RAIS John Magufuli ameeleza kushangazwa kwake na baadhi ya watumishi wa serikali ambao bado wana ‘damu’ ya rushwa kwenye mioyo yao licha ya kuona mifano ya watu wengi waliokamatwa na kufikishwa mahakamani kwa makosa hayo lakini hawajifunzi.
Magufuli amesema hayo baada ya kumwapisha Valentino Mlowola kuwa Balozi wa Tanzania nchini Cuba na kupokea taarifa ya mwaka ya utendaji wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wake, CP Diwani Athuman, leo Alhamisi, Machi 28, 2019, Ikulu, jijini Dar es Salaam.
Katika kushangazwa kwake, alitolea mfano wa watumishi waliotaka ‘kupiga’ pesa za serikali kwa ajili ya kwenda nje kubadili rangi ya ndege ya rais ili itumiwe na Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL).
“Nilipokuwa katika sherehe pale Uwanja wa Ndege, niliagiza ndege ya Rais ipelekwe ATCL, itumike kubeba abiria, nikaambiwa kazi ya kuchora Twiga na Nembo ya Air Tanzania haiwezi kufanyika nchini, nikatajiwa nchi tatu ndizo zinaweza kuchora, yaani hapa nchini hakuna wa kuchora.
“Nikaambiwa gharama za kuchora Twiga na Nembo ya Air Tanzania ni shlingi milioni 60, na malipo ya awali kuhusu kazi hiyo yameshalipwa, na inaondoka na wasindikizaji. Nikasema ndege ikiondoka na nafasi zao wajue zimeondoka, ndege imebaki na kazi imefanyika nchini kwa shilingi milioni tano.
Rais alitoa mfano mwingine ambapo alipata malalamiko dhidi ya viongozi wa CCM waliokuwa wanataka rushwa wilayani Ilala jijini Dar es Salaam ambao aliagiza wawekewe mitego na wakakamtwa na Takukuru.
Alielezea pia tukio la ofisa wa ngazi za juu wa Takukuru ambaye amewauzia viwanja hewa wafanyakazi wenzake lakini hajapelekwa mahakamani.
“Najiuliza, Takukuru ni kwa ajili ya watu wengine na sio kwa wao pia? Nataka hili mlishughulikie,” alisema rais akitaka suala hilo lishughulikiwe.
Rais alitoa wito kwa wateule wake kuanza kazi mara moja bila kupoteza muda. Kauli yake hiyo ilikuwa imemlenga Balozi wa Tanzania nchini Zambia ambaye pamoja na kuteuliwa siku kadhaa zilizopita bado anaonekana nchini badala ya kwenda kwenye kituo chake cha kazi mara moja.
Comments are closed.