The House of Favourite Newspapers

Kauli ya Mwisho Mbongo Aliyeuawa Sauzi Inauma

0

MAMBO mawili yaliyoumiza wengi juu ya kifo cha Mtanzania, Shabani Ally aliyekutwa amefariki dunia ndani ya gari lake baada ya kupigwa risasi tano na wasiojulikana mjini Durban, Afrika Kusini ‘Sauzi’ ni; Moja, kauli yake ya mwisho na pili ni video ya tukio la mauaji hayo, Gazeti la IJUMAA WIKIENDA linakuhabarisha.

 

Chanzo cha habari kilimwambia mwandishi wetu kuwa, Shabani alizungumza na ndugu zake Jumamosi ya wiki iliyopita na kuwaahidi kuwa angekuja nchini Jumatano iliyopita, jambo ambalo halikutimia.

 

“Kauli ya mwisho ya marehemu kwa ndugu zake aliwaambia kuwa watulie anakuja nyumbani hivi karibuni, sasa wakikumbuka alivyowaambia watafurahi atakapofika, lakini sasa wanaumia sana na hasa mama yake analia kama mtoto. Alitegemea mwanaye atafika wiki iliyopita, lakini badala ya Shabani kuja, kilichokuja ni taarifa ya kifo chake.

 

“Walioleta habari ya kifo walituma na video (IJUMAA WIKIENDA limeiona video hiyo inayotisha) ikiuonesha mwili wa marehemu ukiwa umetapakaa damu ndani ya gari, ukiwa na majeraha makubwa kichwani na mwilini; kila aliyeitazama ni kama alipata uchungu mara mbili,” chanzo kilimwambia mwandishi wetu aliyefika Mabibo jijini Dar, nyumbani kwa marehemu Shabani kupata undani wa tukio hilo.

SIKIA KILIO CHA MAMA MZAZI

Mwandishi wetu alijaribu mara kadhaa kuzungumza na ndugu wa marehemu, lakini alishindwa kutokana na wengi kujawa na huzuni isiyokuwa na kifani.

Hata hivyo, mwandishi wetu alimsikia mama mzazi wa marehemu aitwaye Sarah Kubiga akilia kwa uchungu nyumbani hapo huku akisema;

 

“Siwezi kuongea jamani naumia sana, nina uchungu wa kifo cha mwanangu, kwa nini binadamu ni wabaya kiasi hiki jamani?

“Mwanangu umekwenda na kuniacha peke yangu, nilikuwa nakutegemea kwa kila kitu, lakini wamekuua.

 

“Kwa nini mmemuua mwanangu, kwa nini mlimuwekea target (shabaha), mwanangu ulijisikiaje wakati wanakudungua kama ndege wa porini?

“Ulijisikiaje kijana wangu, bora hata ungeumwa ningekuuguza, kuliko kuondoka ghafla namna hii, naumia mimi, naumia sana.”

 

KWA NINI SHABANI AMEUAWA?

Awali, taarifa zililifikia dawati letu kuwa Mbongo huyo ameuawa na watu ambao inadaiwa walikuwa katika mgogoro wa kibiashara ambao haukufahamika ni wa aina gani na ulihusisha nini?

“Jamani huyu ni Mtanzania (anaonyesha picha) alikuwa anaishi huko Afrika Kusini, alipigwa risasi tano na wenzake Jumapili ya Januari 26 (mwaka huu) kwa madai ya kwamba walikuwa wanadaiana (haikutajwa nani alikuwa anamdai mwenzake, ni Shabani au hao wauaji).

 

“Nilivyosikia kutoka kwa mtu aliyenipa taarifa alisema kuwa siku ya tukio hao jamaa walimpigia simu Shabani wakamuelekeza aende sehemu fulani iliyopo katika Mji wa Durban alikokuwa akiishi ili akachukue fedha zake,” alisema mtoa habari wetu ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini.

WIZARA YA MAMBO YA NJE INASEMAJE?

Tukio la kifo cha Shabani bado limejaa utata ambapo mwandishi wetu alilazimika kutafuta ukweli kutoka vyanzo mbalimbali lakini hakufanikiwa.

Ofisa Habari wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Emmanuel Buhohela alipoulizwa juu ya tukio hilo la Mtanzania kuuawa Sauzi alisema;

 

“Hapana, hili tukio bado sijalipata isipokuwa nakuahidi kuwa nitawasiliana na ubalozi wetu Afrika Kusini ili kupata ukweli ambao baadaye nitakujulisha.”

Hadi gazeti hili linakwenda mitamboni, taarifa zilizotufikia ni kwamba mwili wa marehemu ulikuwa unatarajia kufika nchini jana Jumapili kwa maziko ambayo yalitajwa kuwa yatafanyika mkoani Tanga.

Stori: Memorise Richard, Dar

Leave A Reply