi hatapanga bei ya mkulima kuuza mazao yake.

 

“Wengine wanalalamikia bei ya mahindi kupanda, nataka wakulima washangilie kama bei ya mahindi imepanda, biashara hii lazima iwe huru, bei ya mahindi itajipanga yenyewe, wakati wa kuwapangia bei wakulima kwenye mazao yao umekwisha,” amesema.

Comments are closed.