The House of Favourite Newspapers

Kamusoko: Naanza na Waswana

Mzimbabwe, Thabani Kamusoko, amethibitisha kuanza kucheza mechi yake ya kwanza dhidi ya Township Rollers ya nchini Botswana.

Yanga itacheza na Waswana hao kesho Jumanne katika mechi ya raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika itakayochezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

 

Mzimbabwe huyo anarejea uwanjani baada ya majeraha yake ya goti yaliyomuweka nje muda mrefu na mechi hiyo dhidi ya Waswana itakuwa ya kwanza kwake kuonekana dimbani baada ya kupita miezi kadhaa.

Kamusoko alitumia akaunti yake ya mtandao wa kijamii kutamka kuwa atakuwa fiti kucheza mchezo dhidi ya Waswana hao.

 

Alituma meseji hiyo akimshukuru mchezaji mwenzake wa Yanga, kipa Ramadhani Kabwili kwa kumtakia heri katika siku yake ya kuzaliwa.

“Asante sana mdogo wangu Kabwili kwa kunitakia heri yangu ya kuzaliwa, na tutakuwa wote tarehe sita Mungu akijalia tutakapocheza mechi na Township Rollers,” aliandika Kamusoko.

 

Huo ni ujumbe tosha kwa Wanayanga kuwa kiungo wao kipenzi amepona na yupo fiti kucheza mechi na Waswana na Ligi Kuu Bara baada ya kukaa nje muda mrefu.

Kurejea kwa kiungo huyo kutapunguza idadi ya majeruhi katika kikosi hicho baada ya yeye kupona pamoja na Obrey Chirwa ambaye atakuwepo kwenye orodha ya kikosi kitakachoivaa Township huku Ngoma naye akirejea mdogomdogo.

 

Aidha, daktari wa timu wa timu hiyo, Edward Bavu alithibitisha kupona kwa Kamusoko huku akisema: “Kamusoko yupo fiti kwa asilimia 100 kucheza mechi, hivyo ni maamuzi ya kocha kumtumia au kutomtumia.”

Wilbert Molandi, Dar es Salaam.

 

VIDEO: ‘MIMI Ndio Bingwa Subirini Muone Wanazi wa Yanga’

Comments are closed.