The House of Favourite Newspapers

Kamusoko, Chirwa Warudi Yanga SC

Wachezaji wa timu ya Yanga.

NYOTA wa Yanga, Obrey Chirwa na Thabani Kamusoko wakiwa na wachezaji wenzao jana Ijumaa waliingia kambini kujiandaa na mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Township Rollers ya Botswana.

 

Awali Kamusoko hakuwa kikosini Yanga kutokana na kuuguza jeraha la goti huku Chirwa akiwa anasumbuliwa na misuli.

 

Yanga imeingia kambini ikiwa ni siku moja tu baada ya kurejea Dar es Salaam kutoka Mtwara ilipocheza na Ndanda FC mechi ya Ligi Kuu Bara na kushinda mabao 2-1.

 

Yanga Jumanne ijayo itacheza na Township Rollers kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kabla ya kurudiana wiki mbili zijazo huko Botswana.

 

Akizungumza na Championi Jumamosi, Meneja wa Yanga, Hafidh Saleh alisema kikosi hicho kitaweka kambi nzito ya siku nne maalum kwa lengo la kupata ushindi kwenye uwanja wa nyumbani.

 

Saleh alisema, timu hiyo itaingia kambini baada ya mazoezi ya jana jioni yaliyotarajiwa kufanyika kwenye Uwanja wa Chuo cha Polisi Kurasini, Dar.

 

“Tumeingia kambini kwa ajili ya kuanza maandalizi ya mchezo ujao wa Ligi ya Mabingwa Afrika, ni jambo jema tunaanza kambi tukiwa wachezaji baadhi waliotoka kwenye majeraha.

 

“Wachezaji hao ni Juma Mahadhi aliyekuwa anaumwa homa, Kamusoko, Chirwa wenye maumivu ya misuli na Ngoma (Donald) aliyekuwa anaumwa nyonga.

 

“Wachezaji hao wote wataingia kambini kwa ajili ya mchezo huo ambao tunahitaji ushindi mkubwa hapa nyumbani kabla ya kwenda kurudiana kwao Botswana,” alisema Saleh.

Comments are closed.