The House of Favourite Newspapers

Juuko Apigwa Chini Simba, Mkude Yamkuta Makubwa

Juuko Murshid.

BEKI wa kati wa Simba, Juuko Murshid, juzi Jumatatu alizuiwa kufanya mazoezi na kikosi hicho kwa kile kilichoelezwa ni utovu wa nidhamu.

 

Juuko raia wa Uganda, alizuiwa na kocha wa kikosi hicho, Mbelgiji, Patrick Aussems baada ya kuchelewa kuungana na wenzake mara baada ya kumaliza majukumu ya timu ya taifa, mwishoni mwa mwezi uliopita.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya Simba, beki huyo hakutoa taarifa juu ya kuchelewa kwake kitendo ambacho kilimkera kocha Aussems na kuamua kumtupa nje ya kikosi hicho kinachojiandaa kucheza na Nkana FC ukiwa ni mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya kwanza.

 

“Juuko alipotaka kwenda mazoezini kuungana na wenzake kocha akamzuia kutokana na kutotoa taarifa za kuchelewa kwake,” alisema mtoa taarifa.

 

Kiungo wa Simba, Jonas Mkude.

Championi ambalo juzi lilifika mazoezini hapo, likazungumza na Aussem ambapo alisema: “Juuko nimemwambia kwanza akae pembeni mpaka hapo ambapo nitamruhusu kwa sababu amechelewa kuungana na wenzake bila taarifa rasmi.”

 

Wakati Juuko akikumbana na janga hilo, kiungo wa kikosi hicho, Jonas Mkude, yeye aliponea chupuchupu baada ya kuomba msamaha na kukubaliwa.

 

Mkude naye alichelewa kuungana na wenzake mazoezini wakati timu hiyo iliporejea Dar ikitokea Eswatini kucheza na Mbabane Swallows kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya awali, alimuwahi kocha na kumuomba msamaha.

 

“Mkude aliomba msamaha ambapo kocha alimtaka awaombe wachezaji wake pia, baada ya kufanya hivyo akakubaliwa kufanya mazoezi.

 

“Yeye alichelewa kuungana na wenzake mara tu waliporejea walipotoka kucheza na Mbabane, sasa ili kuimarisha nidhamu, kocha anataka kila mchezaji kufuata kwa wakati kile anachoambiwa,” kilimaliza chanzo. Simba inacheza na Nkana, Jumamosi mjini Kitwe, Zambia.

Stori Ibrahim Mussa, Championi Jumatano

LA LIGA Uso kwa Uso na Wachambuzi Na Wahariri Wa Michezo

Comments are closed.