The House of Favourite Newspapers

Juuko atangaza makombe mawili Simba

Na Omary Mdose/CHAMPIONI/GPL
BEKI wa kati ya Simba, Juuko Murshid raia wa Uganda, anaamini kwamba kikosi chao hicho msimu huu kina uwezo wa kuchukua mataji mawili katika ardhi ya Tanzania na hakuna timu itakayowazuia kufanya hivyo.
Juuko ambaye hakuichezea Simba tangu Novemba, mwaka jana, kwa mara ya kwanza alionekana kwenye mchezo wa hatua ya robo fainali ya Kombe la FA walipoibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Madini FC ya Arusha ambapo kauli yake hiyo imeelezwa ni kama anataka kuikomoa Yanga.
Mganda huyo ambaye aliondoka Simba na kujiunga na timu yake ya taifa iliyoshiriki michuano ya Kombe la Mataifa Afrika, mapema mwaka huu, amesema Simba ina kila sababu ya kuwa bingwa wa Kombe la FA na Ligi Kuu Bara kutokana na ubora wa kikosi chao na jinsi hali ya mambo ilivyo.
Simba kwa sasa inaongoza msimamo wa ligi kuu ikiwa na pointi 55 ikifuatiwa na Yanga yenye pointi 53. Timu hizo zote zimebakiwa na michezo sita kuhitimisha msimu huu ulioanza kutimua vumbi Agosti, mwaka jana.
“Tumefuzu kucheza nusu fainali ya Kombe la FA, lakini pia tunaongoza ligi kwa tofauti ya pointi mbili dhidi ya wapinzani wetu Yanga huku zikiwa zimesalia mechi sita tu kumaliza msimu huu.
“Mpaka sasa sijaona timu ambayo inaweza kutuzuia kufanikisha malengo yetu ya kuchukua makombe hayo mawili kwa jinsi tulivyojipanga.
“Sikuwa na timu kwa muda mrefu, lakini nimerejea kwa nia moja tu, kuipigania timu yangu na kufikia malengo ambayo kila mmoja wetu hapa kikosini anayahitaji,” alisema Juuko.

Comments are closed.