The House of Favourite Newspapers

Kassim Kayira: Kutoka mkimbizi, baba n’tilie, BBC hadi Azam TV

0

14_04_kassimk_843Kassim Kayira.

Kassim Kayira, mtu ambaye hakuwahi kuwaza kama angeweza kuwa mtu tajiri na maarufu kama alivyo, kupitia uandishi wa habari na utangazaji, amepambana kujiweka mahali pazuri na sasa anapata kila kitu alichokosa utotoni na anasimulia maisha yake.

Wiki iliyopita, aliishia pale alipoacha kazi baada ya kuona mazingira siyo mazuri, kwamba aliundiwa zengwe baada ya kuanika ufisadi mkubwa uliofanywa na viongozi katika serikali ya Kagame, ikihusisha ununuzi wa magari ya kifahari.

Akaishia kueleza kuwa alikaa nyumbani kwa muda wa siku tatu tu kabla ya kupata kazi nzuri yenye mshahara mara mbili ya ule aliokuwa akilipwa hapo awali, Mungu alikuwa kazini.

SASA ENDELEA…

“Nilipata kazi kwenye shirika moja la kutetea Haki za Binadamu la Inter News, nikawa nazunguka kwenye magereza mbalimbali, mijini na vijijini kuzungumza na wafungwa, hususan waliofungwa kwa kuonewa na ukiukwaji wa haki za binadamu,” anasema Kayira.

“Kufikia hapo, umaarufu wangu ukazidi kuchanua kila kukicha, sasa nikawa napokea maoni kutoka sehemu mbalimbali za dunia, wakieleza jinsi walivyoguswa na kipindi hicho na namna nilivyokuwa nikitangaza,” anasema.

“Warembo wa Rwanda nao hawakuwa nyuma, ila kama nilivyosema hapo awali, mimi ni shehe, kwa hiyo imani yangu ilinilinda sana, hawakuweza kupenya lakini tabu ikabaki kwa mke wangu, hakuwa na amani kabisa na mazingira yangu ya umaarufu,” anasema Kayira na kuachia tabasamu hafifu la kujilazimisha.

“Zaidi ya hapo, sasa nikawa nimejietengenezea kundi kubwa la maadui, unajua kuna watu walifungwa kwa sababu za kiuonevu, kisa mtu ana pesa au mamlaka, anataka amuonee mtu, kwa hiyo nikawa navumbua uozo huo, watu wengi walirekebishiwa vifungo vyao na hatimaye kuwa huru kabisa,” anasema Kayira.

“Nikawa naishi kwa tahadhari sana, sikuwa namuamini mtu,” anaongezea Kayira.
“Nikafanya kazi hadi mwaka 2003, nikawaza kuongeza elimu kwanza, hivyo mimi na familia yangu tukahamia nchini Uingereza, katika Chuo cha Greenwich, nikachukua Masters in Journalism lengo nikujiwekea wigo mkubwa wa kielimu,” anasema Kayira.
“Kwa hiyo elimu yangu si ya kawaida kidogo na sasa najipanga kuchukua PhD katika sheria,” anaongezea Kayira.

“Maisha yalikuwaje nchini Uingereza?,” namuuliza huku nikiwa makini sana.
“Tofauti ni kubwa sana kule, gharama za maisha ni kubwa, mfano katika chakula hali ni mbaya zaidi, unaweza kununua ndizi pakiti moja, kwa shilingi 20,000 za Kitanzania, maisha yakawa ya tofauti kidogo, lakini sikuwa na jinsi zaidi ya kuendelea na mazingira hayo,” anasema Kayira.

“Nikasoma, lakini wakati naendelea na masomo, nikakutana na aliyekuwa mhariri mkubwa sana kwenye Shirika la BBC, upande wa redio akasema ananifahamu kwa hiyo alikuwa ananihitaji sana kwa upande wa redio, nikakubaliana naye na kuanza kazi BBC, lakini kwa upande wa Idara ya Kinyarwanda,” anasema Kayira.

“Idara ya Kinyarwanda? Sijaelewa kaka?” namuuliza nikitaka ufafanuzi zaidi.
“Yeah, kuna idara nyingi sana pale BBC, kuna idara inayohusika na Idhaa ya Kiswahili, Kifaransa, Kiingereza, Kinyarwanda na Kirundi, nilikaa zote hizo mbili kwa kuwa ni mtaalamu sana wa lugha hizo, nilizimudu kwelikweli,” anasema Kayira.

“Wakati naanza, yalikuwepo manyanyaso, dharau na kuonewa kutoka kwa mabosi wa humo ndani,” anasema Kayira.

“Mtu kwa kuwa tu ni mhariri au ana- kicheo fulani anaamua kukuonea na kujiona yeye ni muhimu na bora zaidi, lakini sikujali nikapiga kazi kama mwendawazimu, siku chache tu baadaye, waliokuwa wakinionea, wakawa wanahitaji utaalamu kutoka kwangu na hatimaye nikapandishwa cheo na kuwa bosi wao wote kwa kuwa nilikuwa na uwezo,” anasema Kayira.

“Nikwambie kitu, mtu akikuonea, hususan eneo la kazi, wala usijenge naye bifu au chuki, ulishawahi kuwaona kuku nyakati za asubuhi wakiwa wanaenda kujitafutia riziki?” anasema Kayira kwa mtindo wa swali.

“Yeah,” namjibu nikiwa na hamu kubwa ya kutaka kusikia alikusudia kusema nini.
“Kuku hutoka kwa mbwembwe na furaha kubwa sana, watakaa huko kutwa nzima wakitafuta chakula lakini ikifika jioni, lazima kuku hao warejee bandani,” anasema Kayira na kunitazama usoni huku akisikilizia kama nitamuuliza jambo. Hakuwa amekosea, ikabidi kuuliza.

“Unamaanisha nini kwa msemo huo kaka?” namuuliza huku nikijitengeneza vyema kwenye kiti kusikiliza maana halisi ya mfano wake.
Unataka kujua alimaanisha nini? Usikose kufuatilia wiki ijayo.

Leave A Reply