The House of Favourite Newspapers

JPM: Nafahamu Zaka Zimepungua Makanisani, Zilikuwa za Mafisadi – Video

RAIS Dkt. John Pmbe Magufuli ‘ametupa jiwe gizani’ na kufunguka kuwa kwa sasa Zaka katika makanisa zimepungua kwa sababu fedha zilizokuwa zikitolewa na waumini nyingine zilikuwa za mafisadi na wala rushwa ambao kwa sasa wamebanwa na hawawezi tena kujipatia pesa kwa njia hizo za udanganyifu.

 

Rais ameyasema hayo leo wakati akizindua Ujenzi wa Mradi wa Rada nne za kuongozea ndege katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam ikiwa ni siku chache tangu maaskofu watoe waraka wakilaani kuhusu hali ya amani hapa nchini.

 

“Wako watu waliokuwa wamezoea fedha za bure za kuwaibia masikini hao ndio wanapiga kelele sana. Ninafahamu hata makanisani zaka zimepungua sababu fedha zingine zilikuwa zinatolewa na mafisadi. Yalipotokea mauaji Kibiti wala sikuona waraka, ingawa hili sipendi kulizungumzia kwasababu najua hakuna kitakachofanyika.

 

“Tanzania inaenda vizuri sana Watanzania watembee kifua mbele kwani nchi inakuwa kwa kasi, Ilikuwa ni aibu kwa nchi kubwa kama Tanzania kuwa haina ndege ya Serikali. Tulikuwa hatuna ndege. Ndege ndio heshima ya nchi. Tumeingia madarakani nikasema lazima tuwe na ndege. Wakasema pesa atapata wapi? Nikasema pesa ziko kwa Mafisadi na watazitema hata ikibidi kwa kutapika. 

 

“Miradi yote tunayotekeleza, ununuzi madawa, ndege zinazokuja yote hii ni yenu, sisi viongozi jukumu letu ni kusimamia utekelezaji wa miradi hii, Serikali ipo haijalala na haitalala, ” alisema Magufuli.

 

Comments are closed.