KASHFA! POLISI ASKARI ADAIWA KUSHAMBULIA RAIA KWA PANGA MTAANI

NDANI ya siku chache, Jeshi la Polisi Tanzania limekumbwa na kashfa mbili ambazo ni pamoja na askari wake kudaiwa kushambulia raia kwa panga na raia kudai kukatwa nyeti akiwa kituo cha polisi, Uwazi lina ripoti ya matukio hayo.

 

ALIYEKATWA NYETI

Wiki iliyopita, gazeti hili liliripoti habari ya kijana Wema Boniface Mugendi (28), raia wa Kitongoji cha Kukiganana Kijiji cha Isaba, Kata ya Buruma, Tarafa ya Makongoro Wilaya ya Butiama, Mara akilalamika kukatwa nyeti kituoni, sakata ambalo limeibua mapya juu ya uwezekano wa kupata mtoto.

 

KASHFA MPYA

Pamoja na jeshi hilo kukabidhiwa majukumu mazito ya kusimamia na kuitekeleza sheria ikiwemo kulinda usalama wa raia na mali zao, baadhi ya askari wake wanalichafua kwa kudaiwa kutenda matendo ambayo ni kinyume na sheria. Kashfa mpya iliyolifikia Uwazi ni ile ya malalamiko ya baadhi ya wananchi wa Kata ya Nyangao, Wilaya na Mkoa wa Lindi ambao wanamlalamikia askari mmoja wa jeshi hilo aliyetajwa kwa jina moja la Living.

 

VITENDO VYA UBABE

Madai hayo yanasema kuwa Living ambaye ni askari katika kituo kimoja cha polisi huko Nyangao anadaiwa kufanya vitendo vya ubabe hasa anapokuwa amekunywa pombe. Baadhi ya uhalifu anaodaiwa kuufanya Living na kuchafua jeshi hilo ni pamoja na kupiga watu ovyo.

 

WALIOSHAMBULIWA

Uwazi limeelezwa kuwa miongoni mwa watu walikumbana na kadhia hiyo ya kushambuliwa na askari huyo ni Ally Hassani, Selemani Bakari na wengineo.

 

Watu hao, Mei 9, mwaka huu, majira ya kati ya saa 5:00 na 6:00 usiku, wakiwa kwenye banda la kuuzia chipsi, walidai kushambuliwa kwa panga na afande huyo. Walidai kuwa, askari huyo alitishia kuua mtu akiwa na panga mkononi mwake.

 

Hassani, mmoja wa manusura wa tukio hilo alisema; “Tulikuwa tumeketi kijiweni, mahali panapotumika kuuzia chipsi, ghafla Living alifika na kuanza kutuhoji tulichokuwa tunaongea. “Wakati tukishangaa, yule askari alikunja shati na kunipiga shavu la kushoto, kitendo ambacho kilinichukiza mno.

 

“Nilichokifanya ni kujinasua kutoka mikononi mwake kisha kukimbia.” Hassan alisema kuwa, baada ya hapo askari huyo aliondoka eneo hilo hivyo kila mmoja akafikiri amekwenda nyumbani kwake kujipumzisha. Hassani ambaye katika tukio hilo alipata mchubuko kwenye mkono wake wa kushoto alisema ghafla walishangaa kumuona askari huyo akifikishwa mahali hapo akiwa katika bodaboda.

 

Alisema walipomtazama walimuona na panga mkononi ambapo alianza kumpiga nalo mgongoni na kumsababishia kudondoka chini. “Siyo siri nilipata maumivu makali baada ya kupigwa na lile panga, lakini nilifanikiwa kujiinua na kutimua mbio huku mkono wangu wa kushoto nikidhani ameukata kutokana na maumivu,” alisema.

 

Selemani Bakari, ambaye naye aliambulia kipigo kutoka kwa askari huyo alisema; “Baada ya Hassani kufanikiwa kukimbia, Living alinigeukia na kutangaza kuwa ataua mtu ambapo alinishambulia kwa kunipiga bapa la panga kwenye mbavu. “Hata hivyo, namshukuru Mungu kwani nilinusurika baada ya watu waliokuwa eneo la tukio kufanikiwa kumtuliza na kunyang’anya panga,”alisema Bakari.

 

Alisema kuwa baada ya kufanikiwa kumnyang’anya panga walilipeleka kwa Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Nyangao, Mohamedi Babu kisha walikwenda kuisalimisha silaha hiyo kituo cha polisi. Alisema baada ya kuisalimisha silaha hiyo walichukuliwa maelezo yao kisha walipatiwa fomu namba tatu (PF-3) kwa ajili ya kutibiwa.

 

MWENYEKITI AKIRI

Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Nyangao, Mohamedi Babu alipoulizwa na Uwazi kuhusiana na tukio hilo alikiri kupokea malalamiko ya wananchi dhidi ya askari huyo. “Ni kweli taarifa ya ukorofi wa askari huyo hapa kwetu ninazo,” alisema Babu na kusema tayari tukio hilo lipo polisi. Juhudi za kumpata Living ili kusikia upande wake hazikuzaa matunda.

 

KAMANDA WA POLISI LINDI

Alipotafutwa Kamanda wa Polisi mkoani wa Lindi, ACP Prodansiana Protas ili kujibu kashfa hiyo ya askari wake alisema hana taarifa hiyo na kuahidi kufuatilia. “Kimsingi sijaipata hiyo taarifa ndiyo kwanza ninaipata kutoka kwako, nashukuru kunipa na nitaifuatilia,” alisema kamanda huyo.

 

MAPYA ALIYEKATWA NYETI

Ukiachana na tukio hilo la askari kushambulia raia kwa panga, lile la kijana Wema wa mkoani Mara limeendelea kuibua mapya kutokana na kitendo cha kukatwa nyeti alichodai kufanyiwa kituo cha polisi.

 

Taarifa zilizolifikia Uwazi juzi zilieleza kuwa bado Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi ili kubaini ukweli wa madai ya kijana huyo kwani kwa upande wa Polisi wanakanusha kwa maelezo kuwa alijikata mwenyewe baada ya kukamatwa kwa tuhuma za ubakaji wa mama mmoja, mkazi wa Mtaa wa Majengo wilayani Bunda.

 

MAELEZO YA DAKTARI

Akizungumzia tukio hilo la mwanaume huyo kukatwa nyeti juu ya uwezekano wa kupata mtoto, daktari maarufu jijini Dar, Dk Godfrey Chale alisema inaweza kuwa vigumu kama sehemu nyeti yote imeondolewa.

 

“Labda kwa utaalamu zaidi wa kuchukua mbegu kwa njia ya sindano, jambo ambalo ni gumu sana kufanyika hapa nchini,”alisema Dk. Chale. Aliongeza kuwa, katika hali ya kawaida ni vigumu kwa mwanaume huyo kuweza kutoa mbegu kwa njia ya asili kwa sababu kinacholeta msukumo kuzifanya mbegu zitoke kwenye mifuko yake kimeondolewa.

Waandishi: Said Hauni, Lindi na Igenga Mtatiro, Mara.

WAZIRI MKUU Ashtukia Mchezo wa Maafisa Tarafa” Rudisheni Siku ya Usafi”


Loading...

Toa comment