The House of Favourite Newspapers

Kamusoko Ashusha Presha Yanga

0
Thabani Kamusoko.

KIUNGO mkabaji wa Yanga, Mzimbabwe, Thabani Kamusoko, ameshusha presha ya timu hiyo, baada ya kupona majeraha yake ya nyonga huku akitarajia kuwepo kwenye kikosi cha timu hiyo kitakachoivaa Ndanda FC ya Mtwara.

Mzimbabwe huyo alikosa mchezo dhidi ya Majimaji uliomalizika kwa sare ya bao 1-1 kwenye Uwanja wa Majimaji, Songea baada ya kujitonesha katika mchezo uliopita dhidi ya Njombe Mji.

Yanga na Ndanda zinatarajiwa kuvaana Jumamosi hii kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam katika mechi ya Ligi Kuu Bara.

Daktari Mkuu wa Yanga, Edward Bavu amesema kiungo huyo amepata nafuu baada ya kumpatia matibabu ya haraka ili kuhakikisha anarejea uwanjani mapema.

Bavu alisema kiungo huyo tayari ameanza mazoezi mepesi ya binafsi na kukimbia mbio fupi na ndefu huku akiruka koni chini ya kocha wa viungo, Mzimbabwe, Noel Mwandila.

“Ninaamini mechi ijayo dhidi ya Ndanda ataweza kucheza kama kocha akihitaji kumtumia katika mchezo huo ambao ni muhimu kwetu tutakapokuwa kwenye uwanja wetu wa nyumbani,” alisema Bavu.

Wilbert Molandi, Dar es Salaam

Leave A Reply