The House of Favourite Newspapers

Director Kenny: Mungu Amenikutanisha na Mondi

0

MKALI kunako Bongo Flevani anayewakilisha vyema upande wa watayarishaji wa video kali za muziki huu, Kened Davi SangaDirector Kenny’ anaamini kilichotokea kwenye maisha yake ni Mungu tu!

 

Jamaa huyu juzikati alipeperusha kinoma bendera ya Taifa la Tanzania baada ya kutwaa Tuzo ya Video Bora ya Mwaka Afrika kwenye Tuzo za AFRIMA (All Africa Music Awards 2019), zilizotolewa nchini Nigeria.

Kenny amepiga stori na Over Ze Weekend ambapo amefunguka siri ya mafanikio yake kuwa ni Mungu ndiye anayemsimamia hadi amefika hapo alipo.

 

Kenny amechukua tuzo hiyo kupitia Ngoma ya Tetema ya mwanamuziki Raymond Mwakyusa ‘Rayvanny’ aliyomshirikisha bosi wake kunako Lebo ya Wasafi Classic Baby (WCB), Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’.

Kenny alianza kufanya video za Bongo Fleva mwaka 2015, akiwa chini ya Director Hanscana kama msaidizi wake.

 

Baada ya hapo, jamaa alijiongeza na kuanza kufanya kazi zake mwenyewe mwaka 2017 na sasa amefanikiwa kusimama vizuri na jina lake linajulikana Afrika.

Video yake ya kwanza ni Dede ya msanii wa WCB, Abdul Idd ‘Lava Lava’;

Over Ze Weekend: Ulianza lini kazi hii ya kutengeneza video?

 

Kenny: Nilianza kufanya kazi hii chini ya Director Hanscana, mwaka 2015 nikiwa kama msaidizi wake wa kubeba vitu wakati wa kazi. Baadaye niliongeza ujuzi, nikaanza kumsaidia kusanifu kazi hizo huku nikijifunza kuchanganya rangi na mwisho nikaanza kufanya kazi zangu mwenyewe. Nakumbuka nilianza na msanii Lava Lava kwenye Ngoma ya Dede ambayo ilinifungulia milango kiasi cha kumfanya Diamond (Mondi) anione na kutamani kufanya kazi na mimi.

 

Over Ze Weekend: Baada ya kukutana na Mondi ikawaje?

Kenny: Baada ya kuiona ile kazi na kuipenda, basi akataka tufanye kazi pamoja ndipo tulipoamua kufungua Kampuni ya Zoom Production. Kampuni hii ilikumbana na changamoto nyingi mno hadi kusimama na watu kuiamini, lakini tunamshukuru Mungu alitusimamia ikawa ni moja ya kampuni nzuri na kubwa ya utayarishaji wa video nchini Tanzania na barani Afrika. Ninaamini ni Mungu tu ndiye aliyenikutanisha na Mondi.

 

Over Ze Weekend: Umepenyaje na kuanza kujulikana nje ya mipaka ya Tanzania na kuingia kwenye kinyang’anyiro cha Tuzo za AFRIMA za Nigeria?

 

Kenny: Kwanza ninamshukuru sana Mondi kwani ni mmoja wa watu waliochangia ukubwa wangu ndani na nje ya nchi kimuziki. Mondi amechangia kwa kiasi kikubwa mno kazi zangu kuonekana kwani anafuatiliwa na watu wengi duniani. Kama unavyojua watu huwa wanapenda vitu vikali hivyo walianza kuvutiwa na kazi ninazofanya na Mondi, na hapo ndipo nilipoanza kutambulika nje ya Tanzania kupitia kazi zangu.

Over Ze Weekend: Vipi kuhusu ndugu, jamaa na marafiki, wana mchango wowote kwenye tuzo hii uliyopata?

Kenny: Ninawashukuru ndugu, jamaa na marafiki, ila zaidi ni familia yangu. Nimepata sapoti kubwa sana kutoka kwao kwa kunisihi hasa nipambane bila kukata tamaa kwenye kazi yangu na kweli nilisikiliza asilimia kubwa ya ushauri wao na ndiyo maana leo niko hapa.

 

Over Ze Weekend: Nini siri ya mafanikio yako kwenye safari yako hii?

Kenny: Siri ya mafanikio si nyingine, ni Mungu tu; yaani nilimtanguliza Mungu wangu mbele, sala zilikuwa nyingi na Mungu akasikia maombi yangu.

Over Ze Weekend: Hebu tueleze kidogo, mpenzi wako baada ya kusikia umepata tuzo hii alikuwa kwenye hali gani?

 

Kenny: Kwanza, ninaweza kusema mchango wake kwa kiasi kikubwa umesababisha mimi kuwa hapa nilipo kwani alikuwa tayari kufanya lolote kwenye kazi yangu, ikiwa ni pamoja na kunisaidia kusambaza kazi hizo na mengine mengi. Ninaweza kusema alikuwa na furaha iliyopitiliza baada ya kuona kuwa hakupoteza nguvu zake kunisapoti.

 

Over Ze Weekend: Unawaambia nini vijana wenzako ambao wanaochipukia kwenye tasnia hii na wana ndoto kama yako?

 

Kenny: Ninawasihi vijana wenzangu wapambane sana, wasimsahau Mungu na cha mwisho kabisa ni kuwa na nidhamu na heshima katika kazi. Hivyo ndivyo vitu vinavyonibeba mimi na vinabeba thamani ya mtu pamoja na kazi yake na watu watampenda mtu huyo na kutaka kufanya naye kazi. 

MAKALA: AMMAR MASIMBA

Leave A Reply