The House of Favourite Newspapers

Kada NCCR-Mageuzi Aliyepotea Aokotwa Porini Akiwa Taabani, Hajitambua

0
Mkuu wa Idara ya Uenezi na Mahusiano ya Umma ya NCCR-Mageuzi, Edward Simbeye.

MWENYEKITI wa Jumuiya ya Vijana ya Chama cha NCCR-Mageuzi, Jovine Clinton, aliyepotea tangu tarehe 24 Januari 2023, amepatikana akiwa hajitambui katika pori lililoko nje ya Jiji la Dar es Salaam.

Taarifa hiyo imetolewa Alhamisi Feburuari 2, 2022 na Mkuu wa Idara ya Uenezi na Mahusiano ya Umma ya NCCR-Mageuzi, Edward Simbeye, akizungumza na waandishi wa habari na kusema Jovine ameonekana usiku wa kuamkia tarehe 31 Januari mwaka huu.

Simbeye amedai kuwa Jovine aliokotwa na wananchi akiwa porini hajitambui, ambapo walitoa taarifa Polisi na kwamba hivi sasa anapatiwa matibabu na hali yake kiafya inaendelea kuimarika.

“Leo naomba nitoe taarifa ya awali kwamba Jovine aliokotwa porini, ndani ya msitu mnene na wasamaria wema nje ya Mkoa wa Dar es Salaam akiwa kwenye hali mbaya ya kutojitambua na waliwataarifu Polisi kisha Jeshi la Polisi likawajibika kwa mujibu wa majukumu yao,” amesema Simbeye.

Simbeye amesema NCCR-Mageuzi inalitaka Jeshi la Polisi kuendelea na uchunguzi wa kina ili kubaini waliohusika na tukio hilo kwa ajili ya kuchukua hatua za kisheria.

Kupatikana kwa Jovine kumekuja ikiwa zimepita siku tatu tangu Jeshi la Polisi lionyeshe kusudio la kuanza kufanya uchunguzi wa kisayansi dhidi ya mawasiliano yake, ili kubaini watu aliowasiliana nao kabla ya kupotea.

EXCLUSIVE: KUMBE SCORPION ALIYEMTOBOA MACHO SAID SIYE ALIYEFUNGWA? SAMJET ATOKA GEREZANI, AFUNGUKA

Leave A Reply