The House of Favourite Newspapers

Juma Abdul… Gari limewaka Yanga

KAMWE hauwezi kuwataja mabeki bora wa pembeni, namba mbili bila ya kulitaja jina la Juma Abdul anayeichezea Yanga ambaye alijiunga nayo msimu wa 2011/ 2012 akitokea Mtibwa Sugar ya Manungu, Morogoro.

 

Wakati Abdul anajiunga na Yanga alikutana na upinzani mkubwa kutoka kwa aliyekuwa nahodha wa timu hiyo, Shadrack Nsajigwa na baadaye Godfrey Taita aliokuwa anacheza nao nafasi moja.

 

Awali, Abdul wakati anajiunga na Yanga hakuwa anapata nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza, lakini baadaye akawa anapata baada ya kuaminika na waliokuwa makocha wa timu hiyo Mholanzi, Ernie Brandts, Sam Timbe, Tom Saintifiet na Hans Pluijm.

 

Baada ya kuaminika na kupata nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza, beki huyo akapewa unahodha kama nahodha msaidizi msimu wa 2017/ 2018, cheo ambacho anaendelea nacho hivi sasa.

 

Beki huyo kwenye msimu huu ameonekana kurejea kwa kasi kubwa akicheza michezo mitatu mfululizo ya Ligi Kuu Bara tangu arejee ambayo yote imepata ushindi walipocheza na Coastal Union, Mbao FC na wikiendi iliyopita wakawafunga Ndanda FC.

 

Abdul amerejea uwanjani kwenye msimu huu akitokea kwenye majeraha ya enka yaliyomuweka nje ya uwanja msimu mzima uliopita kabla ya aliyekuwa kocha wa timu hiyo Mkongomani, Mwinyi Zahera kumuamini Paul Godfrey ‘Boxer’ kwa kumpa nafasi ya kucheza na kuwa tegemeo katika timu ambaye hivi sasa yupo akiuguza majeraha ya goti.

 

Yafuatayo chini ni mahojiano maalum kati ya Abdul na Championi Jumatano akizungumzia safari yake ya soka, pia sababu za yeye kurejea katika kiwango chake cha awali.

 

Nini tatizo hadi ukaukosa msima mzima wa ligi?

“Hakuna kingine zaidi ya majeraha ya enka niliyokuwa nayapata mara kwa mara, sikuwa napenda kukaa nje ya uwanja muda mrefu lakini majeraha hayo ndiyo yalisababisha yatokee hayo.

“Niliamua kupumzika kucheza soka huku nikiendelea na matibabu ambayo leo hii unaniona nimerejea uwanjani nikiwa fiti kwa asilimia mia na ndiyo kitu nilichokuwa nakitaka.

 

“Nilihofia kucheza nikiwa bado sijapona kwa sababu kama ningekubali kucheza nikiwa bado sijapona, basi ingekuwa rahisi kwangu kujitonesha na sikutaka hali hiyo initokee, nashukuru hivi sasa nimepona.

“Kama ningelazimisha kucheza nikiwa bado sijapona vizuri, basi ningelazimika kukaa muda kama ingetokea nimejitonyesha jeraha langu hilo lililoniweka nje ya uwanja muda.

 

GARI NDIYO LIMEWEKA SASA HIVI?

“Niwatoe wasiwasi mashabiki wa Yanga kwa kuwaambia kuwa hivi sasa gari ndiyo kwanza limeweka, watarajie makubwa kutoka kwangu kwani hawataniona tena nikipata majeraha kwa sababu mashabiki bado wana hofu na mimi juu ya majeraha yangu.

 

“Ninachokifanya hivi sasa ni kurejesha kiwango changu kile wanachokijua cha kupiga krosi safi kwa washambuliaji wetu wakati nikiwa na mpira, nafikiri kila mtu ananifahamu vizuri, washindwe wenyewe kufunga.

 

NAFASI YAKO KWENYE TIMU IPOJE?

“Namuachia kocha ndiye atakayeamua, lakini mimi ninaamini kwa uwezo wangu niliokuwa nao sioni wa kuniweka benchi, kwani nina sifa zote za kucheza katika kikosi cha kwanza katika timu.

 

“Hivi sasa nilichobakisha ni kurejesha fitinesi ya kupanda kwenda kushambulia kwa maana ya kupiga krosi na kushuka kulinda wakati ninapopoteza mpira.

 

“Kama unavyofahamu mchezaji anapokaa nje ya uwanja muda mrefu anapoteza mechi fitinesi, lakini nashukuru hivi sasa tayari nimeanza kuirejesha tangu nilipoanza kucheza mchezo wa kwanza wa ligi na Coastal Union.

 

UNAMZUNGUMZIAJE BOXER?

“Kiukweli ni bonge la beki, ni kati ya wachezaji wanaokuja kwa kasi kubwa Yanga, anahitaji sapoti yetu wakongwe katika kumtengeneza ili awe tegemeo na tishio katika timu.

 

“Nikiwa nje ya uwanja nikiuguza majeraha yangu kiukweli aliweza kuziba vema pengo langu kutokana na uwezo wa kukaba na kuanzisha mashambulizi kwenye goli la wapinzani, anastahili pongezi nyingi na ninaamini atakuwa tegemeo siku za usoni Yanga na timu ya taifa.

 

VIPI NAFASI YAKO TIMU YA TAIFA

“Mimi ni Mtanzania nina haki ya kuichezea, kuipigania nchi yangu kwa maana ya kuichezea Stars, ipo siku nitarejea tena, kikubwa ninatakiwa kuendelea kuipambania timu yangu kwa kuonyesha kiwango kikubwa ili niitwe tena kuichezea Stars.

 

“Ninaamini linawezekana katika hilo, uzuri kocha wa Stars anaifuatilia ligi hivyo ipo siku ataniona na kuniita na hilo linawezekana kwangu ninaiona nafasi yangu katika timu.

 

NINI KIMESABABISHA MFANYE VIBAYA KIMATAIFA?

“Hatukufanya vibaya, kama tungekuwa tumefanya vibaya basi tusingefika hatua ya mtoano ya Kombe la Shirikisho, kama wachezaji tulijitahidi kupambana kadiri ya uwezo wetu lakini bahati haikuwa yetu tukatolewa hatua hiyo ambayo siyo mbaya licha ya malengo makubwa yalikuwa ni kufika makundi.

 

“Kutolewa kwetu kumetufanya tujifunze mengi kati ya hayo ni kutumia vema uwanja wa nyumbani, makosa tuliyoyafanya ni kukubali kufungwa nyumbani tulipocheza na Pyramids FC ya Misri kwa makosa ya kizembe na kikubwa kukosa umakini.

 

“Ninaamini kama tungekuwa makini kwa kucheza kwa kujilinda ndani ya wakati mmoja tukilinda goli letu, basi tusingefungwa hapa nyumbani mabao 2-1, ninaamini tungekuwa na morali ya juu kupata ushindi ugenini kwa kuwafunga,” anasema Abdul.

WILBERT MOLANDI, Dar es Salaam

Comments are closed.