The House of Favourite Newspapers

KANYASU AISHAURI NMB KUSAIDIA UTALII KUSINI 

Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar, Mahmoud Thabit Kombo akionesha kadi yake ya benki ya NMB alipotembelea banda la benki ya NMB. 
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu (kulia) akimsikiliza Mkuu wa malipo na akaunti wa benki ya NMB, Michael Mungure. 
Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar ,Mahmoud Thabit Kombo (katikati) akizungumza jambo. Kushoto ni Meneja wa benki hiyo kanda ya Kaskazini,Aikansia Muro na kulia ni Meneja wa tawi la Arusha Market, Hermelinda Kasihwaki.

 

 

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu amepongeza juhudi za taasisi za fedha nchini  kuona umuhimu wa kuwapa mikopo wajasiriamali kwenye sekta  utalii ili kuiwezesha sekta hiyo kutoa mchango muhimu kiuchumi.

 

 

Akizungumza katika banda la benki ya NMB kwenye maonesho ya wadau wa utalii yaliyoandaliwa na kampuni ya Karibu-Kili Fair ambayo benki hiyo ni mdhamini amesema uwepo wa taasisi za fedha utasaidia wadau wa utalii kupata mikopo kwa urahisi zaidi.

 

 

“Serikali inaunga mkono juhudi za NMB, mnafahamu namna ambavyo tumekua tukifanya kazi pamoja na umuhimu wa benki yenu katika kusukuma juhudi za wananchi kujiletea maendeleo, nitoe wito sasa mjielekeze kuwasaidia ukanda  wa kitalii katika mikoa ya Kusini ambako kuna fursa kubwa,”alisema Kanyasu.

 

 

Alisema serikali imedhamiria kufungua eneo la ukanda wa Kusini na imewaleta Makatibu Tawala wa mikoa hiyo kuhudhuria maonesho makubwa katika nchi za Afrika Mashariki ili kupata maarifa watakayoyatumia kutekeleza mradi wa Regrow unaofadhiliwa na Benki ya Dunia kwenye mikoa hiyo.

 

 

Katibu Tawala wa mkoa wa Songwe, David Kafulila alisema Rais John Magufuli ametoa maagizo ya ukanda wa Kusini kufunguliwa na wao kama watendaji wa serikali wanaamini benki ya NMB itasaidia kuhakikisha wafanyabiashara wanapata fursa ya mikopo.

 

 

Alisema wataweka mikakati ya kuhakikisha mikoa ya ukanda wa Kusini ambayo ni Ruvuma, Songwe, Njombe, Iringa, Mbeya, Katavi inainuka kwenye utalii ifanane na mikoa ya ukanda wa Kaskazini ambako biashara hiyo imestawi kwa wingi.

 

 

Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Wateja Wakubwa wa NMB, Filbert Mponzi alisema benki hiyo imetenga Sh 500 bilioni kwa ajili ya wajasiriamali wakiwemo walio katika sekta ya utalii eneo ambalo halijachangamkia sana mikopo kwaajili ya kuongeza uwekezaji wao.

 

 

Alisema wamejipanga kushirikiana na serikali katika kuinua sekta ya utalii ukanda wa Kusini baada ya kubainika vipo vivutio vingi maeneo hayo lakini baada ya msukumo wa serikali ya wamu ya tano kuongeza juhudi litakua ni eneo la kimkakati kwao.

 

 

Sisi kama benki tumedhamini maonesho ya utalii ya Karibu Kili Fair lengo likiwa ni kusaidia serikali kukuza sekta ya utalii ambayo imekuwa na mchango mkubwa katika pato la taifa na pia kukuza kipato cha wananchi wanaojikita kwenye biashara za kitalii.

 

 

Kwa sasa tumeanza kutoa mikopo ya fedha kwa ajili ya magari ya kubeba watalii ili kuweza kuongeza uwezo wa kuhudumia watalii kwa wingi zaidi.

 

 

Kwa Upande wake Meneja Wa Kanda ya Kaskzani benki ya kizalendo ya NMB, Aikansia Muro  alisema benki hiyo imeweza Kuunganishwa Na mfumo wa Malipo Wa Serikali ili kuweza kuwarahishia watoa huduma za kitalii kupata huduma kwa urahisi na kuiwezesha Serikali kupata mapato yake kwa uhakika zaidi

Comments are closed.